Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Tuesday, July 17, 2012

Nini Cha Kufanya Katika Ramadhaan Ili Tufaidike Nayo


Shukrani zote ni Zake Mfanya alitakalo; Asiye ulizwa kwa alifanyalo; al Waahidul al Ahadu as Swamad; Asiye zaa wala Asiye zaliwa; Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.

Ar Rahmaan ar Rahiym Ametutunukia Ramadhaan kuwa ni pahala na wakati wa kila mmoja wetu kuonyesha juhudi yake kwa kupania na kujipamba kwa kila aina ya amali nzuri na kubadili mtindo wa maisha yake ya kila siku kama alivyotusunia na kutuwekea mwenendo huo Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam.

Rehma na amani zimfikie Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam aliye kuwa na mtindo na hali tofauti kabisa katika Ramadhaan ukimlinganisha na hali yake ya kawaida katika miezi iliyobaki.  Yeye Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam katika mipango yake, jaduweli yake, taratibu na mikakati yake yote katika mwezi huu huwa anaipamba na kuijaza kwa aina mbali mbali za twaa, utii na kurubati za namna mbali mbali za kumkurubisha kwa Allaah; yote hayo kwa kuelewa ubora na fadhila zilizomo ndani ya masiku haya machache na matukufu, bali Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam alikuwa na yakini kwa Aliyoyatunukia Allaah na kuyapa masiku haya machache, ndio akawa anabadilisha mtindo wa maisha yake ya kila siku katika masiku haya, si kwa kuongeza namna za vyakula, vinyaji, michezo, muda mrefu zaidi wa kulala, muda wa kukeza na kuangalia TV, muda mrefu wa kufanya shoping na kadhalika.
Ndugu zangu katika iman, napenda kujiusia nafsi yangu kwanza na nasfi zenu kumcha Allaah na kumtii, kwa kutekeleza kila Aliloliamrisha kadiri ya uwezo wetu, na kujikataza na kila Alichokikataza mara moja.
Ndugu zangu wapenzi katika imani, napenda kumuomba Allaah Ajaaliye kuwa haya Aliyoni jaaliya kwa tawfiki yake kuyakusanya na leo kunipa uwezo wa kuyawasilisha mbele yenu niwe sijakusudia isipokuwa kwa ajili ya kutafuta na kutaka Radhi zake na Rehma zake; hivyo basi namuomba aturuzuku Ikh-laas kwa tuyafanyayo, tuyasemayo na mengineno ikiwemo huku kuwepo kwetu sote hapa na kuja kwetu katika hafla kama hizi na nyenginezo zote za kheri aturuzuku ndani yake ikh-laas kuwa hatukusudia kuja hapa kujionyesha; kumfurahisha kiumbe; kumridhisha kiumbe; au kutaka kusifiwa; kutaka kushukuriwa, kutaka kuonekana kuwa tunajuwa na yote ambayo yatapelekea kuingia dosari katika amali kwa kukusudia viumbe badala ya Muumba wao.
Ndugu zangu katika iman, Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam alikuwa akibadili mtindo wa maisha yake ya kila siku katika masiku haya kwa kuzidisha na kukithirisha namna mbali mbali za ibadah, juu ya kuwa amesamehewa madhambi yake yote yaliyotangulia.
Ndugu zangu katika iman, Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam alikuwa akidurusu Qur an na Jibriyl ‘alayhis Slaam nyakati za usiku katika masiku haya machache; hivyo basi alikuwa anapokutana nae huwa mbora kwa mambo ya kheri kuliko upepo wenye kheri na baraka, na alikuwa mbora wa watu, na huwa mbora zaidi katika Ramadhaan; hukithirisha ndani yake sadaqa, ih-saan, kusoma Qur an, kuswali, kuleta adh-kaar, kukaa itikafu na kadhakila, kama ilivyothibiti katika hadiythi ya Ibn ‘Abbaas radhiya Allaahu ‘anhumaa aliposema kwamba:
“Alikuwa Mtume Swalla Lllaahu ‘Alayhi Wa’alaa Alihi Wasallam ni mbora -mwenye matendo mema- wa watu, na alikuwa mbora  zaidi katika Ramadhaan wakati anapokutana na Jibriyl alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhaan akimfundisha Qur-aan”  Imepokelewa na Bukhaar, kitabu cha Swawm, mlango alikuwa Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam mbora zaidi katika Ramadhaan.

