Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Saturday, July 28, 2012

Ummu Suleim (RA)

Uislamu umekuja kutuletea furaha ya Dunia na ya Akhera, na Mwenyezi Mungu akatuandalia Pepo kwa ajili ya furaha ya milele kwa wanaume na wanawake.
Katika historia kuna wanawake katika uislamu waliofanya makubwa na matukufu katika upande wa elimu, ibada, jihad, nk.
Kwa vile tunaelewa kuwa mama ndie shule ya kwanza, na sote tumeipitia shule hiyo, basi leo tutawakumbuka waalimu wakubwa hawa (mamama) waliotenda mambo yasiyosahaulika katika historia ya dini yetu tukufu, na tunawaombea Mungu awarehemu, na sisi pia tutie nia ya kufanya kama walivyo fanya watukufu hawa walotangulia.

UMMU SULEIM(RA)
Huyu si swahaba na pia ni mama yake Swahaba Anas bin Malik (RA), na jina lake ni "Rumaila". Alisilimu mapema lakini mumewe - baba yake Anas (R) alikataa kusilimu na ikawa ni sababu ya kufarakana ,na mumewe aliyekwenda kuishi Syria mpaka akafa huko.
Watu wengi walikuja kutaka kumuoa lakini Ummu Suleim (RA) alikataa, isipokuwa alipokuja Abu Twalha (RA basi Ummu Suleim (RA) akakubali na akaweka shuruti (haja) yake kabisa, akamwambia Abu Twalha: "Wewe wajuwa kuwa kuabudu masanamu ni makosa au hujuwi?" Abu Twalha akasema: "Najuwa:", Akamambia: "Basi huoni haya wala makosa kufanya hivo? Mimi niko tayari kuolewa na wewe na sitaki mahari yoyote kwako, isipokuwa nakutaka Usilimu. Uwe Muislamu, na kusilimu kwako ndio mahari yangu" Abu Twalha akakubali na akasilimu, akamuoa na wakaishi maisha ya furaha, imani na dini, na ndie mwanamke peke yake katika maisha ya Mtume (SAW) aliyefanya hivo.
Aliptimia umri wa miaka kumi Ummu Suleim (RA) alimchukua mwanawe kwa mume wa kwanza Anas bin Malik (R) mpaka kwa Mtume (SAW) na kumuambia: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kila mtu katika mji wa Madina amejikurubisha kwako kwa jambo au kitu, lakini mimi sina kitu ila huyu mtoto wangu Anas (RA), nataka akutumikie." Mtume (SAW) akakubali na akamchukua.
Tukiendelea tutaona kuwa Ummu Suleim (R) alimtaka mwanawe apate shule na madrasa ya Mtume (SAW). Anasema Anas (R) "Nimemtumikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) miaka, na hakuna hata siku moja alinambia mimi mbona umefanya hivi au mbona hukufanya hivi."
Msimamo mwengine wa kukumbukwa katika maisha ya Ummu Suleim (RA) ni baina yake na mumewe Abu Twalha siku ile mwanawe mchanga alipofariki dunia na mama akamchukua na kumzika ubavuni mwa nyumba yao, na mumewe aliporudi kutoka safarini, mke akajiandaa kumpokea mumewe asimwambie kuwa mwanawe keshafariki dunia, bali alimwambia: "Mtoto wetu amepumzika", akikusudia kuwa keshapumzika na dunia. Na hakumwambia isipokuwa baada ya asubuhi kuingia na baada ya mumewe kuoga ndipo alipomjulisha ukweli na mume akakasirika sana, akatoka na kwenda kushitaki mkewe kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW).
Hebu tuangaliye ni jawabu gani aliyopata huko? Mtume (SAW) alimuambia: "Mungu aubariki usiku wenu huo." Inasemekana kuwa walizaa watoto saba wasomi wa Quran vizuri.
Ummu Suleim (RA) alishiriki katika vita vingi vya jihad baina Waislamu na Makafiri, kama vita vya Hunain nk., na  ushujaa wake ulikuwa mkubwa sana, hata Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) katika hadithi moja akasema: "Nimeingia Peponi nikasikia sauti ya mam yaake Anas bin Malik (RA)."
Bukhari 3679 Kitab al-Manaqib.
Ukumbusho na ushujaa wake ni wa kukumbukwa milele, Mungu amuweke pema na atupe sisi moyo na imani katika wakati wetu huu ambao vita vya fikra na usasa vimekuwa vikubwa zaidi, na jihadi ya nafsi na moyo ndio kazi ngumu sana.

No comments:

Post a Comment