KESI ya jinai inayowakabili viongozi wa Dini wa Jumuiya ya Uwamsho na
Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) imeanza kusomwa upya leo katika Mahakama Kuu ya Zanzibar baada ya maamuzi ya awali kutenguliwa.
Kesi hiyo namba 9 ya mwaka 2012 ilisomwa mbele ya Jaji Fatma Hamid
Mahmoud na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Ramadhan Nassib, ambae
aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Farid Hadi Ahmed (41) mkaazi wa Mbuyuni,
Msellem Ali Mselem (52) mkaazi wa Kwamtipura, Mussa Juma Mussa (47)
mkaazi wa Makadara na Azzan Khalid Hamdan (48) mkaazi wa Mfenesini mkoa wa
Mjini wa Magharibi Unguja.
Wengine ni Suleiman Juma Suleiman (66), mkaazi wa Makadara, Khamis Ali
Suleiman (59) mkaazi wa Mwanakwerekwe, Hassan Bakari Suleiman (39)
mkaazi wa Tomondo, Ghalib Ahmada Juma (39) mkaazi wa Mwanakwerekwe na
Abdallah Said (48) mkaazi wa Misufini mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Washitakiwa wote kwa pamoja walisomewa mashtaka matatu ikiwemo
kuharibu mali, Uchochezi, Ushawishi na kuhamasisha fujo na kosa la
tatu ni kula njama ya kufanya kosa huku kosa la nne likimkabili
mshitakiwa namba nne Azan Khalid ambae anadaiwa kufanya vitendo
vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa Amani.
Makosa yote hayo yandaiawa kufanyika kati ya Oktoba 17,18 na 19 katika
maeneo tofauti ambapo washitakiwa hao walipotakiwa kujibu tuhuma zao
walizikana.
Mara baada ya kuwasomea mashitaka hayo, Mwenesha Mashtaka wa
Serikali,. Nassib alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari
umeshakamilika lakini hata hivyo aliiomba mahakama hiyo kufanya subra
ya kuweza kuamuwa maamuzi yoyote kutokana na upande huo wa mashtaka
kukata rufaa kitendo ambacho alisema kwamba iwapo mahakama hiyo
itaendelea na kesi hiyo kunaweza mahakama ya rufaa ikatoa maamuzi
ambayo yataweza kuathiri maamuzi ya mahakama hiyo.
Kwa upande wa mawakili wa watetezi uliokuwa ukiongozwa na Salim Toufiq, Abdallah Juma na Suleiman Abdallah, uliiomba mahakama hiyo kuwapatia dhamana washitakiwa wake hao hasa ikiangaliwa kuwa tayari washitakiwa hao wameshakaa ndani kwa muda
mrefu.
“Mheshimiwa Jaji tumefurahi kuona kwamba kwa mara ya kwanza upande wa
mashtaka unatamka kuwa upelelezi umekamilika lakini isiwe sababu ya
kuendelea kubakia rumande wateja wetu kwa vile muda wa kukaa kwako
umekuwa mwingi na kupelekea haki yao ya msingi ya dhamana kunyimwa”,
alisema. Toufiq
Hata hivyo Jaji Fatma alisema kuwa atayachukuwa maombi ya pande yote
mbili na kuyapitia kwa umakini ili baadae aweze kutoa maamuzi
yaliyo sahihi kutokana na kuwa ni mgeni wa kesi hiyo na jalada lake
amelipokea kwa muda mchache ambao haukupata nafasi ya kuipitia vizuri.
“Nayachukuwa maombi yote mawili nitayatafakari kwa kina na kuja kutoa
uamuzi unaofaa”, alisema Jaji huyo ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Jaji Mkuu wa Mahakama hiyo aliyemaliza muda wake wa kustaafu mwaka jana.
Katika maamuzi ya Jaji Abraham Mwampashi alisema kesi hiyo inapaswa kuanza kupaya kutokana na kuwa mrajis hana mamlaka na pia kupinga maamuzi ya Mkurugenzi wa Mashtaka DPP kuwanyima dhamana wahutumiwa hao ambao wanakabiliwa na makosa mbali mbali ikiwemo kuhatarisha usalama wa nchi na kuharibu mali za watu binafsi na serikali, hata hivyo serikali ilikata rufaa kupinga maamuzi ya Jaji Mwampashi na kupangiwa jaji Fatma, kesi hiyo ameakhirishwa hadi Machi 27 mwaka huu, .
No comments:
Post a Comment