Tunakaribia
kumaliza mwezi Mtukufu wa Ramadhaan na mambo matatu yafuatayo ya muhimu
yanayotukabili yanapasa kuzingatiwa ili tukamilishe Swawm zetu ipasavyo
na tupate fadhila zake.
1- ZAKAATUL-FITWR
Inaitwa
Zakaatul-Fitwr (Zakaah ya Kufuturu au Kufutari) kutokana na kumalizika
Swawm ya Ramadhaan. Imefaridhiwa mwaka wa pili wa Hijrah katika mwezi wa
Ramadhaan.
Hikma Yake
Ni
kutwaharisha Swawm ya Muislamu kutokana na maneno machafu, ya upuuzi
wakati alipokuwa amefunga kwa kulisha maskini chakula ili nao wapate
chakula kizuri siku ya ‘Iyd. Ndio maana kutolewa kwake kunakuwa kabla ya kuswali Swalaah ya ‘Iydul-Fitwr. Dalili ifuatayo inathibitisha:
عَنْ ابْنِ عَبَّاس ٍقَالَ
فَرَضَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ
الْفِطْرِ طُهْرَةً لِلصَّائِمِ مِنْ اللَّغْوِ وَالرَّفَثِ وَطُعْمَةً
لِلْمَسَاكِينِ مَنْ أَدَّاهَا قَبْلَ الصَّلاةِ فَهِيَ زَكَاةٌ
مَقْبُولَةٌ وَمَنْ أَدَّاهَا بَعْدَ الصَّلاةِ فَهِيَ صَدَقَةٌ مِنْ
الصَّدَقَاتِ . " رواه أبو داود بِإِسْنَادٍ حَسَنٍ .
Kutoka
Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambaye amesema: “Mtume
amefaridhisha Zakaatul-Fitwr kuwa ni twahaara ya mwenye kufunga kutokana
na maneno ya upuuzi na machafu, na kulisha masikini. Atakayeitoa kabla
ya Swalah basi hiyo ni Zakaah iliyotakabaliwa, na atakayeitoa baada ya
Swalah basi hiyo ni miongoni mwa sadaka” [Abu Daawuud kwa isnaad iliyo nzuri].
Na ndio kusudio ya kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
((قَدْ أَفْلَحَ مَن تَزَكَّى)) ((وَذَكَرَ اسْمَ رَبِّهِ فَصَلَّى))
((Hakika amekwishafanikiwa aliyejitakasa)) ((Na akakumbuka jina la Mola wake Mlezi, na akaswali)) [Al-A’laa: 14-15]
‘Umar bin ‘Abdul-Aziyz alikuwa akiamrisha watu kutoa Zakatul-Fitwr na huku akisoma Aayah hizo tukufu.
Wakati Unaowajibika Kutoa
Kuanzia
Magharibi ya siku ya mwisho ya Ramadhaan hadi asubuhi kabla ya Swalah
ya ‘Iydul-Fitwr. Inaweza pia kutolewa siku mbili tatu kabla. Mtoto
atakayezaliwa siku hiyo kabla ya kuzama jua imewajibika kutolewa
Zakaatul-Fitwr.
Anayewajibika Kutoa Zakaatul-Fitwr Na Kitu Gani Cha Kutoa
عَنْ ابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَال فَرَضَ
رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ الْفِطْرِ
صَاعًا مِنْ تَمْرٍ أَوْ صَاعًا مِنْ شَعِيرٍ عَلَى الْعَبْدِ وَالْحُرِّ
وَالذَّكَرِ وَالأُنْثَى وَالصَّغِيرِ وَالْكَبِيرِ مِنْ الْمُسْلِمِينَ
وَأَمَرَ بِهَا أَنْ تُؤَدَّى قَبْلَ خُرُوجِ النَّاسِ إِلَى الصَّلاةِ . صحيح البخاري
Kutoka
kwa Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma): "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam) ameifanya Zakaatul-Fitwr ni fardhi kwa mtumwa na
aliye huru, mwanamume na mwanamke, mdogo na mkubwa miongoni mwa Waislamu
kwa kutoa swaa'* moja ya tende kavu au swaa’ moja ya shayiri, na
akaamrisha kwamba itolewe kabla ya watu kwenda kuswali (Swalaatul-'Iyd)" [Al-Bukhaariy]
- swaa’ moja = kilo mbili na nusu hadi tatu au (mteko) viganja viwili vya mkono vya mtu wa wastani vilivyojaa mara nne.
Kinachotolewa Ni Chakula Kinachotumika Na Watu Katika Nchi:
عن أبي سَعِيدٍ الْخُدْرِيَّ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ
"ُكُنَّا نُعْطِيهَا فِي زَمَانِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ
وَسَلَّمَ صَاعًا مِنْ طَعَامٍ أو صَاعاً من الشعير, أو صاعاً من تَمر, أو
صاعاً من زَبيب، أو صاعاً من أقِط البخاري
Abu
Sa'iydil-Khudriyy (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: "Tulikuwa tukitoa
zama za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) swaa’ moja ya chakula,
au swaa’ ya shayiri au swaa’ ya tende au swaa’ ya zabibu au swaa’ ya
aqit" (mtindi mkavu) (ambacho ndicho kilichokuwa chakula chao zama za
hizo) [Al-Bukhaariy Na Muslim]
Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho kuhusu mas-alah mbali mbali ya Zakaatul-Fitwr:
Fataawa Za Zakaatul-Fitwr
2- ‘IYDUL-FITWR
Inaitwa
‘Iydul-Fitwr (‘Iyd ya kufuturu au kufutari) kutokana na Waislamu
kumaliza funga ya Ramadhaan. Hivyo haifai kufunga Swawm siku ya ‘Iyd,
bali ni sikukuu ya Waislamu ya kusherehekea, kufurahi kwa kila njia
zilizomo katika mipaka ya Dini.
a) Apasayo Kufanya Muislamu Yaliyo Sunnah
Kuoga Kabla Ya Kutoka Kwenda Kuswali
فقد صح في الموطأ وغيره أَنَّ عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عُمَرَ كَانَ يَغْتَسِلُ يَوْمَ الْفِطْرِ قَبْلَ أَنْ يَغْدُوَ إِلَى الْمُصَلَّى
Imethibitika
katika Muwattwa na vitabu vinginevyo kwamba ‘Abdullaah bin ‘Umar
(Radhiya Allaahu ‘anhuma) alikuwa akioga siku ya ‘Iydul-Fitwr kabla ya
kwenda Muswallaa.
Kujipamba Na Kuvaa Nguo Nzuri
وعن جابر رضي الله عنه قال : كان للنبي صلى الله عليه وسلم جبة يلبسها للعيدين ويوم الجمعة . صحيح ابن خزيمة
Kutoka
kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Mtume alikuwa ana
jubbah akilivaa siku za ‘Iyd mbili na siku ya Ijumaa” [Swahiyh Ibn Khuzaymah]
Na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alikuwa akivaa nguo zake nzuri kabisa siku ya ‘Iyd.
Kwa
hiyo inapasa kujipamba kwa nguo nzuri, na manukato mazuri. Ama wanawake
hawapasi kujipamba na kudhihirisha mapambo yao ikiwa ni mavazi au
kujipaka vipodozi na pia hawapaswi kujitia manukato na kutoka nje.
Wanaweza kudhihirisha yote hayo mbele ya Maharimu zao tu.
Kula Tende Kabla Ya Kutoka Kwenda Kuswali
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ قَالَ كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لا يَغْدُو يَوْمَ الْفِطْرِ حَتَّى يَأْكُلَ تَمَرَاتٍ .. وَيَأْكُلُهُنَّ وِتْرًا . البخاري
Kutoka
kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hatoki kwenda
kuswali Swalah ya ‘Iyd ila baada ya kula tende… na akila kwa hesabu ya
witr. [Al-Bukhaariy]
Hii ni kwa sababu haifai kufunga siku hii ya ‘Iyd. Asiyepata tende anaweza kula kitu chochote.
Ama
katika 'Iydul-Adhwhaa ni Sunnah kutokula kabla ya kwenda Msikitini, na
anaposhuka baada ya Swalah ni bora kitu cha kwanza kula ni ile nyama ya
Udhwhiyah (mnyama aliyechinjwa) ikiwa itapatikana.
Kuleta Takbiyrah Kwa Sauti
Sunnah kuu katika ‘Iyd kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((وَلِتُكْمِلُواْ الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُواْ اللّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ((
((na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Allaah kwa kuwa Amekuongoeni ili mpate kushukuru)) [Al-Baqarah: 185]
Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akileta Takbirah mpaka anamaliza Swalah. [Silsilat Al-Ahadiyth As-Swahiyhah - Shaykh Al-Albaaniy]
Matamshi Ya Takbiyrah
الله أكبر الله أكبر لا إله إلا الله والله أكبر الله أكبر ولله الحمد
Allaahu Akbar Allaahu Akbar, Laa Ilaaha Illa Allaah, WAllaahu Akbar Allaahu Akbar wa Lillaahil Hamdu
Wakati wa Takbiyrah
Unaanza usiku wa ‘Iyd mpaka anapoingia Imaam kuswalisha Swalah ya ‘Iyd
Kupongezana
Ni
vizuri kupongezana siku ya ‘Iyd baina ya Waislamu, kuzidisha mapenzi
baina yao. Na ilivyo Sunnah ni kusema kama walivyokuwa wakiambiana
Maswahaba wanapokutana siku ya ‘Iyd ni kusema:
'Tuqubbila Minna wa Minka’ au ‘Taqabbala Allaahu Minnaa wa Minkum’.
Kuelekea Katika Muswallaa Kwa kutembea Na Kurudi Kwa Njia Nyingine
عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا كَانَ يَوْمُ عِيدٍ خَالَفَ الطَّرِيقَ . رواه البخاري
Kutoka
kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambaye amesema:
“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akibadilisha njia siku
ya ‘Iyd” [al-Bukhaariy]
Hikma
yake ni kwamba njia hiyo itashuhudia siku ya Qiyaamah na ardhi
itazungumza yote ya kheri na shari anayotembelea mja juu yake. Pia
kudhihirsiha Uislamu katika njia mbili, pia kukutana na watu tofauti na
kuwasaidia kwa njia yoyote.
Kuswali Swalah ya ‘Iyd Katika Muswallaa
Ni Sunnah bali, ni waajib kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliamrisha watu wote watoke kwenda kuswali:
عَنْ أُمِّ عَطِيَّةَ رضي الله عنها قَالَتْ "أَمَرَنَا تَعْنِي النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ نُخْرِجَ فِي الْعِيدَيْنِ الْعَوَاتِقَ وَذَوَاتِ الْخُدُورِ وَأَمَرَ الْحُيَّضَ أَنْ يَعْتَزِلْنَ مُصَلَّى الْمُسْلِمِينَ" مسلم
Kutoka
kwa Ummu ‘Atwiyyah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) kwamba: “Ametuamrisha Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tutoke katika ‘Iyd mbili
vijana na vikongwe na kaamrisha wanawake wenye hedhi wajitenge katika
Muswallaa” [Muslim]
b) Yaliyo Bid’ah Katika ‘Iyd
Kuleta Takbiyrah Kwa Pamoja Katika Misikiti Na Muswallaa
Inavyopasa ni kila mtu kuleta Takbiyrah pekee.
Kutembelea Makaburi
Imekuwa
ni ada ya baadhi ya watu kutembelea makuburi siku za ‘Iyd. Jambo hili
halikufanywa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wala Maswahaba
zake. Mtu anaweza uzuru makaburi siku yoyote na si kutenga siku ya ‘Iyd
kwa jambo hilo na hadi kugeuka kuwa ni katika Sunnah za ‘Iyd hivi leo.
Maamkizi Ya Kuiga Makafiri
Kupelekeana
kadi na zawadi kama wafanyavyo makafiri, haipasi kuwaiga kwani ni jambo
tulilokatazwa katika dini na tuwe na fakhari na mila na desturí zetu.
c) Yaliyo Maasi
Kunyoa Ndevu
Kunyoa
ndevu hasa kwa makusudi ya kukusudia ‘Iyd kwa kudhani mtu anapendeza
akifanya hivyo ilihali anavunja sheria na kupingana na Sunnah za Mtume
wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Wanawake Kutokutimiza Hijaab zao za kishari'ah na kudhihirisha mapambo yao mbele ya wasio Maharimu wao.
Sherehe Za Maasi
Kuchanganyika
wanawake na wanaume (party) na kuwekwa muziki, vyakula na vinywaji vya
haraam na kupeana mikono wanawake na wanaume.
((لأَنْ يُطْعَنَ فِي رَأْسِ أَحَدِكُمْ بِمِخْيَطٍ مِنْ حَدِيدٍ خَيْرٌ لَهُ مِنْ أَنْ يَمَسَّ امْرَأَةً لا تَحِلُّ لَهُ))
Mtume (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Ni bora kwa mwanaume kupigwa sindano katika kichwa chake kuliko kuushika mkono wa mwanamke ambaye si halali yake.” [Silsilat Al-Ahadiyth As-Swahiyhah - Shaykh Al-Albaaniy]
Wanawake wanaruhusiwa kuimba Nashiyd siku za ‘Iyd wakiwa peke yao au mbele za Maharimu wao.
Kufanya Israaf ya chakula na mali badala ya kuwasaidia masikini na mafakiri
3- SWAWM YA SITATUSH SHAWWAAL
Swawm
hii inafuatia moja kwa moja baada ya mwezi wa Ramadhaan na siku ya 'Iyd
ul Fitr. Ni Sunnah iliyo na fadhila kuu kwani thawabu zake ni sawa na
thawabu za mtu kufunga mwake mzima kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam)
(( من صام رمضان ثم أتبعه ستًّا من شوال كان كصيام الدهر)) أرجه مسلم في صحيحه،
((Atakayefunga Ramadhaan kisha akafuatiliza na siku sita za mwezi wa Shawwaal itakuwa kama ni funga ya mwaka)) [Muslim]
Hesabu ya kuwa mwaka mzima ni kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((مَن
جَاء بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا وَمَن جَاء بِالسَّيِّئَةِ
فَلاَ يُجْزَى إِلاَّ مِثْلَهَا وَهُمْ لاَ يُظْلَمُون))
((Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. na afanyae ubaya hatalipwa ila sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa)) [Al-An'aam:160]
Na kauli ya Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((إن
الله كتب الحسنات والسيئات , ثم بين ذلك , فمن هم بحسنة فلم يعملها كتبها
الله له عنده حسنة كاملة فإن هو هم بها فعملها كتبها الله له عنده عشر
حسنات , إلى سبعمائة ضعف , إلى أضعاف كثيرة , ومن هم بسيئة فلم يعملها ,
كتبها الله عنده حسنة كاملة , فإن هو هم بها فعملها كتبها الله له سيئة
واحدة )) متفق عليه ،
((Allaah
Ameandika mema na mabaya. Kisha Akayabainisha. Basi atakayetia nia
kutenda jema kisha asilifanye, ataandikiwa jema moja kamili.
Atakapofanya hima na akalitenda, ataandikiwa mema kumi hadi kuzidi mia
saba na ziada nyingi. Na atakayetia nia kufanya kitendo kibaya kisha
asikifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapokifanya ataandikiwa
dhambi moja)) [Al-Bukhaariy ya Muslim]
Maulamaa
wanachambua sababu ya kulipwa mja ujira wa mwaka mzima kwa atakayefunga
Ramadhaan na siku sita hizo za Shawwaal, kwa kusema: Jambo zuri hulipwa
ujira mara kumi, kwa hiyo mtu akifunga siku 30 za Ramadhaan atapata
ujira mara kumi; nazo zitakuwa 300, ukijumlisha na siku sita za Shawwaal
ambazo zikilipwa mara kumi, huwa 60. Kwa hivyo 300 + 60 = 360, mtu
atapata hesabu ya mwaka mzima.
Kwa mantiki hii, tunaona kuna umuhimu na ubora mkubwa wa kuifunga Swawm hii ndugu zangu.
Tunawaombea
Waislamu wote wajaaliwe kumaliza mwezi Mtukufu wa Ramadhaan kwa kheri
na mafanikio, watakabaliwe Swawm zao, na madhambi kughufuriwa, waweze
kutoa Zakaatul-Fitwr za kutakasa Swawm, Wawe na ‘Iyd ya furaha na uwezo
wa kufunga Sitatush Shawwaal.
Taqabballa Allaahu Minna wa Minkum
No comments:
Post a Comment