Waislam Tunapaswa Kubadilika Sasa.
Assalamu Alaikum Wa Rahmatu Allah Wa Barakatuh
Ndugu zangu katika imaan, mara nyingi nimekuwa nikisoma malalamiko
mengi sana kutoka upande wetu sisi Waislam. Kiasi ambacho sasa imekuwa
kama wimbo usiochezeka tena.
Kwanini nasema hivyo, nina sababu nyingi lakini hapa ninaweza kuelezea zile chache amabazo nitajaaliwa kuzieleza Insha’Allah.
Waislam leo inaonekana kama ni watu ambao wapo nyuma kimaendeleo,
kimasomo na kwenye kila Nyanja za kimaisha, japokuwa kwa mtu mmoja mmoja
inaonekana kama waislam tuna maendeleo makubwa, ili linaweza kuwa kweli
kwa sababu mambo mengi ambayo sisi Waislam tunayafanya yanakuwa kama
hayana Baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ukiudhuria mihadhara mingi
ukosi kusikia malalamiko kutoka kwa waadhiri kuwa Waislam tunanyanyaswa
na kuonewa, lakini hapo hapo tunashindwa kujiangalia sisi wenyewe
Waislam, tumefanya nini au tunafanya jitihada gani katika kujikwamua
katika matatizo haya na hapo hapo kufuata mafundisho ya dini yetu.
Wakati mwingine nahisi hii ni kama dalili za adhabu kwetu, maana Waislam
tumekuwa hatuna tofauti na hao Wakristo, Wapagani na wale wasio amini
kuwepo kwa Mwenyezi Mungu. Hizi rehma na riziki ambazo tunazipata mi
nahisi ni kwa sababu kuna viumbe vingine ambavyo havina makosa, kama
vile wanyama na mimea, kutokana na hao ndio na sisi tunafaidika.
Waislam ndio tunaongoza kwenye mambo mengi ya kipuuzi, utakuta waimbaji
wazuri kwenye miziki ni waislam, kwenye uhuni wa kufuta bangi, madawa
ya kulevya na ulevi mwingine, waislam tunaongoza, kiasi hata hao
wakristo uwa wanatufanyia istizahi kuwa mbona mwezi wa ramadhani mabaa
na maeneo yanauza nyama ya nguruwe (kiti moto) uwa yanakosa wateja na
hayajazi kama miezi mingine. Mbona tunapomaliza mfungo ndio mabaa na
majumba ya kufanyia ngono ndio yanafurika?
Si ajabu leo kumkuta
Muislam akisema uongo ili apate pesa, kazi au biashara, leo hii Muislam
yupo radhi kwenda kwenye shirki ili aweze kufanikiwa kwenye biashara
zake. Waislam sisi tupo sawa na hao wasio amini kwenye makatazo mengi,
leo hii sisi ndio matajiri na pesa zetu zipo kwenye mabenki yenye kutoa
riba. Hatuwaangalii watoto yatima, kiasi tumewapa majina kama vile
Machokoraa au watoto wa mitaani, mimi binafsi sijawahi kuona mitaa
ikizaa watoto, lakini ndivyo tunavyo waita.
Matajiri wamekaa
kwenye majumba yao wakila na kusaza na haya wanayajuwa na hata kuonyesha
mfano wa kufungua kituo cha kulelea watoto ili kesho na kesho kutwa
waje kuwa watu wema wanashindwa, hivi tutakuja kusema nini kesho
tutakapo simama mbele ya Mwenyezi Mungu?
Waislam tunapaswa
kubadilika, maana Mwenyezi Mungu awezi kubadilisha hali zetu mpaka sisi
wenyewe tuchukue hatua za makusudi kabisa na kufanya jitihada za dhati
ndipo naye Mwenyezi Mungu atatufungulia milango yake ya Rehma na Uislam
utasimama tena.
Wakati wa kukaa vibarazani na kwenye mimbari na
uku tukilaumu mfumo kristo, bila ya kuchukuwa hatua madhubuti za
kupigania jihadi ya nafsi zetu, hazita tufikisha popote. Mfumo wowote m
baya uondoka pale tu wahathirika wakuu watakapokuwa kweli wameamini ki
kweli kweli na kuwa ni Waislam wa kweli na si Waislam kwa majina na
mavazi tu. Wakati ndio huu, hatuja chelewa bado, turejee kwenye Uislam
aliotuachia Mtume (s.a.w) na si kuhadaika na mifumo ya kidunia, mifumo
ambayo inatutenga sisi Waislam.
Badala yake sisi wenyewe
Waislam ndio tumekuwa watu wa mbele kuiendeleza nifumo hiyo ambayo leo
inatuwacha nyuma. Sisi wenyewe ndio tunaondoa Uislam katika taaluma
zetu. Sisi Waislam ndio wenye majumba ya ufuska; kama vile mabaa, vilabu
vya usiku pamoja na kila kitu ambacho kipo nje ya itikadi na maadili.
Hali hii inapelekea athari za Qur`an na Sunna za Mtume kufichika katika
maisha ya kijamii kama si kuhama kabisa. Hata lugha ambayo Qur’an ndio
inaitumia yaani Kiarabu tunaitupa na ndio sisi hao hao tumekuwa mahodari
katika kutoa fatwa mbali mbali.
