KATIBU Mkuu wa Chama cha wananchi (CUF) Maalim
Seif Sharif Hamad, amesema kuna baadhi ya viongozi ndani ya Zanzibar,
hawafurahishwi na hali ya amani na utulivu iliyoko katika Visiwa hivyo.
Amesema kiongozi anayesajiisha wananchi kukataa umoja na
mashirikiano ya wananchi, anakusudia kuirejesha Zanzibar katika matatizo
na wananchi wake kuishi kwa uhasama na ugomvi kila siku.
Maalim Seif, alieleza hayo katika mkutano mkubwa wa hadhara wa CUF
uliyofanyika jana jioni katika Jimbo la Bububu, nje ya mji wa Zanzibar.
Maalim Seif, alikuwa nje ya Zanzibar, wakati wa kampeni za uchaguzi wa
Jimbo hilo.
Akifafanua hotuba yake Maalim Seif, alisema kuna viongozi ambao
wanawaambia wananchi wakatae mashirikiano ya chini na mashirikiano
yabaki kwa viongozi wa juu, “vipi anawaambia watu kauli hiyo,”? alihoji
Maalim Seif:
“Sikuwepo katika kampeni lakini nimeona kapitia facebook na kila
kitu nakiona lakini niliporudi nikaletewa CD moja kampeni ya ufunguzi wa
kampeni ya CCM na CUF na kuangalia nataka niseme,” alisema na kuongeza:
“Nataka nisema maneno yaliyosemwa pale katika ufunguzi wa kampeni
ile ni kwamba ni dhahiri kwamba watu wale wawili hawaitakii mema
Zanzibar ni dhahiri kabisaaa, vipi wewe kama kiongozi unasema
mashirikiano yabaki huko juu,” alisema na kufafanua zaidi:
“Wananchi kataeni mashirikiano…kataeni chini mashirikiano mashauri
yabaki huko juu tu vipi unawaambia watu kauli hiyo…kama yaliosemwa hivi
eti wale pilau peke yao…kama yalivyosemwa hapa,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif, ambaye pia ni Makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar,
alisema hali ya amani na utulivu iliyopo katika Visiwa hivyo ni kutokana
na wananchi kuchoshwa na kauli za viongozi wasiyoitakia mema Zanzibar
kwa kuwagombanisha.
Alisema Chama chake kinasimamia kwa busara na nguvu zote hali ya
sasa ya amani na utulivu wa Zanzibar, na kufanya hivyo hawana maana
kwamba viongozi wake wanahitaji madaraka bila kuwepo kwa amani miongoni
mwa wananchi wa Zanzibar:
“CUF ikiamua hapakaliki hapa, wewe kiongozi unawaambia wananchi
wakatae mashiriano na yule mwengine yeye anaturejesha katika mapinduzi
kama wao peke yao ndio weneye milki ya Zanzibar, nasema wenye milki ya
Zanzibar ni Wazanzibari wote,” alisisitiza Maalim Seif.
Maalim Seif alisema amesikia maneno ya wanachama wa Chama hicho,
kupitia risala, utenzi na kauli za viongozi wa CUF, zilizotangulia
kutolewa katika mkutano huo na kuahidi hatua zitachukuliwa:
“Nimesikia maneno yenu nimesikia risala, utenzi na maneno yote
lakini nawahakikishia kwamba haya yaliyotendeka ni ushenzi uliofanyika,
hayawezi kupita hivi hivi…hata huko Afrika Kusini hayakufanyika,”
alisema na kuongeza:
“Leo mnakwenda kumshuti mtoto wa miaka 14 hana kosa lolote kisa
nini, kaulizwa kwenu wapi…kasema kwetu Pemba…Dk Shein huu ndio uongozi
unaoutaka? alihoji Maalim Seif.
Maalim Seif alisema katika uchaguzi mkuu wa 2010 askari walikuwa
hao hao, lakini waliambiwa na uongozi uliyokuwepo hawataki fujo,
wanataka nidhamu lakini leo askari wanafanya uhuni:
“Askari ndio hao hao, mbona 2010 ulikuwa na nidhamu kwa sababu
uongozi uliokuwepo, uliwaambia hatutaki fujo tunataka nidhamu lakini leo
askari wanafanya uhuni,” alisema na kuongeza:
“Kwanini 2010 yaliwezekana sasa hivi ishindikane? viongozi wa sasa
wanataka kuturejesha nyuma na mimi nakwambieni hawa wanafanya hivyo kwa
sababu wametishika na umoja wa Wazanzibari,” alisema na kusisitiza:
“Wazanzibari sasa hivi wameungana, sasa walipoona mambo ni magumu
ndio wakatuma watu wao maana siku zote wanataka kutugawa,” alisema
Maalim Seif.
Katibu Mkuu huyo wa CUF, alitoa mfano wa miti na shoka…adui wa miti
ni shoka lakini bila shoka kuwa na mpini wa mti, adui huyo anashindwa
nguvu kuweza kukata miti.
“Hii ni hadithi ya miti na shoka…naijua miti ilikaa ghafla
wakaliona shoka linakuja wakapiga makelele shoka shoka shoka…mzee
akawauliza ndugu yetu yumo? wakasema hayumo, wakaambiwa ondoeni
wasiwasi,” alisema na kufafanua:
“Ghafla akaona shoka linakuja sasa lina mpini mzee akawauliza…ndugu
yetu yumo, wakasema ndio yumo…wakasema mara hii hatuponi. Hakuja Katibu
Mkuu wa CCM kuja kutugombanisha,” alisema na kuongeza zaidi:
“Wala hakuna mwengine Naibu Katibu Mkuu wa CCM hapa kuja
kutungonisha lakini nataka niwaambie waziwazi…hapa tulipofika usiwe na
matumaini kwamba tutarudi nyuma? au mtarudi nyuma,”? alihoji na
kuendelea.
“Mnapambana na mkondo wa maji unataka kusalimika nenda na mkondo na
kama huna kifua utapambana na mabadiliko ya Wazanzibari wanayodai na
yule ambaye anajaribu kupingana na mkondo hufa maji…kwa hivyo hapa
haturudi nyuma…Waheshimiwa kinachogombewa nini? Wazanzibari wanasema
mfumo wa muungano tulionao hatuutaki,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif alisema wakati umefika kwa Wazanzibari kuendesha nchi
yao wenyewe ikiwa na mamlaka ya ndani na nje na yeye ni miongoni mwa
Wazanzibari wanaounga mkono hatua hiyo:
“Wazanzibari wanataka kuendesha nchi yao yenye mamlaka kamili…mimi
binfasi ni muumini wa Muungano wa mkataba,” alisema Maalim Seif.
Alisema kuna baadhi ya watu wakiwemo wanachama wa Chama hicho
wanasema kuwa Kiongozi huyo wa CUF ameleweshwa madaraka na kuwacha
solemba wananchi wa Zanzibar:
“Kama kuna mtu anasema Maalim Seif ana king’ora sijui nini kama
hamjui mimi sio mara ya kwanza kupanda king’ora mie tokea 85,…mie
msimamo wangu unajulikana mimi ni muumini wa muungano wa mkataba,”
alisema na kuongeza:
“Muungano wa mkataba utaturudishia haki zetu Wazanzibari na sasa
hivi tuna Serikali, lakini leo Serikali yetu kila kitu lazima tukapige
magoti Tanganyika,” alisema na kufafanua:
“Tunashangaa kuwa tunashuhudia sote kunatiwa saini baina ya World
Bank na ujenzi wa barabara ya Zanzibar lakini Waziri wetu wa fedha kaa
pembeni…tunataka kurejesha mamlaka kamili, tulikuwa na kila kitu
chetu…tunataka turejee na hali hiyo,” alisema na kusisitiza.
“Tunataka Banki Kuu yetu ya Zanzbar na Tanganyika watakuwa na
yao…halafu tukishapata Muungano wa mkataba Zanzibar huru, Rais wetu
anatoka popote Duniani,” alisema Maalim Seif.
Kiongozi huyo mwenye mvuto kwa wananchi wa Zanzibar, alisema kuna
nchi ndogo kuliko Zanzibar na viongozi wake wanahadhi mbele ya
Ulimwengu, Jumuiya za Kimataifa na Taasisi nyingene, kwanini Rais wa
Zanzibar hathaminiwi:
“Marais wote katika nchi zilizokwenda katika mkutano wa UNESCO
walionekana hata katika nchi ndogo ndogo lakini sisi Rais wetu anatoka
Zanzibar…mmh kama,” aliguna Maalim Seif.
Maalim Seif alisema kufuatia hali iliyojitokeza katika uchaguzi
mdogo wa Bububu, imewaogopesha kutokana na Jeshi la Muungano kusimamia
uchaguzi mdogo uliyochini ya Serikali ya Zanzibar:
“Uchaguzi wa BUBUBU limewaogopesha…leo inakuwaje Jeshi la Muungano
wanasimamia uchaguzi…na cha ajabu hakuna kambi…Maalim anajibiwa ipoooooo
anasema hata ikawepoooo….lakini wana haki gani kuingia katika kituo cha
uchaguzi na silaha nzito nzito,” alihoji Maalim Seif.
Alisema aliwaeleza Wamarekani na Taasisi nyingine kuhusiana na
mchakato wa marekebisho ya Katiba kwamba yanakwenda vizuri na hadi sasa
asilimia 77 wameishauri Tume kuwepo kwa Muungano wa Mkataba:
“Inshallah kwa uwezo wa Mwenyenzi Mungu, Zanzibar itarudi katika
mamlaka kamili…tutaisimamia na mote humo sikutafuna maneno nimewaambia,
Wazanzibari wanachokitaka…nimewaambia wanataka kuungwa mkono na mataifa
makubwa,” alisema na kueleza:
“Nimewaambia kuwa tayari maoni yanachukuliwa na tayari Mikoa miwili
na zaidi ya asilimia 77 wanataka Muungano wa mkataba na Kusini
chake-chake aslimia 75, wanataka Muungano wa Mkataba kwa hivyo
nikawaambia wakubwa hawa haya ndio mawazo ya Wazanzibari,”:
“Wao hawataweka vizingiti kwa Wazanzibari katika kufikia malengo
yao…walituuliza masuali magumu lakini nikawajibu wakatuuliza nyinyi
mnataka mamlaka kamili mtaweza kujiendesha…nikacheka nikawaambia
tunaweza nikawaambia visiwa vidogo vinaweza kujiendesha sisi kwa nini
tushindweeeee wakasema sawa sawa,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif aliwahimiza wananchi wa Zanzibar, kuwa kitu kimoja
katika kutoa maoni yao kwa Tume ya Katiba mpya, ili kusimamia madai ya
nchi yao na waache wasiwasi kwamba Tume hiyo ni ya usanii na kiini
macho.
“Wananchi kama mmekasirishwa na jimbo la BUBUBU lakini muwe makini
kabisa Tume ya Katiba inakuja, mjitokeze mkatoe maoni yenu na msiogope
kitu…ikisha itakwenda Pemba…ni haki yetu kuhakikisha hatuogopi
hatutishwi,” alisema na kuongeza:
“Mimi nasema hayatachakachuliwa na bahati nzuri takwimu zote tunazo
kila shehia watu wametoa maoni vipi kwa hivyo kuna sheria waliotoa,
hivyo Tume haithubutu kutudanganya kwa sababu takwimu zipo..kwa hivyo
nawaomba nyote mkatoe maoni,” alisema Maalim Seif..
No comments:
Post a Comment