Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Friday, August 16, 2013

MWAKYEMBE: NITAANIKA VIGOGO WA ‘UNGA’ LEO



Siku moja baada ya kufanya ziara ya ghafla Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema leo ataweka hadharani majina ya watu wanaosafirisha dawa za kulevya nchini.

Dk Mwakyembe juzi alifanya ziara hiyo JNIA kukagua utendaji kazi kwenye uwanja huo ikiwa ni siku chache baada ya kutokea kashfa ya kupitishwa kwa dawa za kulevya na baadhi ya Watanzania wakiwamo wasanii kukamatwa sehemu mbalimbali duniani.

Aidha, hatua ya waziri huyo imekuja siku tatu baada ya ahadi aliyotoa akiwa Mwanza kwamba katika kipindi cha wiki mbili kuanzia juzi, atahakikisha anawakamata vigogo wote walio katika mtandao wa usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya kupitia viwanja vyote vya ndege nchini.

Akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana iliyoandaliwa na Taasisi ya Jitambue Foundation, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana, Dk Mwakyembe alisema yuko tayari kufa katika vita hivyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake jana, Dk Mwakyembe alisema: “Kesho (leo) nitawataja wanaojihusisha na dawa za kulevya. Kwa sasa nakamilisha ushahidi wa kutosha ikiwa ni pamoja na picha za wahusika.”

Aliwaonyesha waandishi wa habari picha ya mtuhumiwa mmoja ambaye alisema alikamatwa saa nane baada ya waziri huyo kufanya ziara uwanjani hapo. “Ninataka watu wafahamu wanaoliingiza taifa hili katika aibu hii, ambayo inasababisha Watanzania wasiaminike katika viwanja vya ndege vya mataifa mengine.”

“Hatuwezi kuwa taifa la kuogopaogopa, hii ni vita ya kusafisha nchi yetu, kwani ni nani mwenye mkataba na Mungu kuwa ataishi milele?” alihoji Waziri huyo alipokuwa akijibu swali kuwa suala la kuwataja watu wanaowafichua wasafirisha unga linaweza likaweka rehani maisha yake.

“Kama hupendi joto usiingie jikoni”, alisema.

Akizungumzia watendaji wa JNIA kuhusiana na dawa za kulevya, alisema: “Mfanyakazi yeyote atakayebainika kuhusika kuwasaidia wasafirisha unga atafukuzwa kazi na ambaye atafanya juhudi ya kuwakamata wasafirishaji hao atapewa zawadi.”

“Kuna watu wanadhani tunafanya mzaha katika jambo hili. Jana baada ya mimi kuondoka usiku wa saa 2:30 huyu (kijana aliyekamatwa) akaingia na mzigo,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza kuwa alikamatwa na kete 86 za dawa aina ya heroini na misokoto 34 ya bangi aliyokuwa akiisafirisha kwenda Italia kupitia Zurich.

Aliiagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuwatunuku wafanyakazi waliofanikisha kukamatwa kwa kijana huyo.

Akizungumzia hali ya Uwanja wa JNIA baada ya kufanya ziara juzi, Dk Mwakyembe alisema tatizo halipo kwenye vitendea kazi, bali wafanyakazi wasiokuwa waaminifu.

“Tulikagua ili kujiridhisha kwa vifaa vilivyopo na tumeridhika kuwa kiwanja ni kizuri, hata Shirika la Kimataifa linalokagua viwanja vya ndege limeukubali kuwa uko vizuri katika vifaa kwa hiyo tatizo lipo kwa sisi wenyewe wenye dhamana.

“Ukaguzi huu utaendelea katika viwanja vyote hapa nchini mpaka bandarini na kila tutakayemkamata tutachapisha picha yake,” alisema Dk Mwakyembe.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini huku wengine wawili wakikamatwa Hong Kong wakiwa na dawa za kulevya zenye thamani ya mabilioni ya fedha.

Akizungumzia kijana aliyekamatwa, mmoja wa askari ambaye hakupenda jina lake litajwe alisema: “Tulipewa taarifa za kiitelijensia saa tisa alasiri na raia mwema kuwa kuna mtu anasafiri na atafika uwanjani hapo kuanzia saa moja usiku na anasafiri kwenda Italia.

“Baada ya kupewa taarifa hizo tulijipanga na ilipofika saa 1:49 usiku alifika kijana mmoja, kwa kuwa tulishaelezwa wajihi wake, hatukupata shida, tulimchukua, tukamhoji na tulipompekua tulimkuta na kete 84.”

Kamanda wa Vikosi vya Uwanja wa Ndege, Deusdedit Kato akizungumzia tukio hilo alisema: “Alikuwa kwenye ukaguzi wa kawaida akiwa kwenye mstari na ilipofika zamu yake aliamriwa akae pembeni akafanyiwa upekuzi.

Alisema Mtanzania anatumia muda mwingi kukaa Italia na kwamba polisi wanaendelea kumfanyia mahojiano ili kujua alikozitoa na mhusika anayempelekea huko.

Alisema dawa hizo zimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kupimwa ili zifahamike ni za aina gani na anatarajiwa kufikishwa Mahakama ya Kisutu kati ya leo na Jumatatu kutegemea kukamilika kwa upepelezi.

No comments:

Post a Comment