Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Monday, September 3, 2012

Mwanamke Wa Kiislam: Hadhi Yake Katika Ummah



Siri ya umuhimu wa mwanamke wa Kiislam inatanda katika mzigo mkubwa na jukumu ambao alilowekewa mbele yake, na mashaka ambayo yako katika mabega yake. Jukumu na mashaka ambayo hata mengine mwanamme anaweza kubeba.

Hadhi ya mwanamke katika Uislam ina cheo kikubwa na iliyo na taadhimu, na taathira yake ni kubwa mno katika maisha ya kila Muislamu. Kwa kweli mwanamke wa Kiislamu ni mwalimu wa kwanza katika kujenga jamii njema, ikiwa kama atafuata mwongozo kutoka katika Kitabu cha Allaah na Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: “Nakuachieni vitu viwili, hamtapotea kamwe kama mkivishikilia kwa nguvu vyote viwili hivi, Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu.”[ii]

Kama ilivyokuwa katika ukawaida wa Qur-aan na Sunnah humwekwa kila Muislamu mwanaume au mwanamke mbali na upotofu kwa njia yeyote. Upotofu ambao mataifa mbali mbali yanaugua, na upotofu wao hauji ila kwa sababu ya kuwa mbali kabisa na njia ya Allaah, ambaye ni Mkamilifu kushinda wote, Aliye juu kabisa, na pia kuwa mbali na yale ambayo Mitume na Manabii wake (Rehma na Amani ziwafike juu wao wote) wamekuja nayo. Umuhimu mkubwa wa mwanamke wa Kiislam ikiwa mke, dada, au binti, haki ambazo zinatakiwa kutimizwa kwake na haki ambazo anatakiwa kutimiza zimefafanuliwa katika Qur-aan Tukufu, na maelezo zaidi ya haya yamefafanuliwa katika Sunnah iliyotakasika.

Siri ya umuhimu wake umetanda katika kazi yake nzito na mamlaka ambayo yamewekwa juu yake, na shida ambazo anabeba mabegani kwake - mamlaka na dhiki ambazo hata mwanaume hawezi kuzibeba.  Ndio maana imelazimishwa kwa mtu kuonyesha hisani kwa mama yake, kuonyesha upole na uhusiano wa ukaribu ulio mzuri kwake. na katika jambo hili, apewe ubora  kuliko baba mtu. Mwenyezi Mungu Mtukufu kasema:
 "Na Tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni Kwangu Mimi ndiyo marudio." [Surah Luqmaan 31:14].

Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kasema,
"Na Tumemuusia mwanaadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini".  [Surah Ah'qaaf 41:15].

Mtu alikuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa salam) na akasema,
"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Nani miongoni wa watu wote anastahiki uhusiano wangu wa karibu?" Mtume akajibu.  "Mama yako"
Yule mtu akauliza tena, "kisha nani?" Mtume akamjibu 
"Mama yako"
Yule mtu akauliza tena, "kisha nani?" Mtume akamjibu 
"Mama yako"
Yule mtu akauliza tena, "kisha nani?" Mtume akamjibu.
"Baba yako"[iii]

Kwahiyo haya yanasisitiza kwamba mama mtu anapewa heshima mara tatu kuliko baba mtu.

Na kuhusu mke, hadhi yake na taathira yake katika kutuliza moyo na kuliwaza imeonyeshwa wazi wazi katika Aayah Tukufu (kauli ya Allaah), katika msemo wake Mtukufu,
"Na katika Ishara Zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri. [Suuratur-Ruum 30:21].

Al-Haafidh Ibn Kathiyr (Aliyefariki 774H) - RahimahuLLaah - alisema katika kufafanua neno Mawaddah na Rahmah ambayo inapatikana katika Ayaah iliyopita, anasema:

"Al-Mawaddah inamaanisha mapenzi na  mahaba na Ar-Rahmah inamaniisha rehma (upole) na huruma - kama ilivyokuwa mtu anamchukuwa mwanamke ama kwa sababu ya mapenzi kwake, au kwa sababu ya mapenzi juu yake au kwa sababu ya upole na huruma juu yake, kwa kumpa mtoto kutokana na yeye..."[iv]
(Ziada: soma chini kuhusu maonyo ya kuchagua mke aliyoyatoa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam).

Na jinsi mke wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Bi Khadiyjah (Radhiya Allaahu 'anha) alivyosimama kwa namna ya pekee kusaidia sana kumliwaza na kumtuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)   wakati Jibriyl ('alayhis-salaam) alipojitokeza kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kwa mara ya kwanza katika pango la Hiraa.  Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alirudi kwa Bi Khadiyjah (Radhiya Allaahu 'anha) akiwa na wahyi wa kwanza na huku moyo wake unapiga na kutetemeka kwa nguvu, na akamwambia Bi Khadiyjah:
"Nifunika! Nifunike!"
Kwa hiyo, (Bi Khadijah) akamfunika mpaka hofu yake ilipotokomea, baadaye Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akamuelezea Bi Khadiyjah (Radhiya Allaahu 'anha) kila kitu kilichotokea na akasema
"Naogopa juu ya kutokewa na kitu kibaya"
(Bi Khadiyjah) akamwambia,
"Abadan! WaLlaahi! Allaah hatokuangusha. Unaweka mahusiano mema baina yako na jamaa zako, unawasaidia masikini na fukara, unawahudumia wageni wako kwa ukarimu na unawasaidia wale ambao wamekumbwa na maafa."[v]

Na usisahau kuhusu mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) pamoja na taathira yake. Hata Maswahaba watukufu walikuwa wanajipatia elimu ya Hadiyth kutoka kwake., na wengi katika Maswahabiyaat (wafuasi wa kike wa Rasuulu-Allaah) walijifunza vitu mbali mbali kuhusu Sharia zilizowahusu wanawake kutoka kwake.

