Sehemu Ya Kwanza
Katika
usiku wa giza, Abu Lu’lu’ Al-Majuusi alijificha katika vivuli
akijiandaa kwa ajili ya Swalaah ya Alfajiri, wakati ambapo ataendesha
mipango yake ya kishetani kumuua Amiyr wa waumini – ‘Umar bin
Al-Khattwaab (Radhiya Allahu ‘anhu).
‘Umar
(Radhiya Allahu ‘anhu) alikuwa (na kawaida) ya kuongoza Swalah ya
Alfajiri huku akisoma surah ndefu, akiwapa wafuasi wa jamii, muda wa
kuhudhuria mkusanyiko (wa Swalaah). Katika siku hii, wakati (‘Umar)
akisoma (Qur-aan), Abuu Lu’Lu’ akachukua hatua kutoka kwenye nguzo
inayofifia, hali ya kuwa ana kisu cha sumu katika mkono wa vazi lake.
Akaruka mbele ya ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) na akamkata tumbo wazi kwa
(kile) kisu. Baada ya hapo, akajaribu kuukimbia mkusanyiko. Akiwa ana
chana chana mbele na nyuma, akiwauwa watu wengi zaidi ambao walikuwepo
katika njia yake. Swahaabah mmoja akamtupia nguo juu yake na alipo
tahayari kwamba keshakamatwa Abu Lu’lu’ akajiua.
‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (Radhiya Allahu ‘anhu) akaikamilisha Swalaah ya Alfajiri ambayo aliianza ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu). ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) alikamilisha Swalaah yake hali ya kuwa ni miongoni mwa watu (maamuma) katika Jama’ah na akafariki dunia baadaye katika kitanda chake, (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Umuhimu
wa Swalaah katika Uislamu hauwezi kudharauliwa. Ni nguzo ya kwanza ya
Uislamu iliyotajwa na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi
wa sallam) baada ya tamko la Imani (shahaadah), ambayo kutokana nayo mtu
huwa Muislamu.
Swalaah
imefaradhishwa kwa Manabii na watu wote. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
Alitangaza hadhi yake ya kuwa ni faradhi katika tukio Tukufu. Kwa mfano,
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alipozungumza na Muusa (‘Alayhis Salaam),
Amesema:
{{Nami nimekuteua wewe; basi sikiliza unayofunuliwa. Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana mungu ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na ushike Swalah kwa ajili ya kunikumbuka Mimi}} [Twaaha: 13-14]
Hivyo
hivyo, Swalaah imefaradhishwa kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati alipopelekwa mbinguni. Zaidi, wakati
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anawasifu waumini kama katika
Suratul-Al-Mu-uminuun, moja katika sifa ambazo Anazitaja kuhusiana nao
ni kule kushikana kwao na Swalaah:
{{Hakika wamefanikiwa Waumini. Ambao ni wanyenyekevu katika Swalah zao}} [Al-Mu’minuun: 1-2]
Umuhimu
wa Swalaah unaendelea kuonyeshwa katika kauli nyingi za Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa mfano, Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:
“Jambo
la kwanza ambalo mja atahukumiwa katika Siku ya Hisabu ni Swalaah. Kama
ikiwa ni nzuri basi amali zake zilizobakia zitakuwa nzuri. Na ikiwa ni
mbaya, basi amali zake zilizobakia zitakuwa mbaya.” [At-Twabaraaniy].
Kwa kweli, ikiwa Swalaah imeswaliwa vizuri ikiambatana na ukumbusho wa kweli wa kumkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), na kumgeukia Yeye kutaka msamaha, itakuwa na athari kubwa juu ya mtu kwa kipindi kirefu. Mtu anapokamilisha Swalaah yake, moyo wake utajaa ukumbusho wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Atakuwa ana hofu na pia vilevile matarajio juu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Baada ya tukio hilo, hatotaka tena kuondoka kutoka katika sehemu hiyo ya fakhari kuelekea kwa ile ambayo ndani yake atamuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) anaitaja hali hii ya Swalaah katika Qur-aan:
{{Hakika Swalah inazuilia mambo machafu na maovu}} [Al-‘Ankabuut: 45].
Lakini katika wale ambao wanaoswali, utakuta kuna vitendo vya kivivu ambavyo vinahitaji kumulikwa. Kwa mfano:
· Wengine hawazingatii kile ambacho wanakisema.
