Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Thursday, August 30, 2012

MCT yakipongeza Chuo cha habari Zanzibar

Na Husna Mohammed
BARAZA la Habari Tanzania (MCT), limekipongeza Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar (ZJMMC), kutokana na kiwango chake cha elimu inachokitoa chuoni hapo.

Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Kajubi Mukajanga, aliyasema hayo jana alipofungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kitaaluma walimu wa Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar, yaliyofanyika ofisi za Baraza la Habari Zanzibar tawi la Zanzibar hapo Mlandege mjini hapa.

Alisema chuo cha ZJMMC, kinatoa taaluma ya ushindani wa soko la ushindani katika tasnia ya habari ikilinganishwa na vyuo vya habari vinavyochipukia hasa upande wa Tanzania bara.

"Kwa kuwa tasnia hii unaweza kufanya kazi popote ni dhahiri waandishi wanaopata taaluma hiyo wanaweza kuingia katika ushindani mkubwa na si kwa Tanzania bara, nchi jirani lakini pia wanaweza kufanya kazi nchi yoyote na mashirika makubwa ya habari", alisema.

Kajubi, alisema pamoja na mambo mengine, walimu hao wanaopatiwa mafunzo ya siku nne kwa kiasi kikubwa yatawawezesha kutoa elimu ya ubora zaidi inayohitajika NACTE ili kuwawezesha wanafunzi wanaomaliza masomo yao kutambulikana zaidi.

Aidha alisema mafunzo hayo yatawawezesha kwenda sambamba na mitaala inayotakiwa na NACTE, jambo ambalo litawapa upeo mkubwa wa ufundishaji walimu.

"Lengo letu ni kutaka kuona tunawaandaa waandishi kuweza kufanya kazi zao vizuri wanapomaliza masomo yao", alisema.

Nae Mkuu wa Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar, Saleh Yussuf Mnemo, alisema kwa kiasi kikubwa mafunzo hayo yataweza kuwajengea uwezo walimu wanaofundisha chuoni hapo, sambamba na kuelekea katika usajili wa NACTE kwa chuo hicho.

"Ni wazi kuwa sasa tunaelekea katika mchakato wa kupata usajili wa NACTE hasa ikizingatiwa kuwa mitaala hii inaendana hasa na kile wanachokitaka", alisema.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Baraza la Habari Tanzania na kusimamiwa na kuratibiwa na Baraza la Taifa na viwango vya Elimu Tanzania (NACTE).

No comments:

Post a Comment