Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Wednesday, September 5, 2012

Yampasayo Maiti



Kila sifa njema anastahiki Allah na rehma na amani zimfikiye Mtume Muhamad na ahli zake na sahabaze na wenye kufuwata wayo kwa ihsani mpaka siku ya mwisho,

Ama baa’d
Watukufu Waislamu taratibu za kumfanyia mmoja wetu, anapofikwa na umauti ni muhimu sana kwa kila muislamu kuzijuwa, kwani wengi wetu hawalifahamu vyema somo hili kama alivyotufundisha Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam], kwa maana hiyo tumechukuwa muda mwingi kuandaa maudhui haya yaliyo muhimu sana, tunaomba kila Muislamu kusoma kwa makini maudhui haya ili aweze kuufahamu vyema mchakato mzima wa ibada ya maziko, tunaanza darsa hii mwanzo kabisa, tunaomba sote tuwe wenye kuzingatia.

Kumlaqinia afikwaye na umauti
Amesema Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] walaqinieni wafikwao na umauti, kwa neno LAILAHAILALLAH na mwenye kufa hali ametamka neno hili bila shaka ataingiya peponi. Tazama  Swahihi Muslim vol.2, uk. 631, Swahihi Bukhari vol.1, uk.532. Vile inajuzu kwa Muislamu kumtembelea kafiri na kumlaaqinia ili asilimu

Dalili: alikuwa kijana mmoja wa kiyahudi akimuhudumia Mtume[swalallahu alaihi wasalam] akawa amepatwa na maradhi kijana huyo, Mtume akenda kumzuru kijana huyo, akamkuta yuko hoi kitandani na baba yake yuko pembeni , mtume alipoingiya akawa ameketi karibu na kichwa cha kijana huyo akamsalimia, kisha akamwambia silimu, yule kijana akawa anamuangalia baba yake, baba yake akamwambia mtii Abal Qasim[Mtume] ewe mwanangu! Kijana akamtii Mtume [swalallahu alaihi wasalam] na akasilimu, Mtume akatoka huku akisema namshukuru MwenyeziMungu ambaye amemuokowa kijana na moto, alipokufa huyo kijana Mtume [swalallahu alaihi wasalam] akasema kuwaambiya masahaba msalieni rafiki yenu.
Tazama Musnad Ahmad, vol. 3, uk.175, Swahihi Bukhari Vol.1, uk.575.

Yanayowapasa walio karibu na Maiti
Inapokuwa roho imechukuliwa na Malakul-mauti yaani [Malaika wa mauti] na ndiyo jina lake khaswa [siyo izrael] kama watu wengi walivyozowea, jina hili la malakul mauti ndiyo Allah Ta’ala alivyomuita malaika huyo katika Quraan surat Assajdah aya ya 11; Sema ewe [Mtume] uwaambie kuwa atakufikieni Malaika wa mauti aliyewakilishwa kwenu.
Yawapasa Walio karibu na maiti kufanya yafuatayo:
Mosi linalowapasa walio karibu na maiti ni kumfumba macho,
        Dalili: aliingia Mtume nyumbani kwa Abi salman na alikuwa Abi Salman amekodoa macho yake, Mtume akayafumba kisha akasema roho inapochukuliwa macho hufuatisha ile roho inapokwenda. Tazama Musnad Ahmad vol.6 uk.297, Sunan Baihaqi uk.334.
      ii. Jambo la pili ni kumuombeya Duwa Maiti
Dalili: Mtume[Swalallaahu alaihi wasalam] alipofumba macho ya Abi Salman, na huku watu wa Abi  Salman wanaliya kwa kupiga kelele akasema Mtume kuwaambiya; msiombe katika nafsi zenu ila muombeeni kheri kwani hakika Malaika wanaitikia aamin! Juu ya mnayoyasema, kisha Mtume akasema ewe MwenyeziMungu msamehe Abi Salman na inyanyue daraja yake iwe katika watu waliongoka, na utusamehe sisi na yeye ewe Mola wa walimwengu wote na uitanue kaburi yake na utie nuru ndani yake. Taz. Musnad Ahmad vol.6 uk.297
Jambo la tatu; ni kumfunika maiti kwa nguo yenye kusitiri mwili wake wote, 
Dalili: Amesema Bibi Aisha [Radhiyallaahu 'anha] alipokufa Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] alifunikwa kwa nguo iliyositiri mwili wake wote. Rejea Swahih Bukhari Vol.2 uk.651, Sunan Baihaq Vol. 3 uk.385, na jambo muhimu sana kwa wafiwa ni kuwa na subira na kuridhia kwa kile kilichowafika ameema MwenyeziMungu katika Quraan “Na tutakutieni katika msuko suko wa hofu, na njaa na upungufu wa mali, watu na matunda na wapashe habari njema wanaosubiri [al-Baqara aya ya 155] , muhimu ni kutaraji kwa MwenyeziMungu kwa lile lililowafika.

Amesema Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] hakuna Muislamu yoyote mwenye kupatwa na msiba kisha akasema yale aliyoamrishwa na MwenyeziMungu, aseme hivi:- Inalillah Wainailaihi Rajiun, Ewe MwenyeziMungu nipe malipo kutokana na msiba wangu na unibadilishie kheri zaidi  kuliko hii, isipokuwa Mwenyezi Mungu humbadilishia zaidi ya hilo. Taz. Swahihi Muslim Vol.3 uk.37, Sunan Bayhaq vol.4 uk.65, Musnad Ahmad Vol. 6 uk 309
Jambo lingine lenye kujuzu ni kwa walio karibu na maiti ni kuingia ndani na kumfunua uso maiti na kumbusu na kulia kwa kutoa machozi tu,na sio kujipiga piga. Dalili: aliingiya Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] kwa sahib wake Uthman Bin Madhoun alipofariki, akamfunuwa uso wake akambusu, na akawa analia mpaka machozi yakawa yanatiririka mashavuni kwake. Taz. Majmau Zawaid ya Haithami Vol. 3 uk 2, Sunan Tirmidhiy Vol.2 uk.130, pia wakati alipokufa Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam], aliingiya Abubakar [Radhiyallaahu 'anhu] kwa Aisha, Mtume alikuwa  ameshafunikwa nguo, Abubakar [Radhiyallaahu 'anhu] akamfunua usoni, kisha akambusu kati ya macho yake na akalia. Taz. Swahihi Bukhar Vol. 3 uk.89, Sunan Nnasai Vol. 1 uk 26, Ibn Hiban hadith namba 2100, Sunan Bayhaq Vol. 3 uk. 406.
Kumbuka mtukufu Muislamu yule tu aliyekufa akihirimia katika ibada ya Hija, haitakiwi kumfunika uso wake wala kichwa chake
Tunakumbusha ndugu waislamu kuwa haifai kabisa kulia kwa sauti ya makelele, wala kwa kujipiga piga usoni, kutimuatimua nywele, kujichania nguo, kujikwarua kwarua, kujipaka unga na kujimwagia mchanga, haya si katika maomboleo ya kiislamu yapaswa tujihadhari nayo sana.
Dalili: amesema Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] si katika sisi Waislamu mwenye kulia kwa kujipigapiga, kujichania nguo na kuomboleza kwa maombolezo ya kijahiliya, Taz. Swahihi Bukhar Vol.3 uk.127, Swahihi Muslim Vol.1 uk.70
Na amesema tena Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam], jambo hili la kulia kwa kelele si katika mwenendo wangu, bali moyo unahuzunika na macho yanatoa machozi na wala asikasirikiwe Mwenyezi Mungu. Taz. Mustadrak ya Hakim Vol. 1 uk. 382, Ibn Hiban uk 743
Dalili: amesema sahaba wa Mtume[Swalallaahu alaihi wasalam]Anas Bin Malik ya kuwa amesema Mtume, subira inatakikana mwanzo wa pigo[matatizo], Taz, Swahihi Bukhari hadith namba 1252, Swahih Muslim hadith namba 15, Abu Dawd hadith namba 3124

 KUHARAKISHA KUMTAYARISHA MAITI
Amesema sahaba Jaabir Bin Abdillah [Radhiyallaahu 'anhu] kwamba alikufa mtu mmoja, haraka tukamuosha na kumvika sanda na tukamtia manukato na tukaweka linapowekwa jeneza ili Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] amswalie. Taz. Mustadrak ya Hakim Vol.2 uk.58, Sunan Bayhaq vol.6 uk.74, Majmau Zawaid ya Haitham vol.3 uk.39, Musnad Ahmad vol.3 uk 330.

 UTARATIBU WA KUOSHA MAITI
Amesema Imam Abu Hanifa na Imam Malik yakuwa:-anapooshwa maiti avuliwe nguo zake na isitiriwe sehemu zake za siri, wala asikatwe kucha, ndevu, nywele, wala kwapa wala sehemu za siri. Taz. Bidayatul Mujtahid uk.192, Al Mizanil kubra uk.93
Amesema Imam Ibn Qudamah: Ataandaa muoshaji vipande viwili vya kitambaa, kisha atapitisha mkono wake wa kulia tumboni kwa maiti, akimkamua tumbo taratibu na kwa upole, kisha atachukuwa kitambaa kimoja na kuanza kumsafisha maiti sehemu za siri kwa kitambaa, kisha amtawadhishe maiti udhu wa sala na wala asiingize maji mdomoni kwake wala puwani, na ikiwa pana uchafu mdomoni au puwani undolewe kwa kitambaa, kisha aanze kumuosha maiti upande wa kulia na kisha kushoto. Taz. Al Mughni ya Ibn Qudama, vol.2 uk.256.
Na amesema Imam Ahmad Bin Hambal yakuwa:-anapomaliza kutawadhishwa maiti aoshwe kuanzia kichwa chake ndevu zake na upande wa kulia.

Na amesema sheikh Abdullah Ibn Baaz:- Utaratibu wa kuosha maiti ni kumsitiri sehemu zake za siri, kukamua tumbo lake kwa taratibu na kwa upole na kumsafisha kwa kitambaa sehemu za siri kisha kumtawadhisha udhu wa sala na kisha kumuosha kichwa chake, ndevu zake, kisha upande wa kulia alafu kushoto mara tatu au tano, jinsi utakavyoona, Taz. Majmou Fatawa ya Ibn Baaz-durusul muhimah uk.12

KUANZA KULIYANI NA SEHEMU ZA UDHU
Dalili: Amesema Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] alipokuwa akiwaambia wanawake walokuwa wakimuosha binti yake, Zainab alipofariki , aliwaambia hivi:- anzeni kuliani kwake na sehemu za udhu. Taz.Swahihi Bukhar hadith namba 1256, Swahihi Muslim hadith namba 43, Sunan Abu Dawd hadith namba 3145.

Na amesema Imam Shafii ya kuwa: Ni bora kumuosha maiti Kwa maji ya kawaida ila ikiwa kuna baridi kali ndiyo akoshwe kwa maji ya moto [vuguvugu], Taz. Al Mizanul Kubra uk.93

KUMUOSHA MAITI KWA MAJI YA MKUNAZI AU SABUNI
Dalili: amesema Ummu Atwiyyah [Radhiyallaahu 'anha]kuwa aliingiya Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam]kwetu alipofariki  binti yake akasema muosheni mara tatu au tano kwa maji ya mkunazi.
Taz. Swahihi Muslim Vol.3 uk 47, Abu Dawd vol.2 uk 6, Sunan Nnasaiy Vol.1 uk 266.
La muhimu piya kwa maiti mwanamke mwenye nywele ndefu zilizosukwa, zitafumuliwa na  kisha kuzichana na kuzisuka upya kwa mistari mitatu na kuitupa nyuma yake.
Dalili: Amesema Ummu Atwiyya [Radhiyallaahu 'anha] tulipomuosha binti ya Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] tulizifumua nywele zake, kisha tukaziosha na kuzichana, na kuzisuka kwa mistari mitatu tukazitupa nyuma yake. Taz.Swahihi Bukhari vol.3 uk.104, Swahihi Muslim vol.3 uk.48, Musnad Ahmad vol.5 uk.408

MAJOSHO KAMILI YAWE MARA MOJAMOJA
Dalili: Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam], aliwaambia wanawake walokuwa wakimuosha binti yake; Muosheni josho kamili mara moja moja na liwe josho hilo mara tatu au tano au zaidi jinsi mtakavyoona , Taz. Swahihi Bukhari hadith namba 1263, Swahihi Muslim hadith namba 41.

Na amesema Imam Ibn Qudama yakuwa anapomaliza kuoshwa maiti, akaushwe kwa nguo ili zisilowe sanda zake, Taz. Al Mughni ya Ibn Qudama vol.2 uk.464.

KUMUWEKA MAITI MANUKATO
Wapendwa waislamu yatakikana tuwapambe maiti wetu kwa manukato mazuri mazuri, Dalili:- Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] aliwaambia wanawake walokuwa wakimuosha binti yake; Na muwekeeni mwisho wa kumuosha chochote katika manukato. Swahihi Bukhari vol.3 uk.99, Swahihi Muslim vol.3 uk.47, Sunan Tirmidhi vol.2 uk 130, Sunan Nnasai vol.1 uk.266

INAJUZU KWA MUME KUMUOSHA MKE
Dalili: Amesema Bibi Aisha [Radhiyallaahu 'anha] mkewe Mtume yakuwa; aliporejea kwangu Mtume akitoka mazikoni, na mimi nikiwa na maumivu kichwani, na huku nikisema Ee! Maumivu ya kichwa changu [kichwa chaniuma] Mtume [Swalallashu alaihi wasalam] nae akasema, Bali hata mimi Ewe Aisha najisikia maumivu ya kichwa changu, maumivu hayo hayatakudhuru, na lau ukifa kabla yangu basi, nitakusimamia, kukuosha na kukuvika sanda, kukusalia na kukuzika.
Musnad Ahmad vol.6 uk.228, Addaarimiy vol.1 uk 7, Siyrat Ibn Hisham vol.2 uk 366

INAJUZU KWA MKE KUMUOSHA MUME
Dalili: Amesema Bibi Aisha [Radhiyallaahu 'anha]; Lau ningekuwa nimelielekeza jambo la kumuosha Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] alipofariki kuwa jambo hilo katika amri yangu mimi, nisingelipa mgongo jambo hilo na wasingemuosha Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] isipokuwa wakeze
Ibn Majah vol.1 uk.446, Ibn Hiban hadith namba 2156, Mustadrak ya Hakim vol.3 uk.59

SHARTI NA FADHILA KWA MWENYE KUOSHA MAITI
Wapendwa Waislamu ibada hii ya kuosha maiti ina sharti na fadhila zake amesema Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam]ya kuwa; Mwenye kuosha maiti muislamu kisha akasitiri aibu aliyoiona kwa yule maiti, husamehewa madhambi yake mara arobaini.
Mustadrak ya Hakim vol.1 uk.354, Majmau Zawaaid ya Haithami vol.3 uk.21, AL Mundhir vol.4 uk 17. Na amesema Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] yakuwa; Hakika Mwenyezi Mungu hakubali amali yoyote ile, mpaka ifanywe kwa ajili ya kutakwa radhi zake yeye MwenyeziMungu. Sunan Nnasai vol. 4 uk.171.

UTARATIBU WA KUMVIKA SANDA MAITI
Amesema Bibi Aisha [Radhiyallaahu 'anha] ya kuwa; alikafiniwa Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] katika nguo tatu nyeupe, hakuna kanzu wala kilemba katika sanda hizo tatu alizokafiniwa Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam]
Sunan Baihaqi vol.3 uk.399, Musnad Ahmad vol.6 uk.40, Abu Dawud hadith namba 3052

Ndugu waislamu ni wajibu kumvika sanda nzuri maiti, na sanda [au] thamani yake itokane na mali ya maiti , ndugu zake, jamaa zake, na isiwe sanda ya thamani  kubwa, na avikwe maiti sanda hiyo kwa utaratibu alofundisha Mtume [Swalallashu alaihi wasalam] bila kuzidisha chochote. Amesema MwenyeziMungu; Hakika mnao mfano mwema wa kuiga kwa Mtume wa MwenyeziMungu [Ahzab aya ya 21]
Kwa muktadha huo sanda iwe nzuri, amesema Mtume [Swalallsahu alaihi wasalam] Mmoja wenu anapomvika sanda ndugu yake, basi amvike sanda iliyo nzuri akiweza,
Swahih Muslim vol.3uk50 Abu Dawd vol.2 uk.62, Musnad Ahmad vol.3. uk.295, Sunan Tirmidh vol.2 uk.133.

Na amesema Imam Ibnu Mubarak: Na muradi wa sanda nzuri ni ile sanda iwe safi na yenye kutosha kumsitiri maiti mwili wake wote, na siyo kufanya isirafu katika sanda kwa kununua sanda ya thamani kubwa.

AINA YA SANDA
Dalili; amesema Mtume [Swalallashu alaihi wasalam]:- Vaeni katika nguo zenu nyeupe, hakika nguo nyeupe ni bora katika nguo zenu na wavikeni sanda maiti wenu kwa nguo nyeupe.
Sunan Abu Dawd vol.2 uk.176, Sunan Tirmidh vol.2 uk.12, Ibn Majah vol.1 uk.449, Sunan Bayhaqi vol.uk.245 kwa maana hii tunakumbusha tena ndugu Waislamu haifai kupoteza mapesa mengi kwa ajili kununulia sanda za thamani kubwa, amesema Mtume [Swalallsahu alaihi wasalam]:- Hakika Mwenyezi Mungu anachukia kwenu ninyi kutokana na mambo matatu:- [a] Porojoporojo [b] Kupoteza mali [c] Kuulizauliza hovyohovyo. Taz. Swahihi Bukhari vol. 3uk 266, Swahihi Muslim vol.5 uk.131, Musnad Ahmad Vol.4 uk.246.

KUHARAKISHA KUMLIPIA MAITI DENI KABLA YA KUSALIWA
Wapendwa Waislamu, yeyote katika sisi akiwa na haki za watu, basi awarejeshee, na ikiwa hana kabisa basi aache wosia kabla ya kufa.
Dalili; Amesema sahaba wa Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] Jabir Bin Abdillah [Radhiyallaahu 'anhu]; Hakika alikuwa Mtume hamsalii mtu mwenye deni, basi inapoletwa maiti kwanza huuliza je ana deni? Masahaba hujibu ndiyo ana deni, kisha anasema Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] msalieni rafiki yenu, akasema sahaba Abu Qatada, deni hilo litakuwa juu yangu,nitamlipia, ndipoMtume akamsalia yule maiti. Swahihi Bukhari hadith namba 2289, Abu Dawud hadith namba 43, Muslim hadith namba 14.

Tukumbuke Waislamu ya kuwa,  ni muhimu sana kuharakisha kumlipia maiti deni lake kutoka katika mali yake na hata kama itatolewa mali yake yote kulipia madeni, ikiwa hana basi ni juu ya dola ya kiislamu kumlipia madeni yake, ikiwa hakuna dola ya kiislamu, inafaa kwa yoyote kujitolea kwa hiyari yake kumlipia madeni maiti.
Dalili; amesema sahaba Abu Hurayra [Radhiyallaahu 'anhu]:- hakika alikuwa Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] inapoletwa maiti ya Muislamu ili amswalie kwanza huuliza je ana deni na ameacha wa kumlipia? Masahaba wakijibu ndiyo kaacha wa kumlipia, ndipo anamsalia maiti huyo. na pakijibiwa hapana hajaacha wa kumlipia basi anasema msalieni rafiki yenu, basi na MwenyeziMungu, alipomkunjulia Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam] Mtume alisema hivi:- mimi nina haki zaidi kwa Waislamu kuliko nafsi zao, na mwenye kufa akaacha deni mimi ndiye nitakayelipa na mwenye kuacha mali basi mali hiyo ni ya warithi wake.
Swahihi Muslim hadith namba 15, Tirmidhi hadith namba 1069, Ibn Majah hadith namba 2407.

DENI NI LA AINA MBILI
Dalili; Amesema Mtume [Swalallaahu alaihi wasalam]:- deni ni la aina mbili, mwenye kufa na hali ya kuwa anayo niya ya kulipa deni , basi mimi ni msimamizi wake, na mwenye kufa na hali ya kuwa hana niya ya kulipa, basi mtu huyo yatachukuliwa mema yake siku ya Qiyama, na haitakuwa siku hiyo kulipa pesa ya aina yoyote ile [Twabaran fil kabir], tunasisitiza wapendwa Waislamu tulipe madeni. siku hiyo yatachukuliwa mema yako na  kupewa mdeni wako, na ikiwa huna mema, basi yatachukuliwa madhambi ya mdeni wako ubebeshwe wewe kisha utupwe motoni.

Itaendelea toleo lijalo InshaAllah

No comments:

Post a Comment