Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kurejeshwa amani
na utulivu huko Guinea Conakry baada ya makumi ya watu kuuawa kufuatia
mapigano ya kikabila yaliyotokea katika mji mmoja nchini humo. Ban
ki-Moon kupitia msemaji wake ameeleza wasi wasi mkubwa ulionao Umoja wa
Mataifa kuhusiana na mapigano ya kikabila yaliyozuka katika mji wa
N'Zerekore ambao ni wa pili kwa idadi kubwa ya watu nchini humo baada ya
mji mkuu Conakry. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewataka wananchi wa
nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kudumisha utulivu na amani na
kujiepusha na hatua yoyote ile yenye kupelekea amani na usalama kuwa
hatarini. Aidha Ban ki-Moon amewataka viongozi wa kitaifa na kikabila
kulinda kudhamini usalama wa roho na mali za watu na kuheshimu sheria.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito pia wa kuandaliwa mazingira
mazuri kwa ajili ya uchaguzi wa Bunge uliopangwa kufanyika mwezi
Septemba mwaka huu. Zaidi ya watu 54 wameuawa hadi sasa katika
mapigano makali ya kikabila yaliyotokea katika mji wa N'Zerekore nchini
Guinea Conakry. Inaelezwa, mapigano hayo yalianza baada ya watu wa
kabila la Guerze kumpiga na kumuua kijana mmoja wa ukoo wa Konianke kwa
tuhuma za wizi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment