Baada ya
kuuawa kwa khalifa aliye dhulumiwa, Waislamu wakawa
wamedangana/wamehemewa, hawana wa kumkimbilia, likawa
zogo/vurugu/fujo. Na hawakuwa na mtu anaye stahiki kuwa khalifa baada
ya Sayyidna Uthman ila Sayyidna Aliy bin Abi Twaalib. Basi wengi wao
wakamuendea kumtaka autawalie ukhalifa. Naye akauangalia mustakabali
wa hali ya Waislamu kwa umakini mkubwa na akatambua ya kwamba
anakabiliwa na fitina itembeayo, isiyo wezwa kuzuiwa. Akawaambia:
Mtafuteni mtu mwingine, kwani hakika sisi tumekabiliwa na jambo
ambalo lina uwepo wake na lina rangi kadhaa, nyoyo haziliwezi na wala
akili hazithibiti juu yake. Basi wakamuomba na kumsihi kwa ajili ya
Allah na dini yake. Akawaambia: Nimekuitikieni (nimeyakubali maombi
yenu). Na jueni ya kwamba nikikuitikieni, nitakupandisheni garI
ninalo lijua (nitakuongozeni kwa sera zangu). Na mkiniacha (msinipe
uongozi), basi hakika si vinginevyo mimi ni sawa na yeyote katika
nyinyi, ila tu mimi ni mtii na msikivu mno kwa mtakaye mtawadha
ukhalifa. Nao hawakumkubali ila yeye tu.
Kisha wakaona
ya kwamba suala hili haliwezi kutimia ila kwa ulaji
kiapo cha usikivu na utii cha Zubeir bin Al-Awaaam na Twalhah bin
Abdillah. Basi likatoka kundi kuwaendea, wakaja nao wakala kiapo cha
utii na usikivu kwa khalifa. Katika mapokezi mengine yasemekana
waliletwa kwa nguvu. Na yasemekana kwamba Zubeir hakula kiapo aslan.
Halafu ndio na watu wengine wakainuka, wakaenda kula kiapo cha utii
na usikivu kwa khalifa. Na likabakia nyuma lisile kiapo kwa khalifa,
kundi katika maswahaba wakubwa wa Madina, kama Sa’ad bin Abi
Waqaasw, Said bin Zaid, Abdullah bin Umar. Usaamah bin Zaid,
Al-Mugheerah bin Shu’ubah, Abdullah bin Salaam, Qudaamah bin
Madhw-oun, Abu Said Al-Khudriy, Ka’ab bin Ujrah, Ka’ab bin
Maalik. Noumaan bin Bashir, Hassaan bin Thaabit, Maslamah bin
Mukhallad, Fudhwaalah bin Ubeid na wengineo katika maswahaba wakubwa
wa miji mingine. [MUQADDIMAH BIN KHALDOUN]
Sayyidna
Aliy-Allah amuwiye radhi-alipo ona kwamba zoezi la kula
kiapo cha utii na usikivu kwake kama khalifa wa nne wa Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-limekamilika. Akainuka na
kuwakhutubia watu, akamuhimidi na kumsifia Allah, kisha akasema:
(Enyi watu! Hakika Allah ameteremsha kitabu ambacho ni chenye
kuongoza, anabainisha humo kheri na shari, basi kheri ifuateni na
shari iacheni. Yaliyo ya faradhi yatekelezeni kwa Allah Ataadhamiaye,
hilo litakupelekeeni (kuingia) peponi. Hakika Allah ameyatukuza
matukufu mengi ambayo si yenye kufichikana na akaufadhilisha utukufu
wa muislamu juu ya yote yaliyo matukufu. Na akazifunga haki za
Waislamu kwa Ikhlaasi na Tauhid. Kwa hivyo basi, muislamu wa kweli ni
yule ambaye waislamu (wenzake) wamesalimika kutokana na (shari ya)
ulimi wake na mkono wake, ila kwa haki. Na si halali (kumwaga) damu
ya mtu muislamu ila kwa yale yanayo wajibisha (kumwagwa).
Yatangulizeni mbele mambo ya umma khususan anapo fikwa na mauti mmoja
wenu. Kwani hakika watu wako mbele yenu na hakika si vinginevyo
kilichoko nyuma yenu ni saa (Kiyama). Ipunguzeni mizigo ya madhambi,
mtafika salama (Akhera), kwani hakika si vinginevyo watu wanangojewa
na Akhera yao. Enyi waja wa Allah! Mcheni Allah katika mji wake na
kwa waja wake, bila ya shaka nyinyi mtaulizwa hata kuhusiana na
vipande vya ardhi na wanyama. Mtiini Allah na wala msimuasi. Na
mtakapo iona kheri, basi iandameni na mtakapo iona shari, basi
iepukeni. “NA KUMBUKENI MLIPO KUWA WACHACHE, MKIONEKANA WANYONGE
KATIKA NCHI...”. [08:26]
Kisha
akashuka kutoka mimbarini. [TAARIKHUT-TWABARIY 02/698]
-
Wasifu wa Sayyidna Aliy:
Khalifa huyu wa nne wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-yeye ni Aliy bin Abi Twaalib, bin Abdil-Mutwalib, bin
Hashim, mkuraishi wa ukoo wa Hashim, binamu wa Mtume wa Allah. Na
mama yake ni Bi. Fatmah bint Asad, bin Hashim, bin Abdi Manaaf.
[AL-ISWAABAH 04/564, AT-TWABAQAAT AL-KUBRAA 02/259, TAARIKHU KHALIFAH
BIN KHAYYAATW, sah. 80 & TAARIKHUT-TWABARIY 01/537].
Alizaliwa Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi-mnamo mwaka wa
thelathini na
mbili, tangu kuzaliwa kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.
Wakati Mtume anakabidhiwa na Mola wake majukumu mazito ya utume,
Sayyidna Aliy alikuwa chini ya umri wa baleghe. Na alikuwa akisakini
(akiishi) pamoja na Mtume katika nyumba yake (Mtume), akimlisha na
kunywesha kwa sababu ya ufakiri ulio mkumba baba yake (Mzee Abu
Twalib; ami yake Mtume). Kwa ajili hiyo (ya kulelewa katika nyumba ya
Mtume), akaongoka na muongozo wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie. Na wala hakujiboronga na uchafu/najisi ya jaahiliya, yaani
hakupata kuyaabudu masanamu na maovu mengine yaliyo kuwa yakitendwa
katika zama hizo za viza vya jaahiliya.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo gura
(hama) kutoka
Makka kwenda Madina, Imamu Aliy alimfidia kwa kuitoa muhanga nafsi
yake. Pale alipo lala kwenye kirago chake, tena akajifunika shuka
lake, ili wale walio izingira nyumba ya Mtume, waendelee kudhania ya
kwamba Mtume angali amelala, ili wasimpe taabu katika kutoka kwake.
Baada ya fidaa hiyo, naye huyoo akaondoka Makka kwenda Madina
kuungana na Mtume wa Allah huko.
Sayyidna Aliy-Allah amuwiye radhi-alibahatika kushiriki
pamoja na
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika vita vyake vyote, ila
vita vya Tabuuk. Hakwenda katika vita hivyo, kwa kuwa Mtume
alimkaimisha ukhalifa wa Ahali beit wake na akamwambia: “Hivyo
wewe huridhii kuwa kwangu kama daraja aliyo kuwa nayo Harun kwa Musa,
ila tu ni kwamba hapana utume baada yangu”. Bukhaariy [3706,
3503] & Muslim [2404]-Allah awarehemu.
Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi-alikuwa na mchango mkubwa
katika vita
vyote, naye ndiye mtu wa kwanza kufanya mubaaraza (mpambano wa watu
wawili) katika vita vya Badri. Naye ni miongoni mwa wale watu walio
thibiti katika medani, katika vita vya Uhud na Hunein wakati ambao
maswahaba walichangukana kutokana na ukali wa mashambulizi ya adui,
wakamuacha Mtume na maswahaba wachache walio thibiti pamoja nae. Na
kwa mikono (juhudi) yake, ilifunguliwa ngome madhubuti ya Mayahudi,
Khaibar.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimuoza Imamu
Aliy, binti
yake Faatimah, mnamo mwaka wa pili wa Hijra. Bibi Faatimah akamzalia
Imamu Aliy watoto; Hassan, Hussein, Zainab al-kubraa na Ummu Kulthum
al-kubraa.
Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi-alizisoma kwa niaba ya
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-aya za mwanzo za Surat Tauba, katika
msimu wa Hijja. Kwa ajili ya kutangaza kutupiliwa mbali dhima ya
Allah na Mtume wake, kwa washirikina.
Alipo fariki Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na
Sayyidna
Abubakar akachaguliwa kuwa khalifa wake, Imamu Aliy-Allah amuwiye
radhi-naye alimpa baia (kiapo cha utii na usikivu) pamoja na kwamba
alikuwa akiona kuwa yeye ndiye mstahiki wa ukhalifa, kwa sababu ya
udugu wake kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Lakini ni
kwamba yeye alikuwa akiichukia khilafu (kukhitalifiana na kuzozana).
Ni kwa ajili hiyo ndio Muhammad bin Siiriin; taabii akazikadhibisha
kauli zote zilizo nasibishwa kwa Imamu Aliy, kauli ambazo ndani yake
kuna kupomosha (kuangusha) makamo (daraja) ya masheikh wawili;
Abubakar na Umar-Allah awawiye radhi. Kama yalivyo pokewa hayo katika
SAHIH AL-BUKHAARIY.
Na ukhalifa ulipo twaliwa na Sayyidna Umar-Allah amuwiye
radhi-kadhaalika alimpa baia, pamoja na hivyo akamuoza binti yake;
Ummu Kulthum. Na ni mara nyingi tu Sayyidna Umar alikuwa akimkaimisha
uongozi wa Madina pale anapo toka nje ya Madina. Na hata Sayyidna
Uthman-Allah amuwiye radhi-alipo tawazwa kuwa khalifa wa Waislamu
baada ya Sayyidna Umar. Kadhaalika alimpa baia mpaka mwisho wa
ukhalifa wake walipo simama dhidi yake wale waasi na wakamtia dosari
kwa kuwapa madaraka ndugu zake. Na ni mara nyingi tu, Sayyidna Aliy
alikuwa akimpa kwa moyo mkunjufu nasaha na akimuongoza kwenye yale
ambayo ndani yake kumo kufaulu kwa umma. Lilipo timia lililo hukumiwa
na Allah na Sayyidna Uthman akauawa shahidi, Waislamu walimuendea
Sayyidna Aliy na wakampa baia ya ukhalifa, mwezi 25, Dhul-Hijja,
mwaka 35H. Akalibeba jukumu zito la ukhalifa, katika kipindi cha
mzozo na vurugu baina ya Waislamu, kwa kipindi kinacho karibia miaka
mitano ambamo haimkumtakatia hata siku moja. Na amri ya Allah ni
kudra iliyo kwisha kadiriwa.
Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi-alikuwa na rangi ya maji
ya kunde,
mwenye macho makubwa, kitambi na upara. Mwingi wa ndevu na nywele za
kifua. Si mrefu wala si mfupi wa kuchusha, mwenye mikono na miguu
yenye nguvu. Alikuwa mzuri wa sura, mwingi wa tabasamu.
Sayyidna Aliy-Allah amuwiye radhi-mbali na watoto wake
alio zaa na
Bibi Faatimah bint Rasuuli, alijaaliwa kupata watoto wengine kwa wake
zake wengine. Watoto hao ni: Abbas, Ja’afar, Abdullah, Uthman,
Ubeidillah, Abubakar, Muhammad Al-Asghar (mdogo), Yahya na Umar.
Wengine ni Rukia, Muhammad Al-Ausatw (wa kati), Muhammad Al-Akbar
(mkubwa) aliye tangaa kwa jina la Ibn Al-Hanafiyyah. Pia walikuwepo
Hasan, Ramlah al-kubraa (mkubwa), Ummu Kulthum As-sughraa (mdogo),
Ummu Haaniy, Maimunah, Zainab As-sughraa (mdogo) na Ramlah As-sughraa
(mdogo). Watoto wake wengine ni: Faatimah, Umaamah, Khadija,
Ummul-Kiraam, Ummu Salamah, Ummu Ja’afar, Jumaanah na Nafiisah.
[AT-TWABAQAAT AL-KUBRAA 01/108, TAARIKHUT-TWABARIY 02/492 &
AL-BIDAAYAH WAN-NIHAAYAH 07/366].
No comments:
Post a Comment