Uhusiano
wa kubadilishana nyaraka za Kihistoria kati ya Oman na Zanzibar
unaweza kuwasaidia wananchi wa pande mbili pamoja na watafiti wa
masuala ya Kihistoria kuelewa kwa kina maingiliano ya muda mrefu
yaliyopo kati ya Wazanzibar na Waoman ambayo yanafanana Kisilka na
Kiutamaduni.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa
mazungumzo yake na Ujumbe wa Viongozi sita wa Serikali ya Oman
ulioongozwa na Waziri wa Habari wa Nchi hiyo Dr. Abdulmumin Mansour Bin
Said Al- Hasani aliokutana nao hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi
Seif alisema Zanzibar na Oman zimekuwa na uhusiano wa Kihistoria wa
muda mrefu tokea karne ya 18 ambao umethibitishwa na wataalamu pamoja na
watafiti wa mambo ya Kihistoria kutoka vyuo vikuu tofauti Duniani.
Alielezea
haja kwa Viongozi na Wananchi wa Oman na Zanzibar kuendelea kushikamana
na kushirikiana katika masuala mbali mbali ya maendeleo yatakayosaidia
ustawi wa vizazi vya sehemu zote mbili rafiki.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Serikali ya Oman kupitia
ushirikiano wa mamlaka ya kumbu kumbu na nyaraka ya Oman na Chuo Kikuu
cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } kwa kuandaa Kongamano la Kimataifa la
Ustaarabu wa Kiiislamu kwa Nchi za Mashariki mwa Bara la Afrika.
Balozi
Seif alisema uamuzi huo wa kufanywa kwa kongamano hilo hapa Zanzibar
umekuja wakati muwafaka kwa wataalamu wa mambo ya Kale kubainisha
kwamba Historia ya Uislamu imeanzia hapa Zanzibar.
“
Nimefurahi kusikia kwamba Historia ya Uislamu imeanza Zanzibar.
Inaonyesha watafiti wameliona hili kutokana na asilimia kubwa ya wakaazi
wa Visiwa vya zanzibar kuwa waumini wa Dini ya Kiislamu sambamba na
Utamaduni wake “. Alieleza Balozi Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alishauri tafiti za Wataalamu wa masuala ya
Historia ambazo zitaibuka katika Kongamano hilo zielekezwe zaidi
kunufaisha wananchi na waislamu wa ukanda wote wa Afrika Mashariki.
“
Tafiti hizi za Wataalamu wetu wa Kihistoria itapendeza kama zitaendelea
kubakishwa katika maktaba zetu ili zisaidie wananchi, waislamu na hata
wasomi wetu wa vyuo vikuu vya ukanda wetu wa Afrika Mashariki “.
Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi.
Naye
Kiongozi wa Ujumbe huo wa Serikali ya Oman Waziri wa Habari wa Nchi hiyo
Dr. Abdulmumin Mansour Bin Said Al- Hasani alisema ipo haja ya
kuendelea kuhifadhiwa kwa Historia iliyopo ya Zanzibar na Oman kwa faida
ya vizazi vijavyo.
Dr.
Abdulmumin alieleza kwamba upeo wa tabia za watu wa Oman na Zanzibar
unaolingana ndio unaochangia na kushawishi wageni na watalii wa mataifa
mbali mbali duniani kupendelea kuzitembelea nchi hizi zinazofanana
kiutamaduni.
Waziri
huyo wa Habari wa Oman alifahamisha kwamba Kongamano hilo la ustarabu
wa Kiislamu linalofanyika hapa Zanzibar mbali ya utafiti uliopatikana
lakini pia litafungua uhusiano katika Nyanja nyengine za maendeleo kwa
nchi shiriki.
Dr. Abdulmumin alielezea faraja yake
kutokana na umuhimu