Kwa kuoa huchukui tu mke, Bali
unachukua ulimwengu wako mzima. Kuanzia hapo mpaka maisha yako yote mke
wako atakuwa mwenzio, mwandani wako, na rafiki yako mpenzi.
Atashiriki katika nyakati zako nzuri, siku
zako, na miaka yako. Atakuwa pamoja nawe katika furaha na shida, katika
mafanikio na tabu, katika ndoto zako na katika wakati wa hofu. Ukiumwa, atakupa huduma
bora kabisa. Wakati unapohitaji msaada atafanya vyovyote awezavyo kwa
ajili yako. Wakati una siri, ataitunza siri yako, wakati unahitaji
ushauri, atakupa ushauri mzuri kabisa.
Atakuwa
na wewe utakapoamka asubuhi kitu cha kwanza ambacho macho yako yataona
ni macho yake. Wakati wa mchana, atakuwa na wewe, kama kuna wakati
mchache hatokuwa na wewe kwa kimwili, atakuwa anakufikiria wewe,
anakuombea dua kwa moyo wake wote, akili yake yote, na roho yake nyote.
Ukienda kulala usiku, kitu cha mwisho macho yako kuona itakuwa ni yeye, na ukilala bado utakuwa unamuona katika ndoto zako. Kwa kifupi atakuwa ni ulimwengu wako mzima na wewe utakuwa ulimwengu wake mzima.
Kielezo bora kabisa ambacho mimi binafsi nishawahi kusoma kinafafanua ukaribu wa wanandoa juu ya wao kwa wao na kielezo hicho kipo katika aya ya Qur-aan ambayo inasema:
((Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao)) [Al-Baqarah 2:187].
Na Kweli, wanandoa ni kama
vazi juu ya wao kwa wao kwa sababu wanapeana ulinzi, liwazo, kinga
(stara), msaada (tegemeo), na mapambo ambayo vazi linampa mtu. Hebu
jaribu kufikiri msafara wakati wa siku za baridi kwenda sehemu kama vile Alaska
bila ya kuwa na nguo! Wanandoa wetu wanatupa kiwango kile kile cha
faraja (liwazo), ulinzi, na msaada katika msafara wa maisha yetu katika dunia hii kama vile nguo itakavyofanya katika msafara wa Alaska.
Mahusiano baina
ya wanandoa ni ya kustaajabisha kabisa katika mahusiano yote ya
kibinaadamu: Idadi ya mapenzi na mahaba, undani na ukaribu, huruma na
imani, amani na utulivu ambao unajaza nyoyo za wanandoa ni jambo
lisiloelezeka kwa wepesi. Ufafanuzi pekee wa mantiki ambao unaweza
kuelezeka juu ya haya mastaajabu makubwa katika hisia zote za kibinaadamu ni kwamba: Ni kitendo cha Allah Subhanahu wa Ta'ala, ((Na Allaah Amekuumbieni wake [na wenza katika jinsi yenu])) [An-Nahl 16:72]
Mola wetu tu Allaah Subhanahu wa Ta'ala katika katika Utawala Wake usio na upeo wa
huruma Yake isiyo na mipaka na Hekima Yake adhimu Anaweza kujenga na
kuzididimiza katika akili hizi hisia za kustaajabisha na za kubarikiwa
katika nyoyo za wanandoa. Kwa kweli Allah Subhanahu wa Ta'aala
Anawakumbusha wale ambao wanatafuta ishara Zake katika ulimwengu huu
kwamba hisia hizi katika moyo wa wanandoa ni katika ishara Zake ambazo
zinatakiwa zimuongoze mwanaadamu katika kuwepo Kwake kama Alivyosema
katika Qur-aan, (Na
katika Ishara Zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi
zenu ili mpate utulivu kwao. Naye Amejaalia mapenzi na huruma baina
yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo ishara kwa watu
wanaofikiri." [Ar-Ruum 30:21]
Lakini Allaah Subhanahu Wa Ta’aala Anajua kwamba moyo wa binaadamu
sio kitu ambacho kiko tuli, wakati mwengine huwa dhaifu na wakati
mwengine huwa na nguvu. Hisia zinaweza kubadilika na hubadilika pindi
wakati unavyosogea. Mapenzi yanaweza kufifia na kupayuka mbalini.
Mshikamano wa ndoa unaweza kuwa dhaifu kama
haujahudumiwa vizuri. Furaha katika ndoa haiwezi kudharauliwa; furaha
ya kuendelea inahitaji utowaji wa daima kutoka pande zote. Ili mti wa
mapenzi ya ndoa ubaki hai na kuendelea kuishi, udongo lazima udumishwe, uhifadhiwe, umwagiwe maji na ulelewe.
Kumbuka kwamba Mtume wetu Muhammad
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipata nafasi ya kwenda
kwenye majangwa na kushindana mbio na mke wake Bibi 'Aaishah. Bibi
'Aaishah alimshinda Mtume lakini baadae aliponenepa, Mtume alimshinda
Bibi 'Aaishah. Kumbuka kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) alimchukua mkewe kwenda kuwatazama vijana wa Ki-Ethiopia
wakicheza michezo ya utamaduni wao. Maonyesho
ya hisia yanahitajika kuweza kuufanya mshikamano wa ndoa usifanye kutu
na kuoza. Kumbuka kwamba utapata thawabu kutoka kwa Allah (Subhanahu wa
Ta'aala) kwa hisia zozote unazomuonyesha mkeo kama Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyosema: ((Mmoja wenu atapata thawabu kwa chochote ambacho atafanya ili kutafuta radhi za Allaah hata kwa tonge analomlisha mkewe))
Kamwe usidharau umuhimu wa vitu vidogo vidogo kama vile kuweka chakula kwenye mdomo wa mkeo, kumfungulia mlango wa gari, na hali kadhalika. Kumbuka kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anasogeza goti lake kwa mkewe amkanyage kuweza kumpanda ngamia.
Jaribu kutafuta wakati ili nyote wawili muweze kuswali pamoja. Kuuimarisha
uhusiano kati yenu na Allaah (Subhanahu wa Ta'aala) ni hakikisho kubwa
kuwa uhusiano wenu wa kindoa utabaki madhubuti. Kuwa na amani kati yenu na Allah (Subhanahu wa Ta'ala) daima kutapelekea ndani mwenu kuwa na amani zaidi.
Kumbuka kwamba Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwapa habari nzuri
(aliwabashiria) wanandoa wanaoamka usiku kuswali pamoja. Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anamsisitiza mwanandoa anayeamka
mwanzo amuamshe mwenzake, japo kummwagia maji katika uso wake.
Daima
jaribu uwezavyo kuwa mtu mzuri kwa mkeo kwa njia ya maneno na vitendo.
Ongea nae, mchekee, tafuta ushauri wake, muulize juu ya mawazo yake,
tumia wakati maalum na yeye na daima kumbuka kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Wabora katika nyinyi ni wale ambao ni wabora kwa wake zao))
Mwishowe,
ni kawaida kwa wanandoa kuahidi kuwapenda na kuwaheshimu wanandoa
wenziwe mpaka mauti yawatenganishe. Naamini kwamba ahadi hii ni nzuri au
ni bora kabisa, lakini haitoshi! Haitoshi kumpenda mkeo tu. Lazima
upende anachokipenda
pia. amilia yake, anaowapenda yeye uwapende pia. Usiwe kama mwenzangu
mmoja ambaye hakufurahiwa kuja kwa wazazi wa mke wake kukaa kwa wiki
chache. Alimwambia wazi mkewe “Mimi siwapendi wazazi wako”. Bila ya
kusita mkewe alimtazama machoni kwa hasira na kusema, “Na wako pia siwapendi”.
Mapenzi yasiishe na pia tunaamini kuna maisha baada ya mauti ambapo wale ambao walifanya wema katika dunia hii wataungana na wanandoa wenzio ((Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa humo)) [Az-Zukhruf 43:70] Pia wataungana na watoto wao.
Na
mfano bora katika mintarafu hii itakuwa ni Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye mapenzi yake kwa Bibi Khadiyjah,
mkewe aliyeishi naye kwa miaka 25 yalisogea mpaka kwa wale aliowapenda
Khadiyjah; mapenzi yake haya yaliendelea hata baada ya kufa Bibi
Khadiyjah. Ilikuwa miaka mingi baada ya kifo cha Bibi Khadiyjah na Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakumsahau
na kila panapochinjwa mbuzi katika nyumba yake basi hutuma kifurushi
kwa familia ya Bibi Khadiyjah na marafiki zake na kila akihisi kuwa mgeni anayegonga mlango ni Dada ya Khadiyjah aitwaye Hala, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba huku akisema, "Ee Allaah Jaalia awe ni Hala."
No comments:
Post a Comment