Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Friday, May 11, 2012

maalim seif atoa somo la muungano




KATIKA kuondosha manunguniko juu ya Muungano wa serikali mbili ya Tanzania na Zanzibar, njia pekee ya kuondosha hilo ni kujitokeza kwa wingi katika kutoa maoni wakati wa mchakato wa uundwaji wa katiba mpya. Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad jana alipokuwa akihutubia kwenye mikutano ya hadhara ya Chama cha Wananchi CUF huko Kisiwa Panza na Wambaa, Mkoa wa Kusini Pemba ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka wazanzibari bila ya woga kutoa maoni yao ili kupata Muungano usiokuwa na manung’uniko na wenye kujali maslahi ya pande zote.Alisema wananchi wenyewe ndio wenye maamuzi juu ya aina ipi ya Muungano wanaoutaka, iwe wa serikali mbili, tatu, moja au aina nyenginezo, ikiwemo Muungano wa Mkataba.  Akifafanua aina hiyo ya Muungano wa mkataba kwa wanachama, wafuasi CUF na wananchi waliohudhuria kwa wingi katika mikutano hiyo, alisema mnaweza kuwa na serikali mbili ambazo kila moja inakuwa na mamlaka kamili, na baadaye kuwe na mkataba kati yao hizo, juu ya baadhi ya mambo wanayokubaliana yawe ya pamoja.
Alifahamisha chini ya utaratibu kama huo, kila serikali inakuwa na mamlaka kamili, ikiwemo kiti katika Umoja wa Mataifa, lakini katika baadhi ya mambo wanayokubaliana yawe ya pamoja wanawekeana mikataba ya kuyaendesha na kuyasimamia.
Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema Muungano wa aina hiyo hivi sasa umekuwa maarufu na hata nchi 27 zinazounda Umoja wa Ulaya (EU) zimeamua kuwa na utaratibu huo, na zinaenda vizuri bila ya matatizo.  Alitoa mfano, licha ya kuwa na Muungano huo, nchi hizo wanachama bado huwa na uhuru na maamuzi yao kamili na kwa mfano EU zimekubaliana baadhi ya mambo, kama vile kuwa na sarafu ya pamoja, lakini hata hilo, Uingereza ambayo ni mwanachama haijaingia kwenye sarafu hiyo.



“Hatafungwa mtu wala kunyanyaswa kwa kutoa maoni ya Muungano anaotaka, hatuhitaji kuwa na Muungano wa karatasi ambao haumo katika mioyo ya watu lakini tunataka kila mmoja atoe maoni yake huru kabisa”, alisisitiza Maalim Seif.
Maalim Seif alisema kwa Wazanzibari ambao tayari wana katiba yao, suala la Muungano ndilo jambo muhimu na linalowagusa zaidi katika kuandika katiba mpya, hivyo ni jukumu lao wajiandae vizuri juu ya hilo. Aidha aliwahimiza wananchi kuitumia fursa hiyo kikamilifu kumaliza kilio chao cha muda mrefu ndani ya Muungano. Na kusema Wazanzibari wakiwa na sauti moja katika kumaliza malalamiko yao ndani ya Muungano, itakuwa jambo zuri zaidi.
Makamu wa Kwanza wa Rais alisema baada ya hatua ya wiki iliyopita kwa Rais Kikwete kuitangaza Tume hiyo, karibuni inatarajiwa itaanza kupita mitaani kuchukua maoni ya wananchi.
Alieleza kuwa huo utakuwa wakati wa Wazanzibari kujitokeza kikamilifu na waitikie wito aliokwisha utoa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein alipowataka wananchi wajitokeze kutoa maoni bila ya woga.

No comments:

Post a Comment