Wapingaji wa sensa kwa upande wa Zanzibar ni miongoni mwa vinara waliounga mkono wazo la Maalim Seif na Amani karume kwamba tuwaunganishe watu, tusiwagawe tena watu, tuondoe chuki, visasi na mapambano miongoni mwetu. Mimi mawazo yao nayaheshimu lakini sitowacha kuangalia pande zote mbili za shilingi na kulichambua kwa umakini suala hili na kamwe sitafuata mkumbo.
Tuliwahi kukusanyika siku moja katika viwanja vya Maisara wazanzibari na na viongozi wa serikali yatu kumuomba Mungu atuzidishie nguvu umoja wetu na ailinde serikali yetu ya umoja wa kitaifa. Bila shaka kufanya lolote kwa lengo la kuikwaza serikali hii isifanye shughulki zake, hususan za kuwatumuikia watu ni kupingana na kile kilichofanyika siku hiyo. Na kwa lugha hii mwenye kupingana na anachokiamini kwa nini asiitwe MNAFIQ?
Wazanzibari hawakuwa na agenda ya kususia sensa hapo kabla. Baada ya kupigiwa debe agenda hiyo na waislamu kutoka Tanganyika, na UAMSHO nao wakaibeba agenda hiyo ili angalau kupata agenda mpya kwa kuwa ile ya muungano, wenyewe CUF ndio wanaoonekana kwenda nayo kwa taratibu zinazoeleweka na kwa muelekeo unaotoa matumaini makubwa.
Sababu za kususiwa sensa na waislamu wa Tanganyika ni kupingana na mfumo KRISTO kwa kuwa wanahisi kwa kutowekwa wazi takwimu halisi za wakristo na waislamu, mfumo kristo utaendelea kuwakandamiza waislamu kwa visingizio wakristo ni wengi nchini kama zilivyowahi kudai baadhi ya takwimu za kubuni.
Kwanza hatuna budi tufahamu kwamba waislamu wa Tanganyika hawana nia ya kweli ya kuwa na umoja na waislamu wenzao wa Zanzibar. Huko nyuma haikuwa hivyo na hata sasa haiku hivyo. Waislamu wa Tanganyika huonekana kutafuta uungwaji mkono kutoka Zanzibar pale wao tu wanapobanwa na sio pale wazanzibari nao wanapobanwa. Na kama hiyo haitoshi wao pia waislamu wa Tanganyika ndio washiriki wakuu wa maonevu ya wazanzibari.
Ni akina nani waliokuja kuwauwa wazanzibari wasio na hatia mwaka 1964? Si Peter wala Kurwa ni waislamu wenzetu ambao wakiingia misikini na kusali pamoja nasi. Sitaki nizungumze sana kuhusu hili kasome “kwaheri ukoloni, kwaheri uhuru, Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia”.
Wazanzibari walipita katika misukosuko mingi tokea miaka ya 1980, 1990, 2000, hadi mwaka 2009 walipoingia katika maridhiano. Katika kipindi chote hicho wazanzibari ambao ni waislamu waliteswa, kupigwa, kudhalilishwa, kunajisiwa, kuuliwa, kutiwa ulemavu, kuachwa mayatima na vizuka, je taasisin hizi za waislamu wa Tanganyiak wanaotaka waungwe mkono kugomewa sensa walikuwa wapi? Mbona hawakuwahi kutoa matamko makali wala kususia chochote kuonyesha kuwaunga mkono waislamu wenzao wa Zanzibar wanaodhalilishwa na majeshi ya Mkapa wakati huo? Jibu ni kwa kuwa hapakuwa na maslahi yao. Lakini kupinga sensa ya mwaka 2012 kuna haja muhimu kutetea maslahi yao.
Serikali haiwezi kufanya shughuli zake bila ya takwimu hizi ambazo zinachukuliwa kila baada ya miaka 10 tu. Pamoja na kwamba suala la takwimu ni la muungano lakini matumizi ya takwimu hizo yanaihusu serikali yetu ya Zanzibar. Hivyo basi wazanzibari kususia sense si kuikwaza serikali ya Tangantika bali ni kuikwaza serikali yao wenyewe, inayosimamia mahitaji yao kwa gharama zake bila hata ya senti 5 kutoka Tanganyika.
Sensa ndio ilyotumika kupunguza majimbo ya CUF mwaka 2002 na kuongeza majimbo ya CCM. Kwa kuwa kasi ya mabadiliko imekuwa kubwa katika muungano CCM wanayo hamu kubwa watu kususia sensa ili wapate kupunguza nguvu za CUF Zanzibar ili iweze kuunusuru mfumo wa muungano wa serikali 2. Wako wanaojidanganya kuwa hoja hii ina maslahi kwa CUF. Wakidhani hivyo sawa, ila ambAcho CUF inakifanya ni kwa maslahi ya Zanzibar. Hata kama ni kunusuru majimbo ya CUF yasije yakamegwa kwa kisingizio cha sensa ndio pia kunusuru na bunge la katiba lisije likawa na wingi wa wajumbe wa CCM na kufanikiwa kurejesha mfumo wa serikali 2.
Wanaokebehi CUF kwa kisingizio cha kukebehi siasa na kurukia eti dini ndio njia ya ukombozi katika mifumo hii tulio nayo dunianai ni kujidanganya mchana. Bado utaratibu wa kuweka dola, kushikilia dola na nguvu zake na hata utakaoiweka dola huru ya Zanzibar tunayoitamani hapo baadae ni mfumo huu huu wa kisiasa. Hakuna utaratibu mwengine wowote. Kwa mwana CUF kuikejeli CUF na kuona NGO ya kidini ndio italeta dola huru ya Zanzibar si sahihi. Mimi sibezi taasisi za dini. Taasisi yeyote iliyo makini inaweza kutusukuma mbele zaidi katika njia yetu lakini pia taasisi yenye kupoteza muelekeo inaweza kuturejesha nyuma zaidi.
Mimi kwa ufahamu wangu agenda za kususia tume ya katiba zilizokuwepo kabla, kususia sensa na nyengine ambazo zitakuja mbeleni zenye lengo la kutukwaza ni mipango na mikakati inayosukwa kiufundi na idara ya usalama wa taifa na kutumbukizwa katika kila sekta ya maisha hapa Zanzibar ambamo CUF wamo li kupambana na CUF bila ndugu zangu wafuasi wa UAMSHO kufahamu kuwa wanabeba agenda pachikizi. Usalama wa taifa wasiofahamika na raia katika CCM wamo, katika CUF wamejiingiza, katika jumuiya za kidini wamo na kwengineko pia wamo. Hawajulikani, wakifanya hili na lile kwa ufundi mkubwa huku wafuasi wetu wa CUF wakiwaona ni wenzao na hivyo kukaa nao na kupanga nao mambo ya kuwahujumu wenyewe.
Mimi binafsi nawambia watu waliobeba agenda za kisiasa kupita taasisi za dini angalau wangeshauriana na wanasiasa. Siasa wenyewe ni wanasiasa ndio wanaoona mbali katika siasa. Hata Maalim Seif aliziahidi taasisi zote kuwa milango yake yote iko wazi kwa mtu yeyote mwenye agenda yake kufika kwake kwa mashauriano ili kujenga umoja. Lakini bahati mbaya haya yote yanatendwa bila ya angalau kumfika na kumshauri Maalim. Kila mtu anajiona bingwa wa siasa. Siasa za CUF ni kuifikisha Zanzibar kuwa yenye mamlaka kamili, bila shaka ni taasisi hii ndio inayovifahamu mbinu, mikakati, njiavichochoro vya kuopitia kufikia huko. Wanaorukia ngoma si yao na si kwa lengo la kusaidia bali kutafuta njia yao wenyewe inayopingana na ile ya CUF tuanawatanabahisha bado ingali mapema. CCM na idara zake za kiusalama wapo na wanafanya kazi zao, si hasha kuwa wao ndio wanawapeleka watu upande ambao si sawa sawa.
Sisi wengine bado tunawaomba sana wenzetu wafikirie mara nyingi maamuzi yao kabla ya kutangamiza kabisa badala ya kutuokoa. “Wazanzibari kwa kuungana kwetu tutaweza kulifuikia kila jambo ambalo hapo kabla hatukuweza kulifikia kwa kugawika kwetu” Maalim Seif.
Haya ni mawazo yangu binafsi si ya chama changu.
No comments:
Post a Comment