Ndio maana kikawa kizazi hiki
hakijishughulishi na dini wala maadili mema. Hiyo ni natija ya ufisadi
wa nafsi zetu wenyewe maana watoto zetu tunawalea na wanakulia kwenye
mitandao ya internet na video game.
Hakika tumeshafanya makosa
na tunaendelea kufanya makosa, tunajitenga na tabia za Kiislam na
tunarithisha mambo mabaya kwa kizazi chetu kwa maana ya watoto zetu.
Hakika tunakitenga kizazi na Uislam. Hawakukosea wale waliosema: "mtoto
umleavyo ndivyo akuavyo."
Wengi wanaweza kutaka kujuwa dawa yake ni nini kwa hali hii tulio nayo hivi sasa?
Kwa kweli jibu la swali hili si la kulijibu mimi, mimi ni kama mchokozi
na mchokonoaji wa hoja, mambo haya yanataka wasomi na Masheikh
waliobobea wenye akili kubwa zenye ikhlas. Wakae na kuamua nini cha
kufanya na nini cha kutuambia sisi maamuma wao. Kwa kweli tunapaswa kula
chakula cha roho, chakula ambacho kitaweza kurutubisha mioyo yetu na
kumrejea Mwenyezi Mungu, maana yeye ni Mwingi wa rehma na Mwingi wa
Msamaha, na Mwenyezi Mungu hashindwi kufanya Qur`an, sharia yake na
maadili yake, kuwa ndiyo inayotawala leo.
Lakini ni juu yetu
kufanya juhudi kadiri ya uwezo wetu, wala tusingoje muujiza wa mbinguni.
Na kazi ambayo tunaweza kuifanya, nionavyo mimi, ni: kwanza, tuitilie
mkazo elimu ya dini ya Kiislam katika mashule, hasa Qur`an, kuisoma,
kuihifadhi na kuifasiri. Kwani hiyo ndiyo msingi. Basi ni juu yetu
kuwapeleka watoto zetu kwenye mashule ya Kiislam na kufuatilia kile
wanacho fundishwa na tukishindwa basi tuwapeleke madrasa, ili uko wapate
kujifunza misingi ya dini yetu.
Pili, kila mmoja katika watu
wa dini atekeleze wajibu wake kwa ikhlasi, na kujiandaa kuwa kiongozi
mwenye mwamko, anayejua namna ya kuwakinaisha vijana kuwa dini ndio
chimbuko la msimamo ulio sawa, ambalo litawapa maisha mema zaidi.
Tatu, kuufafanua uhakika wa dini, kuufanya mwepesi kufahamika na
kuutangaza kwa kutumia vitabu, hotuba, Tovuti baraza, blog, makala na
matoleo mbalimbali. Tumthibitishie mjinga na mwenye shaka kuwa Uislamu,
kwa sharia na maadili yake, unatosheleza kabisa mahitaji ya mwanaadamu
ya kiroho na ya kimaada; na unaweza kutatua matatizo yake; na kwamba una
lengo la kumfanya afaulu katika dunia yake na akhera yake.
Kuzibadilisha nasfi zetu kunahitaji juhudi na jihadi ndefu, zenye
kutuweka kwenye mitihani na majaribu mengi; kama juhudi aliyoifanya
Mtume (s.a.w) katika kubadilisha ada za kijahiliya na itikadi zao. Mtume
(s.a.w) anasema hivi: "Uislamu ulianza katika hali ya ugeni, na utarudi
katika hali ya ugeni kama ulivyoanza."
Kwa hiyo, hatuwezi
kuepukana na ugeni wake kwani Uislam ni mpana sana na tunatakiwa kufanya
jitahada za makusudi kabisa kuambatana nao, ni wajibu wetu sisi wenyewe
kuamua kwa dhati kabisa kuifanya Qur`an, ndio Mwongozo wetu na si
kimaneno tu, hata tabia zetu ziendane kama tunavyo fundishwa kwenye
Qur'an na Sunna. Maana tunafundihswa na Mtukufu wa darja kuwa, ukiona
jambo baya liondowe kwa mkono wako, kama huwezi basi lisemee watu
wasikie kama hili baya, Jambo la mwisho kama hayo yote uwezi basi
angalau lichukie kwenye moyo wako na hili la kuchukia ni katika Imani
dhaifu sana, na imani dhaifu ndio tuliokuwa nayo sisi Waislam leo.
Na kuna kauli moja inasema hivi, dalili za mtu mnafiki ni tatu,
anaposema anaongopa, anapotoa ahadi hatimizi/anaivunja, anapoaminiwa na
amana hufanya khiyana. Na dalili zote hizo zipo kwa Waislam sisi.
Tunashindwa kuondoa ufisadi na kwenye nafsi zetu, kwenye majumba yetu,
kwenye biashara zetu, ili hali haya yote yapo ndani ya uwezo wetu,
tunacho kijuwa sisi ni kulalamika ili hali haya yote tunayatengeneza
sisi wenyewe
No comments:
Post a Comment