Sina shaka ya kwamba mama yangu- Allaah Amrehemu - alikuwa na taathira makubwa juu yangu, alikuwa ananihimiza nisome, na alikuwa ananisaidia kwa hilo. Allaah Amuongezee thawabu na Amlipe kwa malipo mema kwa yote aliyonifanyia.

Na pia bila shaka, nyumba ambayo ina huruma, upole, upendo na kujali, pamoja na mafundisho mema ya Kiislam itamuathiri mtu. Kwa hiyo atakuwa - ikiwa Allaah atapenda - mwenye kufanikiwa katika mambo yake na katika kitu chochote - ikiwa kutafuta ilmu, biashara, kupata maisha mazuri, au vingine baada ya hivi. Kwahiyo ni Allaah peke Yake ninayemuomba Anipe mafanikio na Atuongoze sote kwenye yale ambayo Anayapenda na Anaridhia. Na Salam na Amani za Allaah zimfikie Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)    na familia yake, Maswahaba zake na wafuasi wake. 






[i] Ni mtu ambaye anayestahili kufuatwa: Abu ‘Abdillaah, ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Baaz. Alizaliwa katika mji wa Riyaadh (Saudi Arabia) katika tarehe ya kumi na mbili (12) ya Dhul-Hijjah katika mwaka wa 1330H. Alianza kutafuta elimu kwa kuhifadhi Qur-aan kwanza kabla ya hata kubaleghe. Baada ya hapa, alianza kusoma elimu au maarifa ya Kiislam kama vile Aqiydah (Imani au Itikadi), Fiqh (Shari’ah ya Kiislam), Hadiyth, Usuulul-Fiqh (Sayansi ya Sheria), Faraaidh (Mirathi), Nahw (Nahau au Sarufi) na Swarf (elimu ya umbo na ujenzi wa wanyama, mimea na lugha) - Shaykh huyu aliweza kufanya yote haya japokuwa alipata upofu wa macho wa kudumu  wakati akiwa na umri wa miaka kumi na nane. Alisoma maarifa ya Kiislam chini ya wanavyuoni maarafu wa Riyaadh na Makkah, wakiwemo Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Latwif bin ‘Abdir Rahmaan bin Hasan na pamoja na Mufti wa zamani ambaye ni mwanachuoni bora, Shaykh Muhammad bin Ibraahiym - ambaye alisoma kwake kwa miaka kumi. Aliishi miaka thamanini na tisa, alikuwa mpole, mkarimu, mstahamilivu, lakini thabiti katika maumbile yake, alikuwa na busara wakati alipokuwa anazungumza mazungumzo ya haki (ukweli). Alikuwa Zaahid (mtu ambaye anajiepusha) juu ya mambo ya kilimwengu na alikuwa mmoja wa wanavyuoni wakuu wa Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah (Wenye kufuata mwendo wa Mtume na Maswahaba) katika umri wake. Shaykh Abu ‘Abdillaah ‘Abdul ‘Aziyz ambaye alikuwa ni mtu bora, kwa rehma ya Allaah aliweka bidii katika maisha yake yote juu ya Uislam na watu wake. Na ni mwandishi wa vitabu vingi vikiwemo vitabu vidogo vidogo, akiwafundisha na kuwatumikia watu chungu nzima, na pia alikuwa na bidii (hodari) katika upande wa Da'waah. Allaah amsamehe Shaykh wetu ambaye ni pia kama baba yetu.
Makala hii ni majibu kuhusu suala maalum ambalo lilihusu cheo na hadhi ya mwanamke wa Kiislamu na imepatikana kutoka Majmu’ul Fataawaa wa Maqaalaatil Mutanawwi`ah (3/348-350) ambayo ni ya Shaykh Abu ‘Abdillaah, ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Baaz.

[ii] Hasan: Imesimuliwa na Maalik katika al-Muwattwaa (2/899) na al-Haakim (1/93), kutokwa kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu). Ilithibitishwa na Shaykh al-Albaaniy katika as-Swahiyhah (Namba 1871).
[iii] Imesimuliwa na al-Bukhaariy (Namba 5971) na Muslim (7/2), kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu).
[iv] Tafsri ya Qur-aan Tukufu (3/439) ya al-Haafidh Ibn Kathiyr.

[v] Imesimuliwa na al-Bukhaariy (1/22) na Muslim (1/139), kutoka kwa masimulizi marefu yaliyopokewa kutoka kwa mama wa waumini  'Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhu).

No comments:

Post a Comment