Ama
kwa hakika katika mwezi wa Ramadhaan kuna fadhila nyingi ambazo mimi
nitazitaja kwa uchache namuomba Allaah Aniwafiqishe 'asaa yawe na
manufaa katika Duniya na Akhera Insha-Allaahu Aamiyn.
1) NI MWEZI WA QUR-AAN:
Kama Alivyosema Mwenyeezi Mungu Mtukufu katika kitabu Chake:
"Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi ambao imeteremshwa Qur-aan ili iwe uongozi kwa watu na hoja na upambanuzi (Baina ya haki na batil)”Qur-aan 2:185
Na
imekua makusudio yake ni kuteremshwa Qur-aan kutoka katika
Lawhum-Mahfuudh ilaa samaai dduniya (Kutoka Lawhim-Mahfuudh mpaka mbingu
ya kwanza).
Vilevile
kama ilivyopokewa na Ibn 'Abbaas (radhiya Allaahu 'anhu) kuwa
makusudiyo yake kwa hakika kuteremshiwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi
wa sallam) Qur-aan mwanzo ni katika mwezi wa Ramadhaan na vilevile
Qur-aan mwanzo wa kuteremka ni usiku wa Laylatul-Qadir na Laylatul-Qadir
iko katika mwezi wa Ramadhaan.
Hivyo basi ni juu yetu kufanya juhudi katika mwezi huu kukithirisha sana
kusoma Qur-aan. Walikua Salafus-Swaalih (Wema Waliotangulia)
wakikilinda kitabu cha Allaah kwa kukisoma na kuyafanyia kazi
yaliyokuwemo kwa mazingatiyo. Pia Tunaambiwa kuwa Sayyidnaa Jibriyl
(‘Alayhis-Salaam) akimfundisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)
Qur-aan katika mwezi wa Ramadhaan, na alikuwa 'Uthmaan bin 'Afaan
(Radhiya Allaahu 'anhu) kila siku akisoma Qur-aan yote yaani
anakhitimisha mara moja kwa siku, kwa maana, msahafu mzima anausoma
kwa siku moja. Na walikuwa baadhi yao
katika wema wakisoma Qur-aan yote kwa siku tatu, wengine kwa wiki moja
na wengine kwa siku kumi. Walikuwa wakisoma Qur-aan ndani ya Swalah na
nje ya Swalah.
Mwenyeezi Mungu Atuwafiqishe mimi na wewe tuisome Qur-aan na kwa mazingatiyo khasa katika mwezi huu tufanye juhudi sana ili tuweze kupata fadhila za mwezi huu mtukufu.
2) NI MWEZI WA SUBIRA:
Subira
ni katika jambo gumu na halipati ila kwa mtu mcha Mungu na mnyenyekevu
kwa Allaah. Na katika kufunga kunatakiwa subira pale mtu anapojizuilia
kutokana na kutokula, kunywa, matamanio na mengineyo. na imekua Swawm ni
nusu ya subira na subira malipo yake ni pepo kama alivyosema Mwenyeezi Mungu Mtukufu:
"Kwa hakika (Mwenyeezi Mungu) Atawapa wenye kusubiri malipo bila ya hisabu"Qur-aan 39:10:
3) MILANGO YA MOTO INAFUNGWA, MILANGO YA PEPO INAFUNGULIWA NA MASHETANI WANAFUNGWA:
Kama ilivyokuja katika Hadiyth iliyopokelewa na Maimamu wawili:
Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema, "Pindi inapokuja Ramadhaan
inafunguliwa milango ya pepo, na hufungwa milango ya moto, na mashetani
wanafungwa kwa Minyororo" (imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim)
Kwa hakika utaona
katika mwezi huu watu wengi wanajitahidi kujiepusha na maasi, watu
wanajaa misikitini kwa kufanya ibada ya mwezi huu hii ni kwa sababu
mashetani wamefungwa na shetani juu ya uasi wake lakini anauogopa mwezi
wa Ramadhaan na vitimbi vyake vinakuwa dhaifu ndio mana wengi nyoyo
zinabadilika wanaswali na kujitahidi kufanya kheri. Lakini ikimalizika
Ramadhaan tu basi Swalah imekwisha kama vile Allaah yupo Ramadhaan tu. Huu ni msiba ndugu zangu Waislamu Allaah Asitujaalie katika hao.
