Tume Huru ya Uchaguzi na
Mipaka ya Kenya (IEBC) imemtangaza Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa kiti
cha rais katika uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa matokeo ya
uchaguzi wa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta mgombea wa kiti cha urais kwa
tiketi ya Muungano Jubilee ameshinda uchaguzi huo katika mchuano mkali
na mpinzani wake Raila Odinga wa mrengo wa Cord. Uhuru Kenyatta amepata
asilimia 50.07 na mpinzani wake wa karibu yaani Waziri Mkuu Raila Odinga
amepata asilimia 43.28 ya kura zote.
Uhuru ni mwana wa Jomo
Kenyatta shujaa wa ukombozi wa Kenya, na sasa anashika hatamu za
kuongoza Kenya baada miaka 50 tangu nchi hiyo ipate uhuru. Uhuru
Kenyatta ameweza kumshinda mpinzani wake mkuu Raila Odinga kwa kumpita
kwa kura laki nane katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 4 mwezi
huu. Mchuano mkali uliokuwepo kati ya wagombea hao wawili uliwafanya
weledi wa mambo watabiri uwezekano wa uchaguzi huo kuingia katika duru
ya pili hapo tarehe 11 mwezi Aprili.
Matokeo ya chunguzi mbalimbali
za maoni pia ambazo zilikuwa zikionyesha tofauti ya kura ya silimia 40
ya Kenyatta na 33 ya Odinga, yalizidisha uwezekano wa kushinda Uhuru
Kenyatta katika uchaguzi huo. Muungano wa vyama vilivyomuunga mkono
Raila Odinga, CORD umesema utakwenda mahakamani baada ya Uhuru Kenyatta
kutangazwa mshindi.
Wakati huo huo serikali ya
Kenya imeimarisha ulinzi na usalama na kutayarisha polisi laki moja ili
kuzuia uwezekano wa kukaririwa matukio ya umwagaji damu kama yale
yaliyotokea katika uchaguzi mkuu uliopita.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa
uchaguzi mkuu wa sasa wa Kenya ni hatua kubwa mbele katika njia ya
demokrasia licha ya dosari za hapa na pale zilizojitokeza katika mfumo
mpya wa kupiga kura kwa njia ya elektroniki.
Katika uchaguzi wa mwaka huu
Raila Odinga alitaka kutekelezwa uadilifu ambao anasema haukutekelezwa
katika uchaguzi wa mwaka 2007. Odinga ambaye anatoka katika kabila la
Luo na anayetambulika kama mzalendo na mwanaharakati wa siku nyingi,
aliendesha kampeni za uchaguzi kwa shaari za "Amani". Hata hivyo
inaonekana kuwa mpinzani wake, Uhuru Kenyatta amefanikiwa zaidi
kuwavutia wapiga kura kwa kutumia nara za "Marekebisho na Mustakbali
Mwema kwa Ajili ya Kizazi cha Vijana". Huenda wapigaji kura vijana
waliona kuwa matarajio yao yanaweza kutimia kupitia ushindi wa Uhuru
Kenyatta mwenye umri wa 51 na si Raila Odinga mwenye umri wa miaka 68.
Alaa kullihal, Uhuru Kenyatta
na mgombea mwenza wake William Ruto wanapaswa kujitayarishwa kwa ajili
ya kujibu mashtaka ya kuhusika na jinai zilizotokea baada ya uchaguzi
mkuu wa mwaka 2007 katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) huko
Hague nchini Uholanzi. Uhuru anawajibika kufika mahakamani tarehe 9
Julai mwaka huu na makamu wake mtarajiwa William Ruto atafika mahakamani
tarehe 28 mwezi huo huo. Uhuru amesema kuwa atashirikiana na mahakama
ya ICC hata kama kesi yake itachukua muda mrefu na kulazimika kuwa nje
ya nchi kwa kipindi kirefu. Suala hilo ndilo lililotumiwa na wafuasi wa
Raila Odinga katika kampeni za uchaguzi wakiwa na matarajio kwamba
lingeweza kuwashawishi Wakenya kumpigia kura kiongozi wao.
No comments:
Post a Comment