Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Monday, July 23, 2012

Miili 76 kuzikwa baharini


Askari wa Jeshi la wananchi(JWTZ)wakiwa katika Bandari ya Zanzibar 
 wakisubiri bila mafanikio miili ya watu walizozama na Meli ya 
Mv. Skagit kabla ya zoezi hilo kusitishwa rasmi na Serikari kupitia
 kwa makamu wa Pili wa Raisi Seif Ali Iddi jana

SERIKALI imesitisha rasmi zoezi la uokoaji wa miili ya watu waliozama katika ajali boti ya Mv Skagit Jumatano iliyopita kutokana na ugumu wa kazi hiyo, huku miili zaidi ya 76 ikipotea baharini. Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Idd alisema hayo wakati akipokea msaada kutoka Benki ya NMB kwa ajili ya waathirika wa ajali hiyo.
Alisema wataalamu waliokwenda kwenye eneo la ajali kwa ajili ya uokoaji wamethibitisha kutopata mwili hata mmoja kwa muda siku mbili, hivyo Serikali imeamua kusitisha zoezi hilo.
“ Tumeamua siku ya kesho (leo) kusoma hitima kwenye misikiti yote ya Unguja na Pemba, lakini kitaifa hitima hiyo itasomwa katika Msikiti wa Mwembeshauri eneo la Rahaleo mjini Zanzibar,” alisema.
Alisema hitima hiyo itafanyika kwenye misikiti mikuu na kwamba katika mikoa yote hitima hiyo itafanyika saa 7.00 baada ya Sala ya Adhuhuri.
Kabla ya kauli hiyo ya Serikali, Jana ilikuwa siku ya nne kufanyika kwa zoezi la kutafuta maiti katika Bahari ya Hindi lakini waokoaji walirejea majira ya jioni bila ya maiti yoyote.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema waliokwenda katika uokozi huo walirejea bila kupata maiti hata moja.
Kati ya watu 290 waliokuwa wamepanda kwenye boti hiyo, ni 146 ndio waliookolewa wakiwa hai huku maiti 68 zikiopolewa baharini ambapo Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Vyombo vya Baharini, Abdalah Hussein Kombo alisema pia zoezi la uokoaji ni gumu.
Awali, mmoja wa wazimiaji ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema : “ Meli inaonekana lakini namna ya kuipindua ili kuziondoa maiti zilizopo tumeshindwa kwa sababu ya ukosefu wa vifaa.”
Katika hatua nyengine Chama cha NCCR-Mageuzi, kimetaka mfumo wa vyombo vya usafiri katika visiwa vya Zanzibar na Pemba kuangaliwa upya ili kuepusha maafa zaidi kutokana na ukweli kuwa hata ndege zinazofanya safari zake katika visiwa hivyo na Dar es Salaam zina walakini.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema, licha ya boti na meli ambazo hazipo katika viwango vya usalama lakini pia ndege zinazofanya safari kati ya Pemba na Dar es Salaam usalama wake ni wa mashaka.
Akizungumzia usafiri wa ndege alisema, mafuta hunuka katika sehemu ya abiria na kuongeza kuwa ni wazi kuwa ndege ya namna hiyo inaweza kulipuka wakati wowote na alienda mbali zaidi kwa kueleza kuwa ndege hizo ndogo nyingi milango yake mibovu.
“Niliwahi kupanda ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Pemba, mlango unagonga gonga na nilipouliza niliambiwa na rubani kuwa kesho utatengenezwa ni kitasa ndio kimeharibika”, alisema Ruhuza na kuongea kuwa hana uhakika kama ndege hizo huwa zinakaguliwa na hilo ni jambo la hatari kuendelea kubaki kama ilivyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii, Constantine Akitanda alisema, kilichotokea Zanzibar ni matokeo ya rushwa kwani chombo hicho kilipigwa marufuku kubeba abiria nchini Marekani lakini fedha zilitumika, ikachakachuliwa Mombasa kisha ikaletwa Zanzibar kufanyakazi jambo ambalo limegharibu roho za watu.
Alisema hali hiyo pia ni matokeo ya watendaji wa Serikali kutaka kufanyabiashara na kufanya siasa vitu ambavyo daima haviwezi kuchanganyika na ikitokea basi matokeo yake huwa kama ilivyotokea Zanzibar.
“Rushwa ndiyo matokeo ya ajali ile, kwani wasimamizi wa sheria na sera ndiyo wafanyabiashara hivyo wanashindwa kunyoosheana vidole na matokeo yake roho za watu zinapotea na ajali ambayo ni ya tatu kwa meli ambazo zinamilikiwa na kampuni hiyo.
Alisema ajali ya kwanza ilikuwa ya meli yao moja iitwayo Mv Fatah ambayo ilizama bandarini kabla haijaondoka na zingine ndio hizo mbili ambazo zimechukua roho za mamia ya watu na kuonya kuwa hatua za maana zisipochukuliwa Taifa kila mara litakuwa katika kazi ya kutafuta miili ya watu.
Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance for Democtaric Change (ADC), Dawi Kadawi Limbu alisema sera ya Serikali ya kujiondoa katika biashara zikiwamo za huduma muhimu ndiyo chanzo cha matatizo haya kwani sasa roho za watu zinashikwa mikononi mwa wafanyabiashara ambao wanaweza kuamua chochote wanachotaka wao.
“Kuna huduma Serikali haiwezi kukwepa kuzitoa ikiwa ni pamoja na za usafiri wa reli, majini na usafiri wa mabasi” alisema na kuongeza kuwa kuziacha huduma hizo muhimu mikononi mwa wafanyabiashara kwa kisizingizo kuwa serikali haifanyabiashara ni uvivu wa kufikiri.
Alisema dunia nzima suala la huduma za usafiri licha ya kuwapo watu binafsi pia Serikali inatoa ili kuwahakikishai usalama wananchi wake na ameshangaa kuiona Serikali ikishindwa kujifunza kutokana na ajali za majini.
“Mv Bukoba ilipoua mwaka 1999 tulidhani Serikali imejifunza kitu lakini cha ajabu hakuna kitu kama hicho na Ziwa Victoria ajali nyingine itarajiwa wakati wowote kwani meli ya Mv Victoria bado inafanyakazi kati ya Bukoba na Mwanza licha ya uchakavu wake”, alisema.

No comments:

Post a Comment