TCRA yahitaji 6bn/ kuweka anuani Dar es Salaam
Na Kunze Mswanyama,DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inahitaji zaidi ya shilingi
bilioni 6 ili kuweka anuwani za makazi kwa mkoa wa Dar es salaam pekee
ikiwa ni gharama za ununuzi wa vitendea kazi, usafiri na mahitaji
mengine ya lazima.
Hata hivyo,TCRA imeomba wananchi kuchangia zoezi hilo kwani kutokana na
kupanda kwa gharama za bidhaa, mahitaji yanazidi kuongezeka na kwamba
imepangwa kufanyika harambee maalum.
Katibu Mkuu wa wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Dk.Florens
Turuka alipokuwa akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya wandishi wa habari
waliojumuika kwa pamoja na wabunge wote wa Dar es salaam.
Alisema, kwa kutambua umuhimu wa mradi huo viongozi wa jiji
walikubaliana kwa pamoja kuandaa chakula cha hisani cha kuweza
kuchangisha na kupata fedha za kuchangia utekelezaji kwa ufanisi na kwa
muda uliopangwa.
“Serikali kwa kupitia TCRA imefungua akaunti maalumu kwa ajili ya
uchangiaji mradi huo ili kutekeleza mfumo wa anwani za makazi katika
mkoa wa Dar es salaam. Akaunti hiyo inaitwa TCRA-Postcode Project
0150315694502 iliyofunguliwa katika benki ya CRDB tawi la Mlimani
City”,alisema Dk.Turuka.
Mradi huo uliozinduliwa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambaye kwa sasa ni Rais wa serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar mwaka 2009, tayari umekwisha fanyiwa majaribio mikoa ya Arusha
na Dodoma ambapo ulionesha mafaniko makubwa.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA
Prof.John Nkoma alisema ni pamoja na uhaba wa fedha na baadhi ya watu
wasiokuwa waaminifu kuiba miundombinu ya anuwani hizo ikiwemo vibao vya
kuonesha mitaa.
Nkoma alisema gharama za mradi huo mkubwa na unaoongeza ajira kupitia
utalii, tayari umekwisha peleka kikosi kazi nchini Afrika Kusini ili
kujifunza namna ya kuweka anuwani za makazi kwenye makazi yasiyopimwa.
Kwa upande wake Meya wa Jiji la Dar es salaam,Dk.Didas Masaburi alisema
jiji lina zaidi ya 70% ya maeneo ambayo hayajapimwa jambo linalofanya
kazi kuwa kubwa zaidi huku muda zaidi ukihitajika kutengwa ili
kuhakikisha kila nyumba inapatiwa namba yake.
Wajumbe wengine ni wizara ya Miundombinu na Mawasiliano ya Zanzibar,
Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati ya SMZ, Ofisi ya Rais,Tawala za
Mikoa-Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa pamoja na wizara ya Fedha.
Aidha,wajumbe wengine wa kamati hii ni viongozi wa juu wa taasisi
zifuatazo.Mkurugenzi Mkuu TCRA,Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta
Tanzania (TPC),Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Vitambulisho vya Taida (NIDA)
na Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Prof.Nkoma pia aliwatoa wasiwasi wananchi kuwa anuwani hizo hazimzuii
mtu yeyote kuhama kutoka eneo moja hadi jingine kutokana na kuwa na
mfumo unaowezesha kubadilisha anuwani kama ilivyo kwa kadi za benki
ambapo mteja huweza kubadilisha namba ya siri muda wowote apendapo.
No comments:
Post a Comment