SHEIKH Mkuu wa Wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya Nuhu Mwafilango,
ameshambuliwa na kujeruhiwa kwa panga baada ya kuzuka kwa vurugu katika
msikiti mkuu wa wilaya ya Kyela.
Vurugu hizo zilisababisha kujeruhiwa vibaya kwa watu wengine watatu baada ya kushambuliwa kwa mapanga na visu.
Mashuhuda wa tukio hilo wameiambia Tanzania Daima kuwa vurugu hizo
zinazoaminika kuwa ni za kugombea madaraka, zilizuka majira ya saa mbili
asubuhi jana wakati sheikh huyo akiongoza ibada ya Idd el Fitri katika
msikiti huo.
Imedaiwa kuwa kundi la vijana likiongozwa na mwanafunzi mmoja wa shule
ya sekondari ya kutwa ya Kyela (jina limehifadhiwa) alimshambulia
kiongozi huyo kwa panga na kusababisha vurugu kubwa.
Imeelezwa kuwa kikundi hicho cha vijana ambao baadhi yao wanadaiwa
kukodiwa kutoka katika misikiti ya mikoa jirani, wakiwa na mapanga,
nondo na visu walianza mashambulizi hayo, na ndipo wakakumbana na hasira
za waumini wengine waliokuwa wamejiandaa kukabiliana na mashambulizi
hayo.
Mmoja wa vijana waliojeruhiwa vibaya kichwani ametajwa kwa jina la
Hamis Hussein ambaye alipambana na vijana walioanza kumshambulia sheikh
huyo.
Imedaiwa kuwa kulikuwa na fununu za kuzuka kwa mapigano hayo, hatua
iliyofanya uongozi wa msikiti kutoa taarifa polisi ambao walijipenyeza
katika swala hiyo ya Idd.
Wengine waliojeruhiwa vibaya ni mmoja aliyetajwa kwa jina la Magogo
anayetuhumiwa kuchochea vurugu na mapigano hayo katika kile
kilichoelezwa jitihada za kuwaondoa viongozi walioko msikitini na
kuwadhamini vijana ambao wanadaiwa kuwa ni waasi wa msikiti huo.
Akizungumza na Tanzania Daima Mwenyekiti wa BAKWATA Wilaya ya Kyela
Daud Mwenda alisema kuwa kikundi hicho kinapingana na uongozi uliopo
msikitini hapo hivyo wanataka kushinikiza waumini wengine waupindue
uongozi uliopo.
Mganga wa zamu katika Hospitali ya Wilaya ya Kyela ambaye hakutaka
kutaja jina lake alikiri kupokea majeruhi watatu waliotokana na vurugu
hizo.
Kwa upande wake Afisa Tarafa ya Unyakyusa Helly William alisema kuwa
ofisi yake imepokea taarifa za vurugu katika msikiti huo na kudai kuwa
jambo hilo limewasikitisha sana kama viongozi wa serikali.
No comments:
Post a Comment