Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Tuesday, July 24, 2012

Baada ya Ramadhaan - Jazaa Ya Waja Wema Ni Pepo


Baada ya kutoka katika mwezi mtukufu wa Ramadhaan na kuwa na matarajio na matumaini kwa kumuomba Allaah سبحانه وتعالى Atukubalie Swawm na vitendo vyetu vyema, Atughufurie madhambi yetu, Atujaalie katika watakaoachwa huru na moto, na pia tunamuomba Atuingize katika Pepo Yake Neema ambako tutaishi milele kwa amani na furaha. Hivyo tuingie Ijumaa hii na kukutana na Aayah hii tukufu inayotubashiria hiyo Pepo ili tuwe na matumaini ya kuzidi kuendelea na Taqwa baada ya Ramadhaan hadi hapo tutakapokutana Naye Mola wetu Mtukufu. Anasema Allaah سبحانه وتعالى :



}}وَبَشِّرِ الَّذِين آمَنُواْ وَعَمِلُواْ الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الأَنْهَارُ كُلَّمَا رُزِقُواْ مِنْهَا مِن ثَمَرَةٍ رِّزْقاً قَالُواْ هَذَا الَّذِي رُزِقْنَا مِن قَبْلُ وَأُتُواْ بِهِ مُتَشَابِهاً وَلَهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ وَهُمْ فِيهَا خَالِدُونَ{


{{Na wabashirie walioamini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo mito kati yake; kila watakapopewa matunda humo, watasema: Haya ndiyo kama tuliyopewa mbele. Na wataletewa matunda yaliyofanana; na humo watakuwa na wake waliotakasika; na wao humo watadumu}} [Al-Baqarah: 25]


Allaah سبحانه وتعالى Anatuelezea hali ya waja wema itakavyokuwa Peponi kwamba kutakuweko na mito inayopita chini yake, chemchemu zinazotiririka.


عن أبي هريرة رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وآله سلم قال (( أنهار الجنة تفجر تحت تلال أو من تحت جبال المسك ))  إبن أبي حاتم 1:87

Kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesema, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema kwamba: ((Mito ya Peponi inachipuka kutoka chini ya vilima au majabali ya misk)) Ibn Abi Haatim 1:87


Isitoshe, Pepo hiyo mchanga wake pia ni wa misk inayonukia vizuri, mawe yake ni ya lulu na johari, nyumba zake ni maqasri ya fakhari, viti vyake vya fakhari vilivyoinuka, matakia na mazulia yaliyotandikwa vizuri, vyombo vya dhahabu na fedha, nguo za hariri, matunda ya kila aina, kitu chochote au chakula chochote utakachotamani humo utakipata bila ya kusubiri kipikwe, wanawake wazuri (Huurul-'Ayn walioandaliwa wanaume), na zaidi ya neema hizi ni kwamba tutaonana naye Mola Mtukufu na kupata Ridhaa Yake. 


Basi nani asiyetamani Pepo baada ya kutambua mazuri yaliyomo humo?  Bila shaka kila mmoja wetu ataitamani na kuomba aipate.  Na kuipata Pepo sio kwa wepesi ila baada ya juhudi ya kuendelea kuwa katika Twa'ah ya Allaah سبحانه وتعالى na Taqwah na kufanya vitendo, vyema kwani Allaah سبحانه وتعالى mara nyingi Anapoitaja Pepo Humalizia kwa maneno haya: {{Ni ujira mwema ulioje huo wa watendao}}.


}}وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُبَوِّئَنَّهُم مِّنَ الْجَنَّةِ غُرَفًا تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا نِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ{{


{{Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka Tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito, wakidumu humo. Ni mwema ulioje huo ujira wa watendao}} Al-'Ankabuut:58


Watu wa Peponi watakapoletewa matunda watakula, kisha wataletewa tena watashangaa kuwa yamefanana na yale waliyokwishakula, lakini kumbe ladha yake ni tofuati ingawa ni ya rangi ile ile kama inavyoeleza Aya  


}}كُلَّمَا رُزِقُواْ مِنْهَا مِن ثَمَرَةٍ رِّزْقا{{ً


{{Kila watakapopewa matunda humo}}
}}قَالُواْ هَذَا الَّذِي رُزِقْنَا مِن قَبْلُ{{


{{watasema: Haya ndiyo kama tuliyopewa mbele}}


}}وَأُتُواْ بِهِ مُتَشَابِها{{ً
{{Na wataletewa matunda yaliyofanana}} Al-Baqarah:25



Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما  amesema, "Hakuna kitu Peponi kinachofanana na cha duniani isipokuwa majina" na katika usimulizi mwingine Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما amesema,"Majina pekee yaliyokuwa katika dunia hii na Peponi ndio yanafanana " At-Twabariy 1:392



 Wake Wa Watu wa Peponi


Allaah سبحانه وتعالى  Amewasifu wake wa watu wa Peponi katika Qur'aan katika Aya mbali mbali kuwa ni wake wenye macho meupe makubwa ya kupendeza (Huur), na hapa Amewasifu kuwa ni wake waliosafika kabisa.


}}وَلَهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ{{
{{na humo watakuwa na wake walio takasika}}


Ibn Abi Twalhah ameeleza kwamba Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما  amesema, "Wametakasika kutokana na uchafu na unajisi" (At-Twabariy 1:295). 


Mujaahid amesema, "Wametakasika kutokana na hedhi, kwenda haja kubwa na ndogo, kutema mate, shahawa (manii) na mimba"  (At-Twabariy 1:396). 
Qataadah amesema, "Wametakasika kutokana na unajisi na madhambi" na katika usimulizi mwengine amesema "kutokana na hedhi na mimba" (Ibn Haatim 1:91)
}}وَهُمْ فِيهَا خَالِدُونَ{{


 {{na wao humo watadumu}}



Ni kwamba, wataishi humo milele kwa furaha na amani bila ya tabu yoyote, wala maudhi au ugonjwa au dhiki ya aina yoyote, bali hakutakuwepo tena kifo, ni maisha ya raha yasiyo na mwisho.

No comments:

Post a Comment