Serikali ya Sudan Kusini imetangaza
kuwa, imeanza kuondoa askari wake katika maeneo ya mpaka wake na Sudan,
kwa ajili ya kuanzisha eneo huru kati ya nchi mbili hizo jirani. Ripoti
iliyotolewa jana na serikali ya Juba ilibainisha kuwa, mwisho wa
kuondoka vikosi vya nchi hiyo katika maeneo hayo ya mpakani ni tarehe 4
mwezi ujao wa Februari na kwamba, Sudan Kusini inatarajia kuona Khartoum
nayo inachukua hatua mithili ya hiyo kama njia ya kutekeleza
makubaliano yaliyotiwa saini na viongozi wa nchi mbili mjini Addis Abba,
Ethiopia. Mwezi Septemba mwaka jana na chini ya mashinikizo ya
kimataifa, Sudan na Sudan Kusini zilikubaliana kuondoa vikosi vyao
katika maeneo yanayogombaniwa na pande mbili. Aidha viongozi wa nchi
hizo Omar Hassan al-Bashir wa Sudan na Salva Kiir wa Sudan Kusini,
walikubaliana kuanzisha eneo huru lisilo na askari wa upande wowote,
hatua iliyotajwa kuwa na lengo la kukata uungaji mkono kwa waasi
wanaoendesha harakati zao katika maeneo ya mpakani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment