Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Tuesday, May 29, 2012

Viongozi wakutana, hali bado ni tete


Waziri wa Mambo ya Ndani Emmanuel Nchimbi na Mkuu wa jeshi la polisi Tanzania Inspekta Jenerali Said Ali Mwema wakizungumza katika kikao cha pamoja kati yao na viongozi wa dini na serikali, haja ya kurejesha hali ya utulivu Zanzibar
HALI bado ni tete katika visiwa vya Zanzibar kwa baadhi ya maeneo ambayo vitendo vya uvunjifu wa amani vinaendelea licha ya juhudi za kutaka kurejesha hali ya amani nchini. Juhudi za pamoja zimeanza kuchukuliwa katika kurejesha hali ya utulivu Zanzibar baada ya machafuko ya siku mbili zilizopita zilizosababishwa na wafuasi wa Uamsho na jeshi la polisi na kusababisha hasara za mimilioni ya fedha na uharibifu wa mali.
Kikao cha pamoja kilichowashirikisha waziri wa mambo ya ndani Tanzania, Emmanuel Nchimbi, mkuu wa jeshi la polisi Said Mwema na viongozi wa taasisi za kiislamu Zanzibar jana walikubaliana kufanya kazi kwa pamoja ili kurejesha hali ya amani.
Katika mkutano huo uliofanyika katika makao makuu ya polisi ziwani zanzibar na pia kuwashirikisha maafisa wa sekta ya utalii na baadhi ya maafisa wa kibalozi kutoka Marekani, Ungereza na Norway. Waziri Nchimbi alisisitiza kuwa suala la kulinda amani ni la wote na akawataka viongozi wote wa kidini na wanasiasa kuhakikisha Zanzibar inaendelea kuwa na amani.
“Kwa mwaka mmoja na nusu hivi sasa serikali ya umoja wa kitaifa imefanya kazi nzuri na tunawapongeza viongozi wote kwa kazi hiyo, rais Dk Shein, Makamu wake wa kwanza Maalim Seif na makamo wake wa balozi Seif Ali Idd, sasa tusiwavunje moyo” alisema Nchimbi.
Alisema kuendelea kwa vurugu Zanzibar ni kuonesha viongozi hao wameshindwa kazi jambo ambalo sio sahihi na kwamba vurugu zinaweza kusababisha watalii kuondoka kabisa nchini na hasa kwa kuzingatia kipindi hiki cha msimu wa utalii kukaribia.
Kikao hicho ambacho waandishi wa habari walihudhuria, Nchimbi alisema ujio wake Zanzibar ulilenga katika mambo matatu muhimu ambapo aliyataja mambo hayo kuwa ni kuwahakikishia wazanzibari wote kuwa jeshi la polisi ni lao na litaendelea kuwalinda.
Jambo la pili alisema ni kwamba viongozi wote wa dini na siasa wana jukumu kubwa la kusaidia kujenga mazingira ya utulivu na amani Zanzibar.
Aidha Waziri Nchimbi katika mambo ambayo alihimiza ni kuagiza jeshi la polisi kuchukua hatua ili kuhakikisha kwamba watu wote walihusika na vurugu hizo kuchukulia hatua za kisheria.
Mkuu wa Polisi Tanzania Jenerali, Said Mwema aliahidi kushirikiana na viongozi wa taasisi za kidini ili kuendeleza amani na utulivu nchini.
Alisema kwamba majadiliano na mazungumzo ni muhimu katika kuimarisha amani na kutatua migogoro iliyokuwepo na kwamba kwa nafasi yake ataendelea kubali Zanzibar.
“Vurugu hazisaidii kujenga lakini matumizi ya nguvu pia tunajitahidi kuyaepuka, na katika kuhakikisha mashirikiano yanaendelea mimi nitabakia Zanzibar kwa muda ili kujenga mawasiliano na programu maalumu za ulinzi shirikishi” alisema Mwema.
Kwa upande wa taasisi za kidini walishauri jeshi la polisi katika kujenga mashirikiano na kuepuka michafuko kama hiyo yaliyotokea na kutumia busara wakati wanapotekeleza majukumu yao.
Dk Mohammed Hafidh Khalfan ni kiongozi wa Umoja Kiislamu, wa Elimu, Uchumi na Maendeleo (UKUEM) aliwataka jeshi la polisi kuepuka matumizi ya nguvu wanapotekeleza majumu yao.
Alisema kwamba taasisi yake pamoja na taasisi nyengine za kiislamu zitatumia juhudi na busara za kuwafanya waumini waepukane na vitendo vya fujo kwa sababu fujo inatoa fursa kwa wahalifu kufanya vitendo vya uharibu wa mali na wizi.
Katika kikao hicho ambacho Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) hawakushirikishwa ambapo Dk Hafidh alishauri kikao kama hicho sauti zao ni muhimu kusikika kwani baadhi ya mambo wangeweza kuyatolea maelezo.
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) Muhidin Zubeir Muhidin ambaye alifanya juhudi za kuwasiliana na polisi na taasisi nyengine katika kutafuta suluhu za machaguko yaliotokea hapa Zanzibar aliahidi kuendelea na mashirikiano na wadau wote wa amani nchini.
“Sote tunajukumu la kuhakikisha hali ya amani inarudi Zanzibar na kwamba, Uislamu hautoi nafasi kwa kufanya uharibifu wala kumdhuru mtu” alisema Sheikh Muhidin.
Kwa upande wao Maafisa wa Mabalozi kutoka Marekani, Uongezeza na Norway ambao walialikwa kama wasikilizaji katika mkutano huo walishukuru ushirikiano kati ya taasisi za serikali katika juhudi za kurejesha amani.
Mkurugenzi wa Utalii Zanzibar, Ali Khalil Mirza alisema sekta ya utalii inachangia pato kubwa la taifa kwa zaidi ya asilimia 75 inaweza kutetereka iwapo hali ya utulivu itatoweka nchini na hivyo kushauri mashirikiano zaidi kati ya taasisi zote na wadau ili kuimarisha hali ya utulivu nchini.
Wiki iliyopita baadhi ya watu wanaosaidikiwa kuwa ni wafuasi wa uamsho walikusanyika katika makamo makuu ya polisi ya mjini magharibi kupinga kukamatwa kwa miongoni mwa wanaharakati wa jumuiya ya uamsho na mihadhara ya kiislamu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment