Wakati wananchi katika visiwa vya Zanzibar wanalalamikia kupanda kwa bei za mahitaji muhimu ikiwemo vyakula, serikali katika visiwa hivyo imepandisha bei ya umeme kwa asilimia 85 ambapo wananchi watalazimika kulipia huduma ya umeme kuanzia tarehe mosi mezi ujao. Zanzibar yenye idadi ya watu wanaokisiwa zaidi ya million moja, ina watumiaji wa umeme zaidi ya laki moja na elfu tano.
Kasi ya matumizi ya Umeme Zanzibar imekuwa ukiongezeka kila mara kutokana na matumizi ya nishati hiyo kuongezeka pamoja na kampeni za kutaka wananchi watumie zaidi umeme na kupunguza ukataji miti ili kuepuka uharibifu wa mazingira.
Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Hassan Ali Mbarouk akitangaza hatua hiyo mbele ya waandishi wa habari ambapo alisema bei mpya itaanza kutumika Juni 1, mwaka huu.
Alisema shirika limepandisha bei kwa watumiaji wote kwamba bei hiyo mpya imepangwa katika viwango vya makundi matano.
Alisema makundi hayo ni pamoja na huduma ya kiwango cha kiwango cha uwezo mdogo, huduma ya jamii, viwanda vidogo, viwanda vya kati na vikubwa na taa za barabarani.
Mbarouk alisema kuamnzia Juni 1, umeme utauzwa shilingi 66 kwa uniti badala ya shilingi 50, kwa watumiaji wa kiwango cha uwezo mdogo.
Alisema watumiaji wa huduma ya jamii watalipa shilingi 161 kwa uniti badala ya bei ya sasa ya shilingi 120 na watumiaji wa kiwango cha viwanda wanunua umeme kwa bei mpya ya shilingi 172.00 kwa uniti badala ya shilingi 140.00.
Alisema watumiaji wa kiwango cha viwanda vya kati na vikubwa watalipa shilingi 169.00 badala ya shilingi 140.00 kabla ya bei mpya na kwamba gharama ya umeme wa taa za barabarani umepanda kufikia shilingi 141.00 kwa uniti kutoka bei ya shilingi 105.00.
Mbarouk alisema ongezeko la bei mpya litafanyika katika awamu tatu kabla ya kufikia lengo la kuongeza gharama ya huduma hiyo kwa asilimia 85.
Alisema katika utekelezaji wa awamu ya kwanza umeme utapanda kwa asilimia 40, awamu ya pili bei itaongezeka kwa asilimia 30 na ya tatu pia kwa asilimia 30.
Alipoulizwa sababu za ongezeko hilo, Mbarouk alisema shirika limechukua uamuzi huo kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji.
Ni kipindi ambacho sauti za wananchi kulalamikia kupanda ovyo kwa bei imekuwa ikiongozeka, lakini viongozi wa serikali wanasema kwamba hali za bei visiwani bado ni nafuu sana kulinganisha na nchi jirani.
Licha ya maelezo ya viongozi wa serikali, wananchi wanasema kuwa serikali haijaweza kujipanga vizuri ili kudhibiti mfumko wa bei wa bidhaa muhimu, hali ambayo inawaathiri wananchi wengi masikini na sasa kuongezeka bei ya umeme lakini Meneja wa shirika la umeme anasema pamoja na kupanda kwa bei za umeme Zanzibar, wananchi watalipia bei mpya kwa awamu tatu.
Zanzibar inanunuwa umeme wake kutoka Tanzania bara kupitia mkonga (Waya) wa umeme unaopita chini ya bahari hadi katika kisiwa cha Unguja na Pemba.
Hata hivyo waya unaoleta umeme Unguja umechakaa, na serikali kwa msaada wa Dola za Kimarikani milioni 72 kutoka serikali ya Marekani inafanya juhudi za kuweka waya mpya.
Licha ya Zanzibar imo katika juhudi za kutafuta vyanzo vyengine vya umeme mfano matumizi ya nguvu za jua na upepo na wawekezaji kadhaa kutoka nje tayari wamejitokeza. Lakini bado itaendelea kuitegemea Shirika la Tanesco la Tanzania bara.
No comments:
Post a Comment