· Wengine wanafanya haraka katika Swalah zao
· Wengine wanaachilia nadhari yao ya macho izurure wakati wa Swalah
· Wengine mara kwa mara husahau nambari ya rakaa zilizotimizwa.
· Dunia inakumbatia mioyo ya baadhi ya watu wakati wa Swalah na inafunika akili zao.
· Na watu wengine katika Jama’ah wanaanza kusujudu kabla hata ya Imaam kusema “Allaahu Akbar”
Linganisha
hii (hali yetu katika Swalaah) na Swalaah za watu ambao walikuja kabla
yetu. Watu walikuwa wanafikiria ya kwamba Ar-Rabiy’ bin Khaytham alikuwa
ni kipofu kwa sababu ya kuinamisha macho yake mara kwa mara. Alikuwa
akiishi nyumbani kwa AbduLlaah bin Mas’uud (Radhiya Allahu ‘anhu) kwa
miaka ishirini na mtumwa wake wa kike akimuona alikuwa akisema: “Rafiki
yako kipofu anakuja” na AbduLlaah alikuwa akimcheka kwa kauli yake.
Ndani ya AL-Bukhaariy na Muslim, Abuu Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu) anatueleza ya kwamba, kuna mtu aliingia msikitini, ambao Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekaa. Akaswali rakaa mbili na kisha akaja kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akatoa salamu. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaijibu
salamu yake na halafu akasema, “Rudi tena ukaswali kwani hukuswali.”
Hivyo, yule mtu akarudi, akaswali (rakaa mbili) kama alivyofanya mara ya
kwanza, akaja tena na kurudia kutoa salamu. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaijibu salamu na akasema “Rudi tena ukaswali kwani hukuswali.” Hivyo, yule mtu akarudi, akaswali (rakaa mbili) kama alivyofanya mara ya kwanza akaja tena na kurudia kutoa salamu. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijibu salamu kwa mara nyingine tena na kwa mara nyingine tena akasema: “Rudi tena ukaswali kwani hukuswali”. Hadi kufikia mara hii ya tatu, mtu huyo alisema: “Naapa kwa Yule ambaye alikutuma wewe na ukweli, Ewe Mtume wa Allaah, sijui vyovyote isipokuwa hivi, Nifundishe.” Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
“Ikiwa
unasimama kwa ajili ya Swalaah sema “Allaahu Akbar”. Halafu soma
ambacho kitakujia kwa wepesi katika Qur-aan. Kisha rukuu mpaka
utakapohisi kwamba umetulia katika rukuu yako. Kisha, simama mpaka uwe
umesimama wima kisawa sawa. Kisha, sujudu mpaka uwe umetulia katika
sujudu yako. Kisha keti mpaka uwe umetulia katika juluus yako. Kisha
sujudu mpaka uwe umetulia katika sujudu yako. Na uwe unafanya hivi ndani
ya Swalaah yako yote”.
(Kwahiyo turudi tukarudie Swalah zetu)
Kwanini
tunakuja msikitini; nini sababu yetu ya kutekeleza Swalah? Tunafanya
hivyo kwa kufuata amri ya Muumba wetu (Subhaanahu wa Ta’ala). Kwanini
hasa tupoteze baraka na thawabu kwa sababu ya moyo usiotulia na mkono
unaowasha. Khushuu ni kiini cha Swalaah zetu. Khushuu ni matunda ya
imani yetu. Lakini, hata baada ya kujua haya, watu hawafanyi juhudi
kukamilisha Swalah zao na kwa hiyo huandikiwa sehemu ndogo tu. Mtume
Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema;
“Kwa
hakika, mtu ataondoka (katika Swalaah yake) na ataandikiwa (thawabu)
kumi za Swalaah yake; tisa, nane, saba, sita, tano, nne, tatu, nusu.” [Abu Daawuud na at-Tirmidhiy]
‘Uthmaan bin Abii Dahshah (Radhiya Allahu ‘anhu) alisema: “Sijawahi
kuswali Swalah ambayo baada yake nilikosa kumuomba Allaah (Subhaanahu
wa Ta’ala) Anisamehe kwa upungufu wangu katika Swalah ile.”
Mtu ambaye anaharakisha Swalah yake ni mwizi. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema katika Hadiyth sahihi, “Mwizi muovu kuliko wote ni yule ambaye anaiba katika Swalaah yake”. Swahaaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakauliza: “Ewe Mjumbe wa Allaah, anaibaje katika Swalah yake?” Naye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hakamilishi rukuu na sujudu zake”
Kwa
sababu ya kasi ya jinsi ya watu wanavyoswali, wanaonekana kama ndege,
wanaodonoa juu na chini. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) alikataza mtu kudonoa (katika Swalah) kama kunguru.
‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) wakati mmoja alisimama katika Minbari akiuhutubia umati wa watu kwa sauti ya nguvu akisema,
“Mtu anaweza akakulia mpaka utu uzima katika Uislamu na asiweze kamwe
kukamilisha kwa ajili ya Allaah hata Swalah moja!” (Watu) wakasema,
“Vipi hali hii?” (‘Umar) (Radhiya Allahu ‘anhu) akasema: “Hakamilishi
khushuu yake, hata unyenyekevu wake, hata nadhari yake juu ya Allaah
‘Azza wa Jalla.”
Wakati mmoja, Ma’aruuf Al-Karkhiy (Rahimahu Allaah) aliposimama miongoni mwa wanafunzi wake, mmoja wao akamwambia mwenziwe, “Tafadhali swalisha Swalaah ya ‘Ishaa”. Mwanafunzi wa kwanza akakubali lakini akasema “Nitaswalisha Swalaah ya ‘Ishaa kwa sharti ya kwamba wewe utaswalisha Swalaah ya Alfajiri sio mie” Ma’aruuf Al-Karkhiy alishtushwa na kauli aliyoisema na akasema, “Naapa kwa Allaah, ikiwa unafikiria ya kwamba utakuwa hai wakati wa Alfajiri, basi naapa kwa Allaah, hujakamilisha Swalah yako”.
Sehemu Ya Pili
Jinsi ya kuwa na Khushuu ndani ya Swalah
Al-Qaasim bin Muhammad (Rahimahu Allaah) alisema: “Nilikwenda nje siku moja, na kila nilipotoka ni lazima nipite kwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anha) na kumsalimia. Siku hiyo nilitoka na nilipomkuta mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anha) akiswali Swalah ya Dhuhaa, akisoma tena na tena Aayah ya Allaah:
{{Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa (adhabu ya Allaah). Basi Mwenyezi Mungu Akatufanyia hisani na Akatulinda na adhabu ya Moto.}} [At-Twuur: 26-27]
Alikuwa
analia na akimwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na huku akirudia
Aayah hiyo. Nilisimama pale mpaka nikachoka, hali ya kuwa yeye amebaki
kama nilivyomkuta. Nilipoona haya nilijiambia, “Hebu niende sokoni,
nifanye ninachotakiwa kufanya, halafu nije tena”. Kwa hiyo, baada ya
kumaliza kufanya nilichotaka kufanya sokoni, nilirudi kwa mama wa
Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anha). Alikuwa kama nilivyomuacha, akirudia Ayaah, akimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na akilia”.
Vipi tuwe na khushuu katika Swalaah?
Katika Sunnah ya Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam tunafundishwa yafuatayo:
1. Njoo mapema kwa ajili ya Swalaah na jitayarishe kuwa na khushuu.
Fuatiliza
adhana pamoja na Mu’adhin na baada ya adhana, sema dua iliyoamriwa.
Omba dua baina ya Adhaana na Iqaamah. Tia wudhuu vizuri, hali
ukisukutuwa mdomo wako, na vaa nguo zako nzuri kabisa.
2. Nuia kupata dhawabu zote za Swalaah yako.
Abu Bakr bin ‘Iyaash alisema, “Nilimuona Habiyb bin Thaabit katika sujudu. Ukimuona utadhania kwamba kashakufa (kwa urefu wa sujudu zake).”
3. Zingatia Aayah na adhkaar ambayo inasomwa ndani ya Swalaah.
Fikiria kuhusu maana za Aayah ambazo unazisoma. Je haivunji moyo ya kwamba mtu anaweza kuswali miaka kumi baada ya kumi, siku baada ya siku na pia bado hajui anasema nini? Qur-aan iliteremshwa ili itafakariwe! Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Kateremsha (katika Qur-aan Ayaah inayosema):
{{Na hiki Kitabu, Tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili.}} [Swaad: 29].
