Ni kuchanganyika kwa mwanamke na mwanamme au kwa wingi wanawake na wanaume.
Kuchanganyika huku ni aina tatu:
1. Kuchanganyika wanawake na mahaarim wao wa kiume, hili jambo limeruhusiwa katika sheria ya Kiislam.
2. Kuchanganyika wanawake na wanaume kusababisha ufisadi, hili limeharamishwa katika sheria.
3. Kuchanganyika
wanawake na wanaume sehemu za kutafuta elimu; mashuleni, vyuoni, au
mahospitalini, maofisini na sehemu mbalimbali za kazi. Na katika vyombo
vya usafiri kama mabasi, matreni, ndege, n.k. Huenda mtu akaona kuwa
hakuna fitna katika michanganyiko ya sehemu hizo, lakini hakika kila
sehemu kuna fitna itakayozuka maadam tu hakuna tahadhari za kuepukana
nazo.
Maasi
haya yanadhihirika sana katika Jamii yetu ikiwa ni majumbani mwetu,
katika shughuli zetu mbali mbali za furaha na misiba, katika vikao mbali
mbali ikiwa ni vya mikusanyiko ya kijamii au ya kifamilia.
Pia
aghalabu shemeji huwa anaishi nyumba moja na mke wa wa kaka yake bila
kuhisi tabu au kuona kuwa hakuna madhara yoyote na hali Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametutahadharisha katika Hadiyth
ifuatayo:
))إياكم والدخول على النساء، قالوا: يا رسول الله أرأيت الحمو؟ قال: الحمو الموت(( متفق عليه
((Tahadharini
kuwaingilia (kuingia majumbani mwao) wanawake)) Wakasema: Ewe Mjumbe wa
Allaah, je, vipi kuhusu shemeji? Akasema: ((Shemeji ni mauti)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Ni
mazoea ambayo yamekuwa mazito kuyaacha kwa wasiotaka kufuata amri za
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na wasiokhofu adhabu Zake. Ama kwa walio
kinyume na hivyo hutahadhari na jambo hili na kuanza kubadilisha nidhamu
ya maisha katika nyumba zao; kwa kumzuia shemeji kuishi katika nyumba
moja na mwanamke au ikiwa mtu kafanya ziara, mwanamke hubakia katika
chumba mbali na kile alicho shemeji yake kama ukumbini, au chumbani
mwake hadi atakapoondoka.
Ajabu
ni kwamba unapokataza, baadhi ya watu huona kwamba ni jambo la
kuzidisha tabu katika dini, au hutaka kujua dalili ya makatazo haya kwa
kudhani kuwa hakuna makatazo. Swali ni kwamba: "Nani aliyekataza maasi
haya?" Jibu ni kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ndio waliokataza kama
tunavyoelezea dalili zake hapa chini.
Makatazo Ya Ikhtilaatw Katika Qur-Aan Na Sunnah
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
((وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاء حِجَابٍ))
((Na mnapowauliza wakeze haja waulizeni nyuma ya mapazia)) [Al-Ahzaab: 53].
((قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ذَلِكَ أَزْكَى لَهُمْ))
((Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao. Hili ni takaso bora kwao)) [An-Nuwr: 30].
((وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَى جُيُوبِهِنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاء بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاء بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُوْلِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَى عَوْرَاتِ النِّسَاء وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ وَتُوبُوا إِلَى اللَّهِ جَمِيعًا أَيُّهَا الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ))
((Na
waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao,
wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi
zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au
baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao,
au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake
wenzao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanaume wasio
na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyokhusu uke. Wala
wasipige chini miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha. Na tubuni
nyote kwa Allaah, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa)) [An-Nuwr: 31].
Ameamrisha
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Aayah hizo tukufu kuinamisha
macho, na kulinda tupu, hivyo bila shaka haya ni kutokana na
kuchanganyika baina ya mwanamke na mwanamume ndipo ikatoka amri ya
makatazo ya hayo ya Ikhtilaatw.
Amri
ya kuinamisha macho ni kuepusha matamanio ya uzuri atakaouona mmoja kwa
mwenzake, kuona, kusikia kote kunampeleka mtu katika zinaa kama
anavyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
عن أبي هريرة رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم قال)) : كتب على ابن آدم نصيبه من الزنا مدرك ذلك لا محالة , العينان زناهما النظر , والأذنان زناهما الاستماع , واللسان زناه الكلام , واليد زناها البطش , والرجل زناها الخطا , والقلب يهوى ويتمنى , ويصدق ذلك الفرج أو يكذبه (( أخرج البخاري ومسلم
Kutoka
kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Ameandika kila sehemu ya
zinaa ambayo humuingiza mtu katika shauku. Hakutokuwa na kuikwepa. Zinaa
ya macho ni kutazama, ya masikio ni kusikiliza, ulimi ni kunena maneno,
mkono ni kuunyoosha, mguu ni hatua zake na moyo hupata matamanio, na
tupu husadikisha (hutenda) au kukadhibisha [huacha])) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Vile vile,
قال صلى الله عليه سلم: ((لا يخلوّنّ أحدكم بامرأة إلا مع ذى محرم )) متفق عليه
Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hawi faraagha
mmoja wenu pamoja na mwanamke ila awepo Mahram wake)) [Al-Bukhaariy Na Muslim].
Kuchanganyika
mwanamke na mwanamume katika sehemu moja ndio maana ya Hadiyth hii.
Sasa vipi anayesababisha fitna na anayesababishiwa kuingia katika fitna
wakakaa pamoja?
Na
Mahram aliyekusudiwa hapo ni; mume au mwanamume ambaye hawezi kumuoa
mwanamke huyo anayekusudiwa katika Hadiyth, mfano: kaka, ami, mjomba,
mtoto wa dada au kaka, au kaka wa kunyonya ziwa moja. Asichanganyike na
mwengine zaidi ya hao kwani
عن عمر رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم: ((ما خلا رجل بامرأة إلا كان الشيطان ثالثهما)) الترمذي
((Kutoka
kwa 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hachanganyiki mwanamume na mwanamke ila
shaytwaan huwa ni watatu wao)) [At-Tirmidhiy].
Tumeonywa
na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Aayah nyingi kwamba shaytwaan
hutuamrisha maovu na uchafu, huanza kumtia binaadamu katika nafsi yake
mawazo ya matamanio mwishowe nafsi humfikisha mtu kufanya maovu kwani
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((إِنَّ النَّفْسَ لأَمَّارَةٌ بِالسُّو))
((Kwa hakika nafsi ni mno kuamrisha maovu)) [Yuwsuf: 53].
Tumeelezewa
kisa cha Nabii Yuwsuf ('Alayhis Salaam) alipokuwa chumbani pekee na mke
wa Mfalme au Waziri ambaye alimtamani Yuwsuf japokuwa alikuwa ni mtoto
aliyemnunua na kumlea hadi akafikia umri wa kubaleghe:
((وَرَاوَدَتْهُ الَّتِي هُوَ فِي بَيْتِهَا عَن نَّفْسِهِ وَغَلَّقَتِ الأَبْوَابَ وَقَالَتْ هَيْتَ لَكَ قَالَ مَعَاذَ اللّهِ إِنَّهُ رَبِّي أَحْسَنَ مَثْوَايَ إِنَّهُ لاَ يُفْلِحُ الظَّالِمُونَ))
((Na
yule bibi wa nyumba aliyokuwamo Yuwsuf alimtamani kinyume cha nafsi
yake, na akafunga milango. Akamwambia: Njoo! Yuwsuf akasema:
Audhubillahi! Najikinga na Allaah. Huyu bwana wangu kaniweka maskani
nzuri, na hakika wenye kudhulumu hawatengenekewi)) [Yuwsuf: 23]
Tukio
hilo lilikuwa baada ya kuweko kuchanganyika pekee mwanamke na mwanamume
japokuwa hakudhania Yuwsuf kwamba mke wa Mfalme au Waziri atafikia
kumtamani na kutaka kuingia naye katika maovu. Lakini kwa Rahma ya
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) alimuoka Nabii Yuwsuf (‘Alayhis Salam).
((وَلَقَدْ هَمَّتْ بِهِ وَهَمَّ بِهَا لَوْلا أَن رَّأَى بُرْهَانَ رَبِّهِ كَذَلِكَ لِنَصْرِفَ عَنْهُ السُّوءَ وَالْفَحْشَاء إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُخْلَصِينَ))
((Na
hakika yule mwanamke alimtamani, na Yuwsuf angelimtamani lau kuwa
hakuona ishara ya Mola wake Mlezi. Hayo hivyo ni kwa ajili Tumuepushe na
uovu na uchafu. Hakika yeye alikuwa katika waja wetu waliosafishwa)) [Yuwsuf: 24].
Anasema
Shaykh ‘Abdullaah Swaalih Al-Faarisy katika kusherehesha Aayah ya 23-24
ya Surah hiyo anasema: “Na mambo ya kukaa mwanamume na mwanamke peke
yao yamekatazwa kabisa katika Sharia kwani lazima yataleta mabaya. Wala
usiseme: “huyu shemeji yangu”-“ndugu wa mke wangu” au “shemeji yangu” -
“mke wa ndugu yangu.” Wote hao hatari kwako na kwao na walio kama hao.
Faragha kitu kibaya kabisa. [Shaykh ‘Abdullaah Swaalih Al-Faarisy,
Qurani Takatifu, Chapa ya nane, uk. 320].
وقال عليه الصلاة والسلا: (( المرأة عورة ...)) الترمذي
Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwanamke ni uchi…). [At-Tirmidhiy].
Maana
ya kuwa ni 'uchi' ni kwamba haijuzu kutazama mapambo yake wala sehemu
ya mwili wake hivyo kuchanganyika kunaleta maana zote hizo.
وقال عليه الصلاة والسلام: ((ما تركت بعدي فتنة هي أضر على الرجال من النساء)) البخاري
((Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Sikuacha baada yangu fitna ambayo ina madhara kwa wanaume kama wanawake)) [Al-Bukhaariy].
Sehemu Zinazotokea Mchanganyiko
Nje kama madukani, sokoni, kazini …
Mwanamke
ameamrishwa kubakia nyumbani kwake ila kwa dharura tu na akitoka
anatakiwa awe amejifunika na kujisitiri vizuri kwa hijaab iliyokamilika
kisheria inayopaswa kutimizwa, nayo ni mavazi yanayotakiwa yatimize masharti nane zifuatazo:
1. Mwili wote ufunikwe isipokuwa uso na viganja vya mikono.[Maulamaa wengine wameona hata uso na mikono pia ifunikwe].
2. Nguo isiwe yenye mapambo.
3. Lazima iwe nzito kiasi isiwe yenye kuonyesha mwili.
4. Lazima iwe yenye kupwaya na sio ya kubana hata ikaonyesha mwili wake.
5. Asijitie manukato.
6. Isishabihi vazi la kiume.
7. Isishabihi mavazi ya kikafiri
8. Isiwe ya kujionyesha, maana kwamba isiwe kwa ajili ya kiburi kuwa ni vazi bora kuliko la mwengine.
Amri ya kubakia nyumbani ni Anaposema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ))
((Na kaeni majumbani kwenu)) [Al-Ahzaab: 33].
Kwa
jinsi iliyvokuwa ni muhimu mwanamke kubakia nyumbani, hata Swalah yake
tumeambiwa kuwa ni bora kwake kuswali nyumbani kuliko kwenda Msikitini.
Na
aliporuhusu wanawake kwa kuwakataza Maswahaba wasiwazuie kwenda kuswali
misikitini, na walipokuwa wakihudhuria, alipendelea mlango mmoja uwe
kwa ajili ya kuingia wanawake:
عن ابن عمر رضي الله عنهما قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: (( لو تركنا هذا الباب للنساء)) . قال نافع : فلم يدخل منه ابن عمر حتى مات" أخرجه أبو داود بسند صحيح
Kutoka
kwa Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Tungeliuacha huu mlango kwa
ajili ya wanawake)). Kasema Naafi': "Hakuingia tena Ibn 'Umar mlango huo
mpaka kufariki kwake". [Abu Daawuwd kwa isnaad Swahiyh]
وعن أم سلمة رضي الله عنها قالت : "أن النساء في عهد رسول الله صلى الله عليه وسلم كن إذا سلمن من المكتوبة قمن وثبت رسول الله صلى الله عليه وسلم ومن صلى من الرجال ما شاء الله فإذا قام رسول الله صلى الله عليه وسلم قام الرجال" أخرجه البخاري . قال ابن شهاب (وهو الزهري ): فأرى والله أعلم أن مكثه لكي ينفذ النساء قبل أن يدركهن من انصرف من القوم .
Kutoka
kwa Ummu Salamah (Radhiya Allaahu 'anha) ambaye amesema: "Wanawake
katika zama za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
walikuwa wakimaliza kuswali Swalah za fardh waliondoka, na akabaki Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wanaume waliojaaliwa
kuswali, kisha alipoinuka Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) na wao waliinuka" [Al-Bukhaariy na Muslim]. Amesema
Ibn Shihaab (ambaye ni Az-Zuhriy) naona kuwa na Allaah Ndiye Mjuzi
zaidi kuwa kubaki kwake Mtume msikitini ni kuachia nafasi ya wanawake
kuondoka kwanza kabla ya wanaume.
Vile
vile, itakapombidi mwanamke kutoka nje kwa dharura basi ahakikishe kuwa
anatekeleza maamrisho ya Mola wake katika hali hiyo, kama tulivyotaja
kuhusu hijaab na pia katika maongezi akaze sauti yake.
((فَلَا تَخْضَعْنَ بِالْقَوْلِ فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ وَقُلْنَ قَوْلًا مَّعْرُوفًا))
((Basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno mema)) [Al-Ahzaab: 32].
Hali Inayoruhusu Kuchanganyika
Kuna
baadhi ya hali za dharura zinazoruhusika kuchanganyika, na mfano wa
hali hizo ni kama imetokea mwanamke kuharibikiwa safarini, kupotea,
kutaka kudhuriwa na watu au kuvunjiwa heshima na ikabidi kumuokoa na
kumsindikiza hadi penye amani au palipo watu wake, kupatwa na ajali
kukawa hakuna wanawake wa kumsaidia ila wanaume tu, na hali nyinginezo
mbalimbali za dharura kama za matibabu ikiwa hakuna madaktari wa kike
n.k.
Katika Haram (Makkah)
Baadhi
ya watu wanatoa hoja ya Msikiti wa Makkah wanapoona kwenye
matelevisheni au kwa waliojaaliwa kufika kuwa kule kuna mchanganyiko wa
wanaume na wanawake. Wengi wanashindwa kuelewa kuwa hali ile ya dharura inayosababisha vile si hoja
ya kumfanya Muislamu kuruhusika kuchanganyika kwani huko kuna ulazima
wa kutekeleza Twawaaf na haiwezekani kuwatenga wanawake katika ibada hii
kutokana na hali ilivyo, watu kuhitajika kufanya Twawaaf wanapoingia tu
Haram, umbali wanaotoka watu nchi kwa nchi, na muda wa ibada hiyo na
kutowezekana kupangika zamu ya utekelezaji wa ibada hiyo kwa wanaume na
wanawake ndio kukapatikana dharura hiyo.
Pamoja
na kuwepo hali hiyo na ugumu huo wa kuwatenganisha wanawake na wanaume
kwenye Twawaaf, askari waliomo Msikitini hapo wanajaribu sana
kuwatenganisha wanawake na wanaume katika kuswali ingawa wengi huwa
wakaidi.
Katika Kazi
Ikiwa
kuna dharura ya kufanya kazi na ikasababisha kuchanganyika, kwani
katika kufanya kazi mfano biashara kutakuweko wanawake na wanaume, ila
lazima izingatiwa sheria isemavyo na kutekeleza inavyopasa na kuepukana
na makatazo.
Kuhudumia Wageni
Wanapokuja
wageni wa mume au jamaa zake mke lakini ambao sio mahaarim wake,
anaweza kuwahudumia kwa kuwatayarishia chakula kama kuwapelekea, muhimu
aweko mumewe. Hii ni kutokana na dalili ifuatayo:
لما
عرَّسَ أبو أُسَيد الساعِدِيُّ دعا النبيَّ صلى الله عليه وسلم وأصحابَهُ
فما صنَع لهم طعاماً ولا قدم إليهم إلا امرأتُهُ أمُّ أُسيد، بَلَّتْ (وفي
رواية: أنقعت) تَمَراتٍ في تَوْر من حجارةٍ منَ الليل، فلما فَرَغَ
النبيُّ صلى الله عليه وسلم من الطعام أماثَتْه له فسقَتْهُ تتْحِفُه بذلك.
(فَكَانَتِ امْرَأَتُهُ يَوْمَئِذٍ خَادِمَهُمْ. وَهْيَ الْعَرُوسُ)
Abu
Asyad As-Saa'idiy alipooa, alimualika Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) pamoja na Maswahaba zake. Hakuna aliyetayarisha
chakula au kuwahudumia isipokuwa mkewe Ummu Asyad. Aliroweka tende
katika bakuli la udongo usiku uliopita. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) alipomaliza kula, alimpakulia na kumtunikia, hivyo
mkewe akawa ndiye mwenye kuwahudumia wageni na alikuwa ndiye bi harusi. [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo].
Katika Kusaidia Kazi Za Jihaad
Inafaa
wanawake kusaidia katika kazi kama hizo kama kuwatibu waliojeruhiwa, au
kuwapelekea maji n.k. kwani hivyo walifanya wanawake zama za Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na kazi kama hizo kwa
ajili ya maslahi wa Waislamu.
Swafiyyah bint 'Abdul-Mutwalib, Shangazi yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alishiriki katika kuwapiga makafiri na kumkinga Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), pia
aliweza kumuua Myahudi kwa kumkata kichwa chake hata wakaingiwa na
khofu Mayahudi waliotaka kuvamia kambi waliyoachwa wanawake, watoto na
wazee kwa kudhania kwamba kuna mwanamume hivyo hawakuthubutu
kuwasogelea.
Vile
vile katika kushirikiana kutekeleza kazi za Dini kama kufunza watu,
kuwapatia misaada wanayohitaji, kutoa ushauri mbali mbali n.k. maana
kuna baadhi ya wanawake wamejaaliwa kuwa na busara na hikma katika mambo
haya. Vile vile uwezo kwa kusaidia kwa njia yoyote ile, kama ni wa
kifedha, kielimu n.k.
Katika Sehemu Za Kutafuta Elimu
Wanaruhusiwa
wanawake kuhudhuria madarsa yanayotolewa na wanaume ikiwa mashuleni,
Misikitini, vyuoni, au kwenye kumbi, ila lazima kuweko mtengano baina
yao, ama kwa kuweka pazia baina yao au wanawake wakae nyuma ya wanaume.
Hali
kadhalika baadhi ya wanawake wanaweza kutoa mafunzo na wakasikilizwa na
wanaume ila lazima pia shari’ah zake za stara zitekelezwe kama
tulivyotaja juu. Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha)
alikuwa akiwafunza Maswahaba walipomjia kwa masuala mbali mbali ya Dini
yao.
Wa Allaahu A’alam
No comments:
Post a Comment