4) LAYLATUL QADR:
Katika mwezi huu kuna siku ya Laylatul-Qadr siku ambayo ni bora kuliko miezi elfu kama Alivyosema Mwenyeezi Mungu:
"Huo ni usiku wa hishima ni bora kuliko miezi elfu.
Huteremka Malaika na roho (za viumbe watakatifu) katika (usiku) huo
kwa idhini ya Mola kwa kila jambo.
Ni amani (usiku) huo mpaka mapambazuko ya alfajiri"
Qur-aan 97:3-5
Imehisabiwa mtu atakapofanya ibada katika usiku huo mmoja ni kama amefanya ibada sawa na miaka 83 na hii ni katika fadhila kubwa kabisa. Na katika kitabu Muwatwaa, Imamu Maalik amesema.
Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ameona umri wa umma za mwanzo ni
mrefu, na umri wa ummah wake ni mfupi akapewa usiku wa Laylatul-Qadr uwe ni bora kuliko miezi elfu.
(Muwatwaa1/321 (Muhammad Fuad 'Abdul-Baaqy)
Hakuna siku tukufu na kubwa kama
siku hii ni wajibu kwetu kuutafuta usiku huu katika kumi la mwisho
kufanya ibada ili tupate fadhila hizo. Ninamuomba Allaah atuwezeshe kwa
hilo, AAMIYN.
5) DU'AA NI ZENYE KUKUBALIWA:
Katika hadiyth iliyopokewa na Imaam Ahmad:
Kutoka kwa Jaabir (radhiya Allaahu 'anhu) kwa isnadi iliyo nzuri
Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Amesema: "Kila Muislam du'aa zake ni
zenye kukubaliwa atapomuomba katika mwezi wa Ramadhaan"
Na
imepokewa katika Hadiyth kuwa du'aa ya mwenye kufunga pia ni yenye
kukubaliwa. Basi mtu ajipinde katika kumuelekea Allaah kumuomba mambo ya
kheri ya dunia na akhera aombe pepo ya Jannaatul Firdaus na alete
maombi mengine Insha Allaah Mwenyeezi Mungu Atayapokea maombi yetu,
AAMIYN.
La mwisho ambalo nitakua nimekamilisha maudhui yangu:
6) MWEZI HUU NI MWEZI WA KUTOA:
Na alikua Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akizidisha kheri nyingi katika mwezi wa Ramadhaan.
Imepokewa na At-Tirmidhiy kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu 'anhu) Kasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) "Bora ya (wakati wa) kutoa sadaqa ni kutoa katika mwezi wa Ramadhaan"
Na
imepokewa na Zayd bin Aslam kutoka kwa babake, amesema nimemsikia 'Umar
bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu 'anhu) anasema, "Ametuamrisha Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) tutoe sadaqa nikatoa mali yangu nikasema leo nimemtangulia Abu Bakr nimekwenda na nusu ya mali, akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kuniambia, "Umewabakishia nini watu wako?" Nikasema, nusu kama hii, na akaja Abu Bakr na kila mali
yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akamuuliza,
"Umewabakishia nini watu wako?Akasema, nimewabakishia Mwenyeezi Mungu na
Mtume wake. Nikasema huyu Abu Bakr hapitiki na kitu chochote abadan"
Kuonyesha
wema waliotangulia walikua wakishindana katika kheri lakini tofauti
kubwa katika zama zetu hizi watu wanashindana katika mambo ya kidunia na
kujifakharisha nayo.
Tunamuomba
Allaah Atuonyeshe mema tuyafuate na mabaya tuyawache na tushindane
katika kila kheri ili tuwe ni wenye kufuzu na kupata daraja ya juu ya
Pepo.
No comments:
Post a Comment