4. Swali Jama’ah. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anaamrisha:
{{Na shikeni Swalah, na toeni Zakaah, na rukuuni pamoja na wenye kurukuu.}} [Al-Baqarah: 43].
5. Usikose
kamwe kuswali Swalah zako za nawaafil (Sunnah zilizotiliwa mkazo), hasa
zile ambazo Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
alikuwa akiswali siku zote, kama vile Witri na Sunnah ya Alfajiri.
6. Usiharakishe Swalah yako.
Chukua
muda wako na usikubali kuifanya Swalah yako kuwa kitendo kilichokuwa
hakina thamani katika siku yako. Ibn Wahb (Rahimahu Allaah) alisema: “Nilimuona Ath-Thawriy (Rahimahu Allaah) kwenye Kaa’bah. Baada
ya Swalah ya Magharibi, alinyanyuka kuswali na kisha akasujudu.
Hakunyanyuka katika ile sujudu mpaka adhana ya ‘Ishaa ilipoadhiniwa.”
7. Jua
ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anajibu Swalah yako. Mtume
Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
“Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Aliyetukuka alisema: “Nimeigawa Swalah kati Yangu na mja Wangu katika
nusu mbili, na mja Wangu atapata alichokiomba” [Kutoka katika Surat ul-
Faatiha ] Wakati mja anaposema, “Sifa njema zote ni za Allaah
(Subhaanahu wa Ta’ala), Mola Mlezi wa viumbe vyote,” Allaah (Subhaanahu
wa Ta’ala) Anasema, “Mja Wangu Amenihimidi” . Wakati mja anaposema
“Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.” Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
Anasema, “Mja wangu Amenisifu.” Wakati mja anaposema, “Mwenye Kumiliki
Siku ya Malipo”, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema mja Wangu
Amenitukuza”. Wakati mja
anaposema, “Wewe tu tunakuabudu na wewe tu tunakuomba msaada.” Allaah
(Subhaanahu wa Ta’ala) anasema, Hii ni kati Yangu Mimi na mja Wangu, na
mja Wangu atapata alichokiomba”. Wakati mja anaposema “Tuongoze katika
njia iliyonyooka, njia ya uliowaneemesha, sio ya wale uliowakasirikia, wala ya wale waliopotea,” Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema, “Hivi vyote ni kwa ajili ya mja Wangu, na mja Wangu atapata alichokiomba” [Muslim]
8. Swali pamoja na kizuizi (weka sutrah) mbele yako na swali karibu yake.
Kitu
chengine ambacho kitakusaidia kuwa na khushuu’ [utulivu] ni
kushughulika (au kuwa makini) katika suala la kuwa na kizuizi (sutrah)
na kuswali karibu yake. Kuwa na sutrah kutazuia uoni wako, kutakulinda
juu ya Shaytwaan, na kutazuia watu kupita mbele yako, kitu ambacho
husababisha wasiwasi na hupunguza thawabu za Swalah. Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
“Ikiwa mmoja wenu ataswali basi na aswali akielekea kwenye sutrah, na awe karibu nayo” [Abuu Daawuud].
9. Tafuta ulinzi] kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kutokana na Shaytwaan.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitufundisha vipi tupambane na wasi wasi wa Shaytwaan. Abu’l- ‘Aas (Radhiya Allahu ‘anhu) kasimulia ya kwamba alisema, “Ewe
Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),
Shaytwaan ananisumbua wakati ninaswali, na hupata wasiwasi katika kisomo
changu.” Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
akasema, “Huyo ni Shaytwaan ambaye
jina lake ni Khanzab. Ikiwa utahisi kwamba yupo, jilinde kwa Allaah
(Subhaanahu wa Ta’ala) kutokana naye, na tema mate (makavu) katika
upande wako wa kushoto mara tatu”. Abu’l –‘Aas (Radhiya Allahu ‘anhu)
alisema: “nilifanya hivyo na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
Akaniondoshea.” [Muslim].
10. Swali kama kwamba umeambiwa kuwa baada kumaliza Swalah utarudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Abu Bakr Al-Muzaniy (Subhaanahu wa Ta’ala), alisema, “Kama unataka Swalah yako ikufae, basi sema: “Nitakufa baada tu ya Swalah hii!”
No comments:
Post a Comment