Mafundi wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO)
tawi la Pemba wakiwa katika harakati za kuwafungia transfoma wananchi wa kijiji
cha Kichaka Shehia ya Mtangani Jimbo laKiwani Wilaya ya Mkoani Pemba , ambapo
transfoma hiyo pamoja na nguzo 25 zimesgharimu zaidi ya shilingi 39 milion
ambapo ni mchango wa wananchi zaidi ya shilingi 18 milion (picha na Haji Nassor, Pemba)
Na Haji Nassor, Pemba
ZAIDI
ya shilingi 39 milion, zimetumiwa na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Tawi la
Pemba, kwa ajili ya ununuzi wa trasfoma na nguzo 25, ambapo tayari jana trasfoma
hiyo, imeshafungwa katika kijiji cha Kichaka Jimbo la Kiwani Wilaya ya Mkoani
Pemba.
Kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi 18
milion, ni mchango wa wananchi na shilingi 20 milion na laki nane, zimetolewa
na ZECO ili kukamilisha upatikanaji wa huduma ya umeme kwa wananchi zaidi ya
1000 wa eneo hilo.
Akizungumza mara baada ya kazi ya ufungaji
wa transfoma hiyo, huko Kichaka Msaidizi Afisa Uhusiano wa ZECO Tawi la Pemba
Faki Othuman Sharif, alisema kuwa shirika kwa sasa limekuwa na utamaduni wa kusaidiana
gharama na wananchi, iwapo wanahitaji kuwekewa transfoma.
Faki alieleza kuwa, hilo linatokana na shirika kujipanga upya kwa
sasa, ili kuwaletea huduma bora wananchi kwenye sekta ya umeme, katika miji na
vijiji mbali mbali ili uweze kuwasaidia katika kuinua kipato chao.
Afisa huyo aliwaambia wanavijiji vya
Kichaka juu, Kinyasini, Utaani, pamona na Nga’ambu kuhakikisha wanajiungia
umeme kwa lengo la kujinasua na umasikini uliokithiri miongoni mwa jamii za
kizanzibari.
‘’Leo tumekamilisha ile kiu yenu ya miaka
zaidi ya 20 mliokuwa nayo ya kutaka huduma ya umeme, na leo tayari tumeshafunga
transfoma mpya kwa kushirikiana na nyinyi, hivyo huduma hii iwe kwa ajili ya
maendeleo yenu’’,alifafanua .
Katika hatua nyengine Msaidizi huyo Afisa
Uhusiano wa ZECO Tawi la Pemba amewahakikisha
wananchi wa vijiji hivyo kuwa, kabla ya wiki tatu shirika la umeme litasambaaza
waya mdogo, ili kutoa fursa kwa wananchi kuvuta majumbani mwao.
Mapema wakizungumza na mwandishi wa habari
hizi, mara baada ya kazi hiyo wananchi wa kijiji hicho na vyengine, walisema
kuwa walisubiri huduma ya umeme tokea mwaka 1993 mara baada ya kuwekewa laini
kubwa ya umeme.
Mohamed Omar Hamad (55) alisema kuwa hata
hivyo ameliharakisha shirika la Umeme juu ya kuweka waya mdogo kijijini hapo,
ili kila mwananchi mwenye uwezo aweze kuvuta badala ya kuwepo kwa transfoma kama pambo.
‘’Mje tena mtufungie waya mdogo, ili wenye
uwezo wavute umeme na sisi tunywe juisi baridi kama
mnavykunywa nyinyi huko mijini mtokeako’’,alifafanua na kusema kuwa iwapo
watafungiwa waya huyo watavuta majumbani mwao.
Nae kijana Chande Khamis Rashid (28)
aliwataka vijana wenzake kuanza kujipanga ili huduma hiyo ya umeme iwawezeshe
kujiajiri ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vidogo vidogo, saluni pamoja na
maduka ya vinywaji baridi.
‘’Vijana wenzangu umeme sasa tayari maana
tumeshawekewa trasfoma mpya sasa kilichobakia ni sisi tu ndio wakujipanga ili
kuona huduma hii inatunufaisha kwa kuweza kujiajiri ‘’,alifafanua kijana huyo.
Kijiji cha Kichaka na vijiji jirani kwenye
Jimbo la Kiwani Wilaya ya Mkoani, vilipitiwa na laini kubwa ya umeme tokea
mwaka 1994 uliosambaaza na kampuni na NEREMKO bila ya kuwepo kwa transfoma,
hadi mwaka huu walipoamua kuchangana fedha na kufungia mashine hiyo.
No comments:
Post a Comment