Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Sunday, September 29, 2013

Maalim Seif: Katiba bora hutokana na mawazo ya wananchi


Baadhi ya Wazanzibari wanaoishi Tanga wakimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika ukumbi wa Tangamano jijini Tanga, leo tarehe 27/09/2013. 




Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na Wazanzibari wanaoishi Tanga, katika ukumbi wa Tangamano jijini Tanga.
(picha na Salmin Said, OMKR)
 Na Hassan Hamad, OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amesema katiba bora ni ile inayotokana na mawazo ya wananchi, na sio inayotengenezwa na kikundi cha watu au chama cha siasa.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo Mkoani Tanga, wakati akizungumza na Wazanzibari wanaoishi Tanga, ikiwa ni mfululizo wa ziara zake za kuzungumza na Wazanzibari wanaoishi nje ya Zanzibar.
Amesema ili katiba iweze kuwa ya wananchi, haina budi ipitishwe na zaidi ya theluthi mbili ya wananchi, vyenginevyo itafuata matashi ya vyama vya siasa au kikundi kinachojali maslahi yake binafsi.
Maalim Seif ametoa ufafanuzi huo baada ya kuwepo madai ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba yanayolenga kuidhinisha katiba kwa ushindi mdogo wa kura (simple majority).
Ametoa changamoto kuwa duniani kote hakuna katiba iliyopitishwa kwa ushindi mdogo wa kura, na kwamba haitokuwa busara kwa Tanzania kupitisha katiba kwa mfumo huo.
Mapema akizungumza katika mkutano huo, Mwakilishi wa Jimbo la Ole, Mhe. Hamad Massoud Hamad, ametoa wito kwa Wazanzibari wanaoishi Tanga ambao wametimiza masharti ya kujiandikisha, kwenda kujisajili katika daftari la kudumu la wapiga kura wakati utakapofika.
Sambamba na hilo amewatanabahisha Wazanzibari hao kufanya juhudi za kutafuta vijambulisho vya Uzanzibari Mkaazi kutokana na umuhimu waka katika maisha ya kila siku ya Wazanzibari.
Amesema iwapo Mzanzibari atakosa kitambulisho hicho, anaweza kupoteza fursa nyingi zikiwemo utambulisho wake kama Mzanzibari, masomo, hati ya kusafiria na biashara.
Hassan Hamad (OMKR)

No comments:

Post a Comment