Mwezi
huu mtukufu umejaa fursa ya kujichumia mengi ya kheri ambayo thawabu
zake huanzia tokea kumi hadi zaidi ya mia saba pamoja na malipo maalum
yatokayo kwa Allaah kwa Mfungaji, kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم
قال صلى الله عليه وسلم : ((كل عمل ابن آدم له الحسنة بعشر أمثالها إلى سبعمائة ضعف . يقول الله عز وجل : إلا الصيام فإنه لي وأنا أجزي به ، ترك شهوته وطعامه وشرابه من أجلي، للصائم فرحتان ؛ فرحة عند فطره ، وفرحة عند لقاء ربه، و لخلوف فم الصائم أطيب عند الله من ريح المسك)) أخرجه البخاري ومسلم
Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم,: ((Kila amali njema ya mwanaadamu inalipwa mara kumi na inaongezewa thawabu kutoka kumi hadi mia saba, na Allaah سبحانه وتعالى
Anasema isipokuwa Swawm, kwani hiyo ni kwa ajili Yangu na Mimi Ndiye
Nitakayemlipa. Ameacha matamanio yake na chakula chake na maji yake kwa
ajili Yangu. Kwa aliyefunga atapata furaha mbili; furaha anapofuturu
na furaha atakapoonana na Mola wake, harufu inayotoka kinywani mwa
aliyefunga ni nzuri mbele ya Allaah سبحانه وتعالى kuliko harufu ya misk)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Kwanza kabisa inatupasa tuanze mwezi huu mtukufu kwa kutia Nia moyoni (si kuitamka) yenye Ikhlaasw ambayo ndio msingi wa kutaqabaliwa amali ya ibada yoyote, na ili kupata Ridhaa ya Allaah سبحانه وتعالى kama Anavyosema:
((وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاء وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ وَذَلِكَ دِينُ الْقَيِّمَة))
((Nao
hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Allah kwa kumtakasia Dini, wawe
waongofu, na washike Swalah, na watoe Zakah. Na hiyo ndiyo Dini
madhubuti)) [Al-Bayyinah: 5]
Ifuatayo
ni baadhi ya milango ya kheri ambayo inampasa kila Muislamu ajitahidi
kuiingia na kutekeleza hizo amali njema katika mwezi huu mtukufu wenye
kheri na baraka nyingi ili kujichumia mema mengi yatakayomfaa mtu
Akhera.
1-Swawm kwa imani Ili Kufutiwa Madhambi:
قال صلى الله عليه وسلم : (( من صام رمضان إيماناً و احتساباً غفر له ما تقدم من ذنبه )) أخرجه البخاري ومسلم
Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ((Atakayefunga Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia )) Al Bukhaariy na Muslim.
2-Qiyaamul-Layl (Kusimama Usiku katika Swalah); Tarawiyh na Tahajjud:
قال صلى الله عليه وسلم : ((من قام رمضان إيماناً واحتساباً ، غفر له ما تقدم من ذنبه )) أخرجه البخاري ومسلم
Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم: ((Atakayesimama [kwa Swalah ya usiku] kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
3-Sadaka:
قال صلى الله عليه وسلم: ((أفضل الصدقة صدقة في رمضان )) أخرجه الترمذي عن أنس
Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم: ((Sadaqah bora kabisa ni ile inayotolewa katika mwezi wa Ramadhaan)) [At-Tirmidhiy kutoka kwa Anas]
4-Kumfuturisha aliyefunga:
قال صلى الله عليه وسلم : ((من فطر صائماً كان له مثل أجره غير أنه لا ينقص من أجر الصائم شيء)) أخرجه أحمد والنسائي وصححه الألبان
Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم: ((Atakayemfuturisha aliyefunga, atapata ujira kama ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga)) [Ahmad, An-Nasaaiy – Ameipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy]
Na Allaah سبحانه وتعالى Anasema:
((وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَى حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا)) (( إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاء وَلَا شُكُورًا ))
(( إِنَّا نَخَافُ مِن رَّبِّنَا يَوْمًا عَبُوسًا قَمْطَرِيرًا)) (( فَوَقَاهُمُ اللَّهُ شَرَّ ذَلِكَ الْيَوْمِ وَلَقَّاهُمْ نَضْرَةً وَسُرُورًا)) ((وَجَزَاهُم بِمَا صَبَرُوا جَنَّةً وَحَرِيرًا))
((Na
huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na
wafungwa)) ((Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Allaah Hatutaki
kwenu malipo wala shukrani)) ((Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu
Mlezi hiyo siku yenye shida na taabu)) ((Basi Allaah Atawalinda na
shari ya siku hiyo na Kuwakutanisha na neema na furaha)) ((Na Atawajazi
Bustani za Peponi na maguo ya hariri kwa vile walivyosubiri)) [Al-Insaan: 8-12]
Vile vile kasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :
(( أيما مؤمن أطعم مؤمناً على جوع أطعمه الله من ثمارالجنة ومن سقى مؤمناً على ظمأ سقاه الله من الرحيق المختوم )) رواه الترمذي بسند حسن
((Muumin
yeyote atakayemlisha Muumin mwenzake mwenye njaa, Allaah Atamlisha
katika matunda ya Peponi, na atakayemnywesha Muumin mwenye kiu Allaah
Atamnywesha kutoka katika 'Rahiyqul-Makhtuum' [Kinywaji safi kilichofunikwa kwa kizibo madhubuti] )) [At-Tirmidhiy na Isnaad yake ni nzuri]
5-Kusoma Qur-aan sana na kujua maana yake:
Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi ulioteremshwa Qur-aan kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى:
((شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَان))
((Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi)) [Al-Baqarah: 185]
Kwa hiyo inampasa Muislam azidishe kusoma Qur-aan na ajitahidi kukhitimisha japo mara moja katika mwezi huu kama alivyokuwa akifanya Jibriyl عليه السلام wakati akimfundisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم Qur-aan kila Ramadhaan. Vile vile Maswahaba na Salaf Swaalih (Wema Waliopita/Watangu wema) walikuwa wakijihimiza sana kusoma Qur-aan mwezi huu. 'Uthmaan bin 'Affaan رضي الله عنه
alikuwa akikhitimisha Qur-aan kila siku mara moja. Na baadhi ya Salaf
wakikhitimisha katika Kisimamo cha usiku kila baada ya siku tatu. Na
wengineo kila siku saba, na wengine kila siku kumi. Na walikuwa
wakiisoma katika Swalah na nje ya Swalah.
6-Kukaa kwa kumkumbuka Allaah baada Swalah ya Alfajiri hadi jua litoke:
عن أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم ، أنه قال (( من صلى الفجر في جماعة ثم قعد يذكر الله حتى تطلع الشمس ثم صلى ركعتين كانت له كأجر حجة وعمرة تامة تامة تامة) ) أخرج الترمذي صححه الألباني .
Imetoka kwa Anas kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم
amesema: ((Atakayeswali Alfajiri katika Jama'ah kisha akakaa
anamkumbuka Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Raka'ah mbili,
atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio kamili kamili kamili)) [Imetolewa na At-Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy]
(Kuswali Jama'ah kumesisitizwa kwa wanaume, ama mwanamke anaweza naye kupata ujira wa thawabu zilizotajwa akiswali nyumbani kwake)
Thawabu
hizo ni katika siku za kawaida ndugu Muislamu, seuze mwezi wa
Ramadhaan? Ni fadhila ya tendo moja tu, na endapo ndugu Muislam
utatekeleza tendo kama hilo
kila siku, ni thawabu ngapi utakazozichuma? Basi hii sasa ndio fursa
itumie. Na ukishindwa kila siku, japo kwa wiki mara moja, utakuwa una
thawabu za Hajj na 'Umrah mara nne kwa mwezi, na ukiendelea hivyo miezi
yote kumi na mbili basi utakuwa na thawabu za Hajj na 'Umrah mara 48 kwa
mwaka. Yatakuwaje malipo yake ukitimiza kila siku? Na hii ni mojawapo
ya neema na uadilifu wa Allaah سبحانه وتعالى
kwamba hata maskini asiyeweza kujilipia kwenda Hajj au 'Umrah aweze
kupata thawabu hizi akiwa mjini kwake, tena chumo lenyewe hilo, lenye
thawabu nyingi zenye kumshinda hata yule mwenye uwezo wa mali, ni kwa
muda wa usiozidi masaa mawili; tokea Alfajiri hadi kuchomoza jua. Hizi
ni neema za Allaah ambazo hazipatikani tu katika mwezi huu mtukufu bali
zinapatika siku zote.
7- I'itikaaf:
عن عائشة – رضي الله عنها- قالت "كان النبي يعتكف في كل رمضان عشرة أيام؛ فلما كان العام الذي قبض فيه اعتكف عشرين يوماً - أخرجه البخاري
Kutoka kwa 'Aashah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba: "Mtume صلى الله عليه وآله وسلم
alikuwa akikaa I'itikaaf kila Ramadhaan katika siku kumi za mwisho, na
mwaka ambao aliondoka duniani alikaa I'itkaaf siku ishirini. [Al- Bukhaariy]
I'itikaaf ni ibada ambayo inajumuisha Twa'a nyingi kama tilawah (kusoma) Qur-aan, Swalah, Dhikr na Dua'a, na wala haina tabu. Na fadhila zake ni kubwa mno khaswa katika zile siku kumi za mwisho ndio imo siku ya Laylatul-Qadr. Ni fursa kubwa ya mtu kuweza kuupata usiku huo mtukufu kwa kujiepusha na mambo yanayomshughulisha kila siku ya kidunia na kuulekeza moyo na nafsi yake katika Twa'a kamili kwa Mola wake akiwa msikitini.
8-'Umrah katika mwezi wa Ramadhaan:
Imethibiti katika hadiyth kwamba thawabu za kwenda 'Umrah katika Ramadhaan ni sawa sawa na Hija.
(( عمرة في رمضان تعدل حجة )) أخرجه البخاري و مسلم
(('Umrah katika Ramadhaan ni sawa [kwa thawabu] na Hijjah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
9-Baraka za Suhuur (Daku):
Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم
(( تسحروا فإن في السحور بركة )) رواه البخاري ومسلم
((Kuleni daku kwani katika huko kula daku, kuna baraka)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
10-Du'aa:
Ramadhaan ni mwezi wa Du'aa pia kwani baada ya Allaah سبحانه وتعالى Kutaja ayah za kufunga Ameendelea kusema:
((وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُواْ لِي وَلْيُؤْمِنُواْ بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ))
((Na
waja Wangu watakapokuuliza khabari Zangu, waambie kuwa Mimi nipo
karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie
Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka)) [Al-Baqarah:186]
11-Kuomba Maghfirah na Tawbah
Ramadhaan ni mwezi wa Maghfirah na Tawbah na ni fursa kubwa kutumia wakati wa Suhuur (kukesha kwa ajili ya kula daku) kuomba Tawbah na Maghfira kwani Allaah سبحانه وتعالى ni katika sifa za wenye kupata Pepo.
((وَبِالأََسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُون))
((Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfira)) [Adh-Dhaariyaat: 18]
Vile vile Allaah سبحانه وتعالى Huteremka nyakati hizo katika mbingu ya kwanza::
عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((ينزل ربنا تبارك وتعالى كل ليلة إلى السماء الدنيا حين يبقى ثلث الليل الآخر فيقول: من يدعوني فأستجيب له؟ من يسألني فأعطيه؟ من يستغفرني فأغفر له )) )) رواه البخاري ومسلم
Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وسلم amesema: ((Allaah سبحانه وتعالى
Huteremka kila siku katika mbingu ya dunia [mbingu ya kwanza]
inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba
Nimtakabalie? Nani ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfira
Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy Na Muslim]
12-Kuunga udugu na ujamaa:
((الرحم معلقة بالعرش ، تقول : من وصلني وصله الله ، ومن قطعني قطعه الله )) رواه البخاري ومسلم
((Fuko la uzazi linaning'inia katika 'Arshi linasema, atakayeniunga, Allaah Atamuunga, na atakayenitenga Naye Allaah Atamtenga [Atamkatia])) [Al-Bukhaariy na Muslim]
13- Laylatul-Qadr
Ni usiku ambao ibada yake ni bora kuliko ibada utakayoifanya miezi alfu.
((إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْر)) ((وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ)) ((لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْر))
((Hakika
Sisi tumeiteremsha Qur-aan katika Laylatul-Qadr, Usiku wa Cheo
Kitukufu))((Na nini kitacho kujuulisha nini
Laylatul-Qadr))((Laylatul-Qadr ni bora kuliko miezi elfu)) [Al-Qadr: 1-3]
Basi na tujitahidi ndugu zetu tusipoteze fursa kubwa ya kuingia katika milango hiyo mingi ya kheri ili tutoke katika mwezi huu Allaah سبحانه وتعالى Akiwa Radhi na sisi na Aulipe malipo mema.
No comments:
Post a Comment