Ndugu zangu katika iman, mtindo wa maisha wa kila siku wa Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam hubadilika kwa kuanza Ramadhaan, kwani alikuwa akiuwekea mwezi wa Ramadhaan aina za ibadah asizo ziwekea miezi mengineo, mpaka akawa anafikia kuwasilisha kuunganisha funga -hafuturu- wakati mwengine, ili apate wakati zaidi wa kujishughulisha na ibadah, kama ilivyothibiti katika hadiythi ya Abi Hurayrah radhiya Allaahu ‘anhu kuwa Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam amesema:
“Jihadharini na kuunganisha kufunga, jihadharini na kuunganisha kufunga; pakasemwa: hakika wewe unaunganisha, akasema Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam: Hakika mimi huwa ananilisha Mola wangu na huninyisha ….” Imepokelewa na Bukhaar, kitabu cha Swawm, mlango alikuwa Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam mbora zaidi katika Ramadhaan.

Ndugu zangu katika imani, Ramadhaan ndio hiyo imewadia; nini cha kufanya ndani yake? Au vipi tufaidike na Ramadhaan? ndani ya mwezi huu; kuna makundi mawili tu ya kuchagua mtu lipi awe; Fariyqun fil Jannat wafariyqul fis Sa’iyr; tuwe kama walivyokuwa Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam na Swahaba zake na Salafus Swaalih wa huu ummah, tuje kwa tawfiki yake Mola insha Allaah kuambiwa Salaamun ‘Alaykum, ingieni Peponi; au vyenginevyo wal’iyaadhu bil Laahi kuwa katika watoambiwa ingieni milango ya Jahannamu mdumu humo.
Ndugu zangu katika imani, kila mmoja wetu achaguwe apendacho baada ya kuelewa kuwa mwezi wa Ramadhaan ni msimu wa kusamehewa madhambi yote yaliyotangulia kwa mwenye kufunga na kusimama huku akiwa na imani na kutarajia malipo kwa Mola wake kwa kuwa haoni uzito wala halalamiki, bali anasubiri kwa kuelewa kuwa Aliyemtaka afunge ni Ar-hamur Raahiymin; ni Mwenye huruma kupita mama kwa mwanawe, hivyo hakuwa na lengo la kumuonea wala kumsumbuwa au kumuudhi tu kwa kumzuilia kula, kunywa na kadhalika, ndio akasema mwisho wa aya za Swawm:
“ ….  Allaah anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Allaah kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru” al-Baqarah aya ya 185.

Ndugu zangu katika iman, jichagulie ukipendacho kwani Ramadhaan ni msimu wa kurehemewa, msimu wa kutolewa katika moto, msimu wa kutenda mema kwa wingi, msimu wa kujilazimisha kutenda kila litalo weza kwa tawfiki yake Mola kukupelekea kujikurubisha na Mola wako, msimu wa watu kuingia Peponi, msimu wa kufunguliwa na kuwekwa wazi mlango wa Rayyaan, msimu wa kutekeleza ‘amali katika ‘amali zinazomuhusu Allaah na hakuna ajuae malipo ya ‘amali hiyo isipokuwa Allaah pekee, msimu wa watu kutolewa katika Moto, msimu wa Qiyaam, Siyaam na ‘Itt’aam, msimu wa kujikumbiwa thawabu na kujijazia kurasa za daftari lako kwa kila aina ya mema, msimu wa kusoma Qur an kwa wingi na kujichumia thawabu kwa kila herufi uisomayo; msimu wa kukutana kwa ajili ya kusoma Qur an, kusikilizana, kuihifadhi, kupima hifdhi yako ya Qur an, kuisikiliza Qur an, msimu wa kutoa sadaqa kwa wingi, msimu wa kulingania watu.
Ndugu zangu katika iman, jichagulie ukipendacho kwani Ramadhaan kuna usiku wa Laylatul Qadr, usiku wenye kutafutwa na kila mwenye uchu na hamu ya kutaka kufutiwa majidhambi yake na kutolewa Motoni, msimu wa kufunga mdomo wako na kila lenye kuchukiwa na Allaah, msimu wa kula daku jambo ambalo litakupeleka kuwa macho wakati thuluthi ya mwisho ya usiku (kabla ya alfajiri) wakati wa As haar, wakati ambao Allaah Huteremka (kama inavyolingana na utukufu Wake) katika wingu ya dunia na Kuuliza kwa kusema: Nani ananiomba Nimkubalie? Nani ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?, wakati ambao watu wema na watiifu wanautumia kuomba maghafira, msimu wa kupunguza kula na kujihimu kwa kuzidihsa matendo mema kwani kila tumbo likijaa huwa hakuna njia ya kuwa na uchangamfu katika kutekeleza amali nyingi ambazo Ramadhaan ndio msimu wake.

Ndugu zangu katika imani, kila mmoja wetu achaguwe apendacho baada ya kuelewa kuwa kufuatilia misimu ya kheri na msimu mkubwa wao ni Ramadhaan na kufaidika nayo kwa kujishughulisha na kila lenye kheri ni dalili yenye kuthibitisha kuwa mfuatiliaji ni mwenye imani yenye nguvu, na kufurahi kwa kuja au kuwasili kwa misimu hiyo pia ni dalili yenye kuthibitisha imani yenye nguvu, na mwenye kuweka matayarisho na maandalizi mazuri ya kuipokea hiyo misimu ya kheri ni dalili ya imani yenye nguvu; na wenye imani yenye nguvu wanasema :
Kwa hakika katika hii dunia kuna Jannah –pepo- asiye iingia basi hakuna njia ya kuingia Jannah ya Akhera

Ndugu zangu katika imani, huu ndio utamu na raha ya iman na ladha ya uhusiano na mawasiliano na Allaah. Ni ipi njia ya kupita kuingia Jannah? Vipi tufunge? Vipi tusimame Qiyaam? ili tuwe miongoni mwa rijaal ambao biashara –kazi/kupindwa- wala kuuza hakuwashughulishi -wala hakuwazuilii- na kumdhukuru Allaah, kusimamisha Swalla, kutoa Zaka wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka; au tupate waliyoyapata rijaal walio timiza waliyo ahidiana na Allaah.

Ndugu zangu katika imani, tunatakiwa tufunge na tusimame kama alivyokuwa akifunga na kusimama Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam, na lililo muhimu ni kujiuliza kwanini nafunga???

Ndugu yangu katika imani, jiulize nafsi yako hasa katika Ramadhaan, kwanini nafunga? Suali hili huenda likakusaidi sana katika kukupelekea kuweza kufikia kwa tawfiki yake Mola kupata waliyoyapata waliofunga, jiulize suali hili liweza kukusaidia kwa uwezo wa Rabbuka na Rabb wa Ramadhaan katika kuidhibiti Swawm yako ipate kukutapia makusudio na matunda yake, na pia isije kubadilika na kugeuka Swawm yako badala ya kuwa ibadah kama anavyotaka Allaah ikawa ada au mila au desturi ukaja kuambukia kiu na njaa tu.

Ndugu zangu katika imani, jitahidi kulifatutia jawabu suala hili, kwani wengi hufunga kwa kujizuilia kula kunywa na kadhalika lakini ni wachache wao ndio wanao elewa kwanini wanafunga; na huku kuelewa kwanini nafunga ndio tofauti baina ya ada na ibadah.  Hivyo basi kwanini nafunga???

Ndugu zangu katika imani, suali litakusaidia kuweza kufikia kuelewa lengo lililo pelekea kufaradhishiwa Swawm ya Ramadhaan, na lengo katika amali yo yote ile likiwa wazi na kueleweka basi huwa ni wepesi amali hiyo kutekelezeka kwani unakuwa na msukumo unaokupelekea kujitahidi na kufanya kila uliwezalo kwa tawfiki yake Mola ili uweze kufikia hilo lengo.

Ndugu yangu katika iman, tunajizuilia kula kunywa kuingiliana na kustarehe ahli zetu zaidi ya nusu ya siku, kwanini? Tunakaa na njaa na kui, kwanini? Tunakesha na kujitaabisha na kupata taabu, kwanini? Vyakula vitamu na vyenye kuvutia viko mbele yako na vyinywaji vya namna mbali mbali baridi moto viko machoni mwako, na hata harufu yake hupendi kuinusa, unaweza kula kunywa na asiweze yo yote kujuwa, lakini hupeleki mkono wako na hakuna akuonae, kwanini?

Ndugu yangu katika iman, kitu gani unataka, nini unatarajia, nini unatafuka kwa kutofanya hayo yote? Nini lengo lake? Wapi unataka kufika? 

Ndugu yangu katika iman, huenda tukasema kuwa tunafunga kwa kuwa Allaah Ametufaradhishia na Ametuamrisha tufunge, hivyo inatuwajibikia kutii na kuitikia wito Wake Sub-haanah kwa Aliyo amrisha, kwani hilo ni wajibu kwa kila Muislamu, hata kama haikutubainikia hekima na tunda la amri au katazo hilo; hii ina maana kuwa hakuna haja wala ulazima wa kutafuta lengo la Aliyo amrisha Allaah na Mtumewe Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam kama hawakulitaja na kulibainisha, kwa kuwa sisi waislamu tumejisalimisha kwa Allaah na kheri yote iko katika yale Aliyo amrisha Allaah na Mtumewe Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam, na wanapo bainisha –kama hapa- lengo na kuliainisha ni vyema tufanye kila tuliwezalo kuhakikisha kwa tawfiki yake Mola kulifikia lengo lililo wekewa hiyo amali unaitekeleza; Qur aan inasema:
“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Swawm, kama waliyoandikiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu”. al Baqarah aya ya 183.

Ndugu yangu katika iman, tukirejea katika anuani ya mada yetu Vipi tufaidike na Ramadhaan au Nini cha kufanya katika Ramadhaan, hili ni suali linalo washughulisha wenye iman yenye nguvu na wenye pupa na hamu ya kuhakikisha kuwa Ramadhaan haimaliziki isipokuwa wameweza kwa tawfiki yake Mola wa Ramadhaan kufikia lengo lililo wekwa wazi kutaka kufikia na kwa tawfiki yake Mola wa Ramadhaan kuweza kujinyakulia tiketi ya makalio -kiti- ya kweli kweli kwa Mfamle Mwenye uweza kama isemavyo Qur aan:

“Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na mito.  Katika makalio ya haki kwa Mfalme Mwenye uweza” al Qamar aya ya 54-55.

Ndugu yangu katika iman, tunataka hayo, je tunataka kiti cha kweli kweli ambacho hakuna atae kuja hata kwa wingi gani wa kura kukuondoa katika kiti chako hicho?  Kama tunataka basi tufikirie haya, je utapenda mwaka huu ufunge Ramadhaan mbili au zaidi –moja kwa mbili buy one get others free-, kama uko tayari na hayo basi namna yake iko katika hadiythi ya Zaiyd bin Khaalid radhiya Allaahu ‘anhu kutokana na Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam amesema:

   Ramadhaan ni mwezi wa ukarimu, huruma, rahma na mapenzi.

                               
“Atakayemfutarisha aliyefunga, atapata ujira kama ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga” Imepokelewa na Tirmithiy, Kitabu cha Swawm kutokana na Mjumbe wa Allaah Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam, mlango yaliyo kuja katika fadhila za kumfutarisha aliyefunga.

Ndugu yangu katika iman, hatutowi cho chote katika njia ya Allaah kwa kuwa labda hatuna, lakini wako wenye nacho na hawatowi, hupendi kuwa katika wenye kushajiisha watu kutowa walichoruzukiwa na Allaah, hupendi kuwa miongoni mwa wenye kuamrisha mema na kukataza mabaya, kazi aliyo ifanya Mjumbe wa Allaah Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam, ukawa mbora? Qur aan inasema:

 

“Na ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa Mwenyezi Mungu na akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni katika Waislamu” Fussilat aya ya 33.

Ndugu yangu katika iman, hatukujaaliwa kumuona al Habiyb Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam wala Sahaza zake radhiya Allaahu ‘anhum wala walio kuja baada yao, lakin bado wako waja wema hatuwajui na karibu wote wenye kuonyesha kwenye TV sio wema wala kitu chenye kuitwa wema hawakitambui, sasa wewe unakodolea macho kwa kuwatizama na unawawekea wazi masikio yako na kuwasikiliza yote wayasemayo na baadae kuwa mtangazaji na msambazaji wao; je unataka kuangalia na kusikia chenye kuburudisha macho na moyo?  Kwanini basi mwezi mzima usifunge TV na kuamuwa kwenda kuwatafuta waja wema wa Rahmaan utawapata au hata wenye kuwapenda hao waja wema katika mikusanyiko ya kheri, sio mipira wala kucheza bao au karata, mikusanyiko ya kheri inayo hudhuriwa na kushuhudiwa na Malaikatur Rahmaan.

 

Ndugu yangu katika iman, tembelea misikiti katika eneo lako utakuwa waja wa Rahmaan; wako wenye kuswali, kusoma Qur aan, kulete adh-kaar, kusikiliza mawaidha na kadhalika, je hupendi wewe na rafiki zako au watoto wako wawe kama hao utaowakuta msikitini?  Jiulize wako wapi watoto wako? Wako wapi rafiki zako? Kwa nini huwashajiishi na kuwashawishi washiriki na waja wa Rahmaan katika yenye kumfurahisha Rahmaan na yenye kuwafikisha kufikia lengo alilo liweka Rahmaan kufikiwa na wenye kufunga Ramadhaan.

 

Ndugu yangu katika iman, hakikisha kuwa katika mwezi huu unatumia wakati wako mwingi kusoma Qur aan na kuhitimisha zaidi ya mara moja, jitafutie au asisi kikundi kidogo cha watu make pamoja na kusoma Qur aan japo kwa muda wa saa moja kila siku, jiwekea lengo katika Ramadhaan hii la kuhifadhi japo juzuu moja au sura na kujifunza tafsiri yake.

 

Ndugu yangu katika imani, ni mengi ya kufanya ya kheri na mazuri katika Ramadhaan bila ya kusahau kuwa ni miongoni mwa kawaida tulizojiwekea kabla ya kuanza kwa Ramadhaan kuweka siku au wakati wa kujikumbusha hukumu za Swawm, yaliyo wajibu kuyawacha mwenye kufunga, yaliyo halali na kuruhusiwa kwa mwenye kufunga, yenye kuchukiza kwa aliye funga, yenye kuharibu funga na kadhalika.

 

Ndugu zangu katika imani, pia ni katika desturi tulizojiwekea kutafuta siku au wakati kabla ya kumalizika kwa ibada ya funga kukumbushana na kuelezana kila yenye kuhusiana na zakaatul fittr; hukumu za ‘Iyd, swalla ya ‘iyd; maqaasiyd ya ‘iyd; funga za sunnah zikiongozwa na siku sita (6) za Shawwaal; nini baada ya Ramadhaan na kadhalika; yote hayo kwa lengo la kutaka kusaidiana na kushirikiana katika kukumbushana na kushajiishana kutekeleza mema kwa tawfiki yake Rahmaan kuweza kufikia kukubaliwa ibada yetu tukufu ya swawm; kusamehewa madhambi yetu;kurehemewa na kutolewa katika Moto na kuwa katika wenye kupongezwa na Malaika siku ya ‘iyd wakati wa kwenda kuswali swallla ya ‘iyd kwa kuambiwa Mabrook ‘alaykum kwa kukubaliwa swawm yenu.
Ndugu zangu katika imani, yote haya na mengine kama haya ambayo hupatikana ndani ya mwezi katika siku zake tofauti kadiri ya wasaa ya wahusika, huwa na lengo la kutaka kuweza kuwaanda waislamu na kuwatayarisha kuwa tayari kuitekeleza ibada tukufu ya swawm kama atakavyo Mola kwa kupitia namna au njia aliyoipita na aliyotuelekeza na kutufundisha Mjumbe wa Allaah na Kigezo chetu Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wa Sallam itakayokubaliwa na Allaah.
Ndugu Waislamu, Ramadhaan inakuja kwa lengo la kutusafisha, kutufunza heshima, utii na kadhalika, tuwe wavumilivu katika kupata mafundisho yake na tuwe wastahalimivu katika kukabiliana na mitihani inayotukuta kila siku. 
Ndugu Waislamu, Ramadhaan haiwi Ramadhaan kama hatutokuwa tayari kusameheyana, kukumbushana, kuwaidhiana, kuusiana na kuamrishana mema na kukatazana maovu katika shughuli zetu zote za kila siku, kurekebishana kwa namna itakayoheshimu kila mmoja utu wake.
Ndugu Waislamu, tumuombe ar-Rahmaan Atuwafikishe katika kuipokea na kuitekeleza ibada ya swawm ya Ramadhaan, tumuombe Atuwafikishe katika kuishi na kukaa na Ramadhaan kwa kuifunga, kutekeleza Ayatakayo Muumba, na kuachana na makatazo Yake, pia twamuomba Muumba Atupe uwezo wa kufikisha amana kama alivyoifikisha Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam, Atutie mapenzi baina yetu, mapenzi yatayotupelekea kuwa tayari kusameheyana, ili na Yeye atusamehe kama alivyoahidi, kuhurumiana, kuvumiliana, kuheshimiana na kukosoana na kurekebishana kwa njia na namna alivyokuwa akiwarekebisha Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa‘alaa Aalihi Wasallam Sahaba zake Radhiya Allaahu ‘Anhum.

No comments:

Post a Comment