Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Thursday, July 26, 2012

Vifo vya Mv. Skgit, wahusika washitakiwa kwa makosa 60 ya mauaji




Miili ya watu waliokolewa jana katika ajali iliyotolea jumatano iliyopita
ya Mv. Skagit ambayo imeuwa watu zaidi ya 70
WATU watatatu wanaomiliki Kampuni ya Meli ya Seagul, wamefikishwa katika mahakamani wakikabiliwa na mashitaka 60 ya mauwaji. Washitakiwa hao wanadaiwa kuhusika na mashitaka hayo, kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya Mv. Skagit iliyotokea Julai 18 mwaka huu, karibu na maeneo ya kisiwa cha Chumbe.
Walioshitakiwa ni Mussa Makame Mussa (49) mkaazi wa Kazule, ambaye ni Kepteni wa meli hiyo, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Said Abdulrahman Juma (46) wa Mwembetanga, pamoja na Meneja wa tawi la Dar es salaam Omar Hassan Mkonje (50) mkaazi wa Magomeni.
Wote hao wamefikishwa mbele ya Naibu Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar Ali Ameir Haji, na kusomewa mashitaka ya kuua bila ya kukusudia kinyume na vifungu vya 195 na 198 vya kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
Mashitaka hayo yalisomwa mahakamani hapo na Wanasheria wa serikali Suleiman Massoud Juma na Sabra Mselem Khamis, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Wanasheria hao waliiambia mahakama hiyo kwa kudai kuwa, watuhumiwa wote hao majira ya saa 7:30 za mchana wa Julai 18 mwaka huu walisababisha vifo vya watu 60 katika maeneo ya kisiwa cha Chumbe wilaya ya Magharibi Unguja.
Kwa mujibu wa maelezo ya mashitaka hayo yaliyosomwa na Suleiman Massoud Juma, washitakiwa hao wakiwa na dhamana na majukumu ya kuchukua abiria na mizigo yao, kwa uzembe walishindwa kuchukua tahadhari katika majukumu yao pasi na kuzingatia usalama wa tahadhari kwa abiria na kusababisha meli hiyo kuzama na kuua.
Miongoni mwa watu waliotakiwa kufariki katika ajali hiyo ni Omar Khamis Hamza, Kulthumu Haji Khamis, Rahma Ali Abdallah, Husna Ali Khamis, Mwanaidi Abdallah Ramadhan, Idd Mahmoud Omar, Batuli Abdulrahman Ame, Batuli Abdulrahman Amri, Halima Sharif Abdallah pamoja na Husna Ali Salum.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kuhusiana na maelezo hayo ya upande wa mashitaka, kutokana na kwamba mahakama hiyo iliyo chini ya Naibu Mrajis hana dhamana ya kusikiliza kesi za aina hiyo.
Badala yake Naibu Mrajis alifamisha kuwa washitakiwa hao watajibu mashitaka hayo mbele ya Mahakama Kuu Zanzibar, watakapofikishwa mara baada ya upelelezi wake kukamilika.
Mara baada ya maelezo hayo ya mahakama, upande wa mashitaka ulioongozwa na Sabra Mselem Khamis uliiambia mahakama hiyo kwa kudai kuwa upelelezi wake bado haujakamilika.
Hivyo wameiomba mahakama hiyo kuiahirisha kesi hiyo na kuipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa.
Upande wa utetezi ulisimamiwa na Mawakili wa Kujitegemea Abdallah Juma na Rajab Abdalla Rajab kutoka Kampuni ya AJM Solicitor & Advocate Chamber ya Mjini Zanzibar uliiomba mahakama hiyo iwapatie dhamana wateja wao.
Walifahamisha kuwa, ijapokuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, lakini uwezo wa kutoa dhamana kwa washitakiwa hao unao, na kuomba masharti hayo yawe mepesi yatakayoweza kutekelezeka, ombi ambalo upande wa mashitaka haukuwa na pingamizi na uwamuzi utakaotolewa na mahakama hiyo.
Naibu Mrajis aliwataka washitakiwa hao kila mmoja kujidhamini kwa fedha taslimu shilingi 5,000,000 pamoja na wadhamini wawili wenye vitambulisho watakaosaini bondi ya kiwango kama hicho cha fedha kila mmoja, na mmoja kati ya wadhamini hao awe ni mfanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Wakili wa upande wa utetezi Abdallah Juma, aliiambia mahakama hiyo kuwa masharti hayo ni magumu kutekelezeka kwa wateja wake, na kuomba iwaondolee fedha taslimu badala yake iwaekee maandishi na wako tayari kuwasilisha warka wa mali zisizohamishika.
Sambamba na hilo, ameiomba mahakama iwaondolee sharti la kuwa na mdhamini mwajiri wa serikali, na badala yake waekewe mdhamini madhubuti, ombi ambalo mahakama hiyo ililikataa na kutaka watekeleze masharti hayo, ijapo kuwa upande wa mashitaka haukupinga hoja hizo kwa madai kuwa wanaiachia mahakama katika maamuzi yake.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 8 mwaka huu kwa kutajwa, na hadi mwandishi wa habari hizi anaondoka mahakamani hapo watuhumiwa hao walikuwa bado hawajatekeleza masharti hayo ya dhamana.

No comments:

Post a Comment