Samuel John Sitta, Waziri wa Afrika Mashariki wa Tanzania.
Waziri wa Afrika Mashariki wa
Tanzania Samuel Sitta amependekeza kuwa, Katiba mpya ya Tanzania itaje
moja ya sifa za wagombea Urais kuwa ni uadilifu ili kuwabana watu ambao
wamejilimbikizia mali na wezi kuongoza nchi. Samuel Sitta amependekeza
pia kuwa, Katiba mpya ijayo iweke idadi ya wabunge badala ya kugawa
majimbo kila baada ya uchaguzi, jambo ambalo alisema ni kuwaongezea
ulaji baadhi ya watu. Mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuwa Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesisitiza kuwa,
Katiba ijayo ya
Tanzania inapaswa kutambua haki za kijamii na haki za wengi kuliko
ilivyo sasa ambapo Katiba inatambua haki ya mtu mmoja mmoja. Hayo
yanajiri katika hali ambayo, mchakato wa ukusanyaji maoni kwa ajili ya
Katiba mpya ya Tanzania unaendelea nchini humo. Hivi karibuni Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini Tanzania alijikuta mashakani
baada ya kutoa agizo la kupinga kutolewa baadhi ya maoni na wananchi.
Jaji Mstaafu Joseph Warioba anayeongoza tume hiyo yenye dhima ya
kukusanya maoni kuhusu katiba mpya aliagiza maafisa kutopokea maoni ya
makundi maalumu. Warioba alisema watu watoe maoni yao binafsi bila
kufungamana na makundi yoyote. Hatua hiyo imemuweka pabaya jaji huyo
mstaafu baada ya makundi ya kutetea haki za binadamu kusema kuwa, agizo
hilo ni ukiukaji wa haki ya kujieleza.
No comments:
Post a Comment