Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Thursday, August 15, 2013

Ulaya wanavyomuandika Sheikh Ponda


IMG-20130814-WA0001
Nchini Uingereza gazeti la Daily Mail linalotoka kila siku limeandika kwamba, Katibu wa Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda Issa, anaweza kuwa mtuhumiwa mkuu wa tukio la wasichana wawili raia wa nchi hiyo waliomwagiwa tindikali hivi karibuni.
Kirstie Trup (18) na Katie Gee (18t), wakazi wa Hampstead, Kaskazini-Magharibi mwa London ambao wanatibiwa hospitali moja nchini humo, walimwagiwa tindikali Agosti 7, mwaka huu huko visiwani Zanzibar, madai makubwa yakiwa ni kuvaa mavazi yasiyoendana na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
MAHUBIRI YA PONDA YATAJWA
Pamoja na kupigwa risasi begani huko Morogoro, kwa mujibu wa gazeti hilo lililoingia mtaani Jumatatu iliyopita, pamoja na kutomhusisha moja kwa moja, Shehe Ponda aliwahi kutoa mahubiri Zanzibar ambayo kwa akili ya kawaida ni kama yalichochea wasichana hao kumwagiwa tindikali.
Gazeti hilo liliandika kuwa kuna uwezekano Kikundi cha Uamsho kuhusika huku mahubiri ya Ponda yakihusishwa na utendaji wa kundi hilo, jambo ambalo hata polisi wanalihisi.
Gazeti hilo lilidai kuwa Shehe Ponda alipigwa risasi huko Morogoro huku akiwa anasakwa huko Zanzibar kwa sababu ya mahubiri yaliyosemekana yalikuwa ya kichochezi.
“Alitembelea Zanzibar wiki kadhaa zilizopita na baada ya mahubiri ya chuki aliyoyatoa kwa wafuasi wake akiwataka kuandamana kupinga ukoloni ndipo Kirstie na Katie wakamwagiwa tindikali.
“Tindikali imekuwa ndiyo silaha kubwa Zanzibar ikitumiwa na kundi hilo linalotaka kujitenga katika nchi ya Tanzania na kuongozwa na Sharia,” liliandika Dail Mail la Uingereza.
GAZETI LINGINE
Gazeti lingine la The Telegraphic la nchini humo liliandika: “Shehe Ponda alitumia wiki nzima Zanzibar mwanzoni mwa Agosti akihubiri misikitini akiunga mkono maandamano ‘kama ya Misri’ hadi ‘memba’ wao 10 waliofungwa waachiwe.
“Alikuwa akizunguka akiwaambia vijana wafanye maandamano yasiyokuwa na kikomo kuonesha wao wana nguvu.”
MTANZANIA AISHIYE LONDON AFUNGUKIA HALI ILIVYO
Mtanzania aishiye Jiji la London, Uingereza (jina tunalo) aliliambia Risasi Mchanganyiko juzi kwamba, baadhi ya Waingereza wametokea kumchukia Shehe Ponda baada ya habari yake na picha kuchapishwa kwenye gazeti hilo likimhusisha na tindikali ya wasichana hao waliokuwa wakijitolea kufundisha huko Zanzibar.
“Waingereza wengi wametokea kumchukia Shehe Ponda huo ndiyo ukweli. Wanasema kama Tanzania hawataichukulia ‘siriasi’ ishu hiyo, basi Shehe Ponda siku akitua London, itakula kwake,” alisema Mbongo huyo.
Aliongeza kuwa sera ya Uingereza tangu Mkutano wa Berlin, Ujerumani mwaka 1884/85 wa nchi za Ulaya kuweka maazimio ya kuitawala Afrika, kila nchi ilitakiwa kulinda watu wake hivyo sera ya Uingereza kwa sasa ni kulinda raia wake wa nje na ndani kwa gharama zozote zile.
“Unakumbuka ule Mkutano wa Berlin mwaka elfu moja mia nane na themanini na nne, nchi za Ulaya ziliweka maazimio kuhusu kujilinda na kuingia katika makoloni ya Afrika.
“Uingereza iliamua kuweka sera ya kulinda raia wake wa ndani na nje kwa gharama yoyote ile.

“Ndiyo maana naweza kusema Ponda atachukiwa tu mpaka mwisho. Unajua Waingereza siku zote wanawachukia watu wenye misamamo mikali, watu wanaoweza kufanya lolote bila kujali uhai wa mtu mwingine,” alisema Mtanzania huyo.
WABONGO WAITAKA SERIKALI KUMWONGEZEA ULINZI PONDA

Jijini Dar es Salaam, juzi baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili nje ya wadi aliyolazwa Shehe Ponda, Hospitali ya Muhimbili waliitaka serikali kumwongezea ulinzi kiongozi huyo.

Bakari, mkazi wa Kigogo, Dar alisema: “Tayari magazeti ya Ulaya yameanza kumtuhumu Ponda kwamba alichochea wale Wazungu kumwagiwa tindikali, ni vyema kama serikali ikawa makini naye.
“Wenzetu (Waingereza) wana uwezo mkubwa na zana kibao, wanaweza kutua juu ya paa la hospitali hapa wakamchukua na kumpeleka Uingereza.”
KISA CHA PONDA NA SERIKALI

Licha ya watu kuitaka serikali kumlinda zaidi Shehe Ponda, tayari kiongozi huyo yuko chini ya ulinzi hospitalini alikolazwa.

Inadaiwa kuwa Shehe Ponda akipona atafikishwa mbele ya sheria kujibu tuhuma za uchochezi wakati akihubiri huko Zanzibar hivi karibuni wakati bado akiwa kwenye kifungo cha nje baada ya kuhukumiwa kifungo cha nje miezi kadhaa iliyopita.
Wakati hayo yakiendelea Bongo, huko London wasichana waliomwagiwa tindikali wanaendelea na matibabu katika Hospitali za Chelsea na Westminster ikielezwa kuwa mmoja atawekewa ngozi ya bandia kutokana na kuharibiwa kupita maelezo.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete alilaani vikali kitendo cha kinyama walichofanyiwa wasichana hao kwa maelezo kuwa ni aibu kwa Tanzania.

No comments:

Post a Comment