Misri kwa mara nyingine tena imeshuhudia maandamano ya wananchi
dhidi ya Marekani. Maelfu ya Wamisri wameandamana mbele ya ubalozi wa
Marekani huko Cairo mji mkuu wa Misri na kuichoma moto bendera ya
Marekani. Wafanya maandamano wametaka pia kufungwa ubalozi wa Marekani
huko Misri na kuondoka balozi wa Marekani nchini humo. Wananchi wa Misri
wamefanya maandamano hayo wakilalamikia kutengenezwa filamu ya
Kimarekani inayomvunjia heshima Mtume Muhammad (s.a.w). Sambamba na
Misri, huko Libya pia baadhi ya waaandamanaji wameuvamia ubalozi mdogo
wa Marekani huko katika mji wa Benghazi ambapo imeelezwa kuwa,
mfanyakazi mmoja wa ubalozi huo raia wa Marekani ameuawa na mwingine
kujeruhiwa. Japokuwa hii si mara ya kwanza kwa Wamarekani kuzivunjia
heshima itikadi za Waislamu, lakini kwa kuzingatia hali maalumu ya sasa
katika eneo la Mashariki ya Kati, baadhi ya duru za kisiasa zinaamini
kuwa, kuchaguliwa kipindi hiki kwa ajili ya kutengeneza filamu hiyo
inayomvunjia heshima Mtume wa Uislamu ni jambo lililoratibiwa na
halikutokea sadfa. Kwa ibara nyingine ni kuwa watengenezaji wa filamu
hiyo inayomvunjia heshima Mtume Muhammad (s.a.w) wamefanya hivyo ili
kuzusha hitilafu na mivutano kati ya nchi za Kiarabu zilizoshuhudia
mapinduzi ya wananchi hivi karibuni. Wataalamu wengi wa masuala ya
kisiasa wanaamini kuwa kwa kuzingatia kwamba idadi kadhaa ya watu wa
kabila la Kibti la Misri wenye misimamo mikali wameshirikiana na Tery
Jones Kasisi wa Kimarekani mwenye chuki dhidi ya dini ya Kiislamu
kutengeneza filamu inayomvunjia heshima Mtume wa Uislamu, lengo la hatua
hiyo ni kuzusha vita baina ya Waislamu na kabila la Kibti la Misri.
Hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya Wakibti wa Misri hawajafurahishwa na
kile kinachojiri sasa katika uga wa kisiasa wa nchi hiyo yaani kuingia
madarakani wanaharakati wa Kiislamu nchini humo. Itakumbukwa kuwa Kasisi
Tery Jones huko nyuma alikabiliwa na wimbi kubwa la malalamiko ya
Waislamu kutokana na kitendo chake cha kishenzi cha kuchoma moto nakala
kadhaa za kitabu Kitukufu cha Qur'ani. Hakuna shaka kuwa, hivi sasa pia
baadhi ya pande zinafanya kila linalowezekana ili kuitumbukiza Misri
katika hali ya mchafukoge na hivyo kunufaika na hali hiyo ya kutokuweko
uthabiti nchini humo. Marekani na utawala wa Kizayuni zinafahamu vyema
kwamba Misri mpya inatofautiana sana na ile ya zama za dikteta Husni
Mubarak, zama ambazo Misri ilikuwa ikifuata kibubusa siasa za Tel Aviv
na Washington. Hii ni kwa sababu tofauti hizo zimeathiri pakubwa maslahi
ya Marekani na utawala wa Kizayuni huko Misri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment