WAISLAMU mkoani Arusha wamepinga uteuzi wa Kadhi Mkuu na Makadhi wengine
wa mikoa 14 uliofanywa na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban Simba
kwa madai kuwa uteuzi huo ni wake binafsi na unalenga kuwavuruga
waislamu nchini.
Hivi karibuni Mufti Simba alimtangaza Sheikh Abdallah Mnyasi kuwa Kadhi
Mkuu na kuwateua Manaibu wake wawili, Sheikh Abubakar Zubeir na Sheikh
Muhidini Mkoyogole.
Akipinga uteuzi huo, Imamu wa msikiti mkuu mkoani Arusha, Mohammed
Hambal alisema kwamba uteuzi huo una makosa makubwa kwa kuwa Kadhi Mkuu
huteuliwa na jopo la wasomi na sio mtu mmoja.
Alihoji kwamba taifa liko kwenye hatua ya uundwaji wa mchakato wa katiba
mpya kwa sasa na kilio cha waislamu nchini ni uundwaji wa mahakama ya
kadhi iingizwe kwenye katiba hiyo na kushangaa uteuzi huo kufanyika
wakati huu.
“Wakati tume ya kukusanya maoni ikipita tunashangaa Mufti anamteua Kadhi
Mkuu kitu ambacho ni kinyume na taratibu na mwogozo wa nchi,” alisema
Hambal.
Hata hivyo, Hambal alihoji uteuzi huo umezingatia katiba ipi kwa kuwa
katiba ya nchi pamoja na katiba ya BAKWATA haina kipengere wala
maelekezo ya mfumo wa uundwaji wa mahakama ya kadhi.
Naye, Mwenyekti wa msikiti huo, Abdulazizi Mkindi alisema kwamba
amepokea uteuzi wa Mufti kwa masikitiko makubwa kwa kuwa uteuzi huo
umefanywa na kikundi cha watu wachache kwa lengo la kuwaongoza wailsamu
nchini na taasisi zao.
Alisema kwamba masuala ya uteuzi wa Kadhi Mkuu yanapaswa kusimamiwa na
watalaamu na wasomi waliobobea katika sheria na sharia za kiislamu na si
vinginevyo.
“Kilio cha mahakama ya kadhi ni kilio cha wailsamu wote na si kilio cha
BAKWATA pekee,masuala ya Kadhi yanatakiwa yasimamiwe na wataalamu
waliosomea sheria na sharia za kiislamu na si watu wa ovyo,” alisema
Mkindi.
Mustapha Kihago na Salim Mvungi maarufu kama Shefu kwa upande wao
walipinga uteuzi huo na kusema kwamba wameshutushwa na wanahisi kwamba
hizo ni njama za serikali kuitumia taasisi ya BAKWATA kuwavuruga
wasilamu.
Walimnyooshea vidole Mufti Simba kuwa amelifanya suala la uteuzi wa
Kadhi Mkuu kama ajenda yake binafsi wakati jambo hilo ni la wailsamu
wote nchini.
No comments:
Post a Comment