Balozi mpya wa Tanzania katika Umoja
wa Mataifa Balozi Tavaku Manongi amesema Uongozi wake utajitahidi
kuangalia maeneo yanayoigusa Zanzibar moja kwa moja katika jitihada za
kunyanyua Uchumi na kustawisha Maendeleo ya Jamii.
Balozi Tavaku akiambatana na Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania
Umoja wa Mataifa Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi alieleza hayo wakati
akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
hapo Nyumbani kwake Mtaa wa Namanga Mjini Dar es salaam.
Alisema yapo masuala ambayo Zanzibar ina fursa ya kuyafanya na
kuyafuatilia bila ya kuathiri yale maeneo ambayo hushughulikiwa moja kwa
moja kwa mujibu wa taratibu za Kimuungano.
Balozi Tavaku alisisitiza kwamba utendaji wake mara zote utazingatia
zaidi Umoja na Ushirikiano kati yake, Watendaji atakaowaoongoza pamoja
na Taasisi, Jumuiya na Nchi washirika.
“ Nitahakikisha muda wangu pia nautumia katika kuangalia maeneo
yanayoigusa Zanzibar kuyafanyia kazi katika muda wangu wote” Alisisitiza
Balozi Tavaku.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza nguvu na msimamo wa Tanzania katika ushiriki wake kwenye Nyanja za Kimataifa.
Balozi huyo wa Tanzania Umoja wa Mataifa alimuomba Balozi Seif
kuendelea kuwapa msaada watumishi hao wapya kutokana na uzoefu alionao
wa muda mrefu kwenye masuala ya Kimataifa.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alimpongeza Balozi Tavaku kwa kuteuiwa kushika wadhifa huo na kumtaka
awe makini katika kupambana na changa moto zitakazomkabili katika
utumishi wake huo mpya.
Balozi Seif alimueleza Balozi Tavaku kwamba miongoni mwa changamoto
hizo ni pamoja mchakato wa Tanzania kuelekea katika katiba mpya ambayo
tayari Wananchi wameanza kutoa maoni yao.
Alisema yapo matatizo katika katiba ya sasa na kitachozingatiwa zaidi
katika fursa ya Wananchi ya utoaji wa maoni ni kuhakikisha kasoro na
upungufu uliopo unaondoshwa kwa kujenga katiba madhubuti itakayokidhi
mahitaji ya Jamii yote ya Watanzania. “ Naamini Katiba mpya
ijayo kwa kuwa itahusisha Wananchi wote itaondowa kero na mapungufu
yaliyokuwa yakileta migongano miongoni mwa Wananchi wa pande zote”.
Alifafanua Balozi Seif.
No comments:
Post a Comment