Mawaziri wa Mambo ya Nje waEneo la
Maziwa Makuu Barani Afrika wametaka kusitishwa mashambulio dhidi ya
waasi wa M23 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kutoa mwanya kwa
mazungumzo ya amani ya Kampala, Uganda.
Aidha wametaka kikosi cha uingiliaji cha
Umoja wa Mataifa kuwashambulia waasi kutoka Uganda, Rwanda na Burundi
ambao wanaendesha shughuli zao huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kati ya waasi hao ni wale wa FDLR, FNL na ADF.
Hayo yamebainika katika kikao cha
faragha cha wakuu wa ulinzi na mawaziri wa mambo ya nje wa Eneo la
Maziwa Makuu Barani Afrika waliokutana Kampala Jumatano usiku.
Akizungumza baada ya kikao hicho Katibu wa Kudumu wa Wizara ya Mambo ya
Nje wa Uganda Balozi James Mugune amesema machafuko katika eneo
yanapaswa kutatuliwa kwa njia za amani. Leo Alkhamisi Viongozi wa Eneo
la Maziwa Makuu Barani Afrika wanatazamiwa kukutana nchini Uganda
kujadili hali ya Mashariki mwa Kongo. Nchi wanachama wa Kongamano la
Kimataifa la Maziwa Makuu ni pamoja na Angola, Burundi, Jamhuri ya
Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,
Kenya, Uganda, Rwanda, Sudan, Tanzania na Zambia.
No comments:
Post a Comment