Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa
Ufaransa amewataka viongozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Muungano wa
Waasi wa Seleka wahitimishe mapigano na kukaa katika meza ya mazungumzo.
Laurent Fabius ametoa wito pia wa kuundwa serikali ya muungano katika
nchi hiyo ya Afrika ya Kati. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa
amenukuliwa na mtandao wa Intaneti wa wizara hiyo akisema kwamba, kwa
sasa kufanyika mazungumzo baina ya waasi wa Seleka na serikali ya Rais
Francois Bozize wa nchi hiyo ndio njia bora kabisa ya kuupatia ufumbuzi
mgogoro wa nchi hiyo.
Waziri Fabius amewataka waasi na serikali ya
Jamhuri ya Afrika ya Kati kujiepusha na hatua yoyote ile hasa katika mji
mkuu Bangui ambayo inakinzana na roho ya mazungumzo na amani katika
nchi hiyo sambamba na kulinda usalama wa raia. Wakati huo huo, Waasi wa
Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekutana na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika
na kusema kuwa wako tayari kuchunguza pendekezo lililotolewa na Rais wa
nchi hiyo la kushiriki katika serikali ya umoja wa kitaifa. Msemaji wa
muungano wa waasi hao wa Seleka amesema kwamba, hata hivyo lengo lao si
kuingia serikalini bali ni kuwawezesha wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya
Kati kupata maendeleo na kujitegemea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment