Afisaa mmoja mkuu wa kundi la
kigaidi la Alshabaab, amefahamisha BBC kuwa kundi hilo ndilo limehusika
na shambulizi dhidi ya duka la kifahari la Westage mjini Nairobi Kenya.
Kwa mujibu wa Afisaa huyo mashambulizi hayo
yalikuwa ya kulipiza kisasi kwa Kenya kwa kujihusisha na vita vya
Somalia ambako wanajeshi wake wanakabiliana na kundi hilo.Afisaa mkuu wa mambo ya ndani Kenya amesema idadi ya waliofariki ni kumi na moja lakini shirika la msalaba mwekundu linasema idadi hiyo imefika watu 30 huku zaidi ya hamsini wakijeruhiwa.
Taarifa kutoka Ikulu ya Rais Kenya zinasema kuwa mshukiwa mmoja aliyekamatwa alifariki kutokana na majeraha yake.
Kundi hilo limesema limekuwa likitoa onyo mara kwa mara kwa Kenya kuwa ikiwa haitaondoa vikosi vyake nchini Somalia, athari zitakuwa mbaya mno.
Kupitia mtandao wao wa Twitter, Al Shabaab limesema kuwa Kenya ilijidai kutosikia onyo hizo, na kuendelea kuwaua waisilamu wasio na hatia nchini Somalia.
Taarifa hiyo ya Twitter ilisema kuwa Shambulio la Westgate ni tone tu katika bahari ya mfano wa yanayowakumba wasomali nchini Somalia.
Taharuki ilianza hii leo saa saba mchana wakati watu wanaokisiwa kuwa kumi walipovamia jengo la kifahari la Westgate la kuwapiga risasi kiholela wakenya waliokuwa wanaendelea na shughuli zao za kawaida.
Kwa mujibu wa shirika la msalaba mwekundu , takriban watu 30 walifariki kwa kupigwa risasi au kutokana na majeraha yao na wengine wengi wenye majeraha ya risasi kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
BBC SWAHILI
No comments:
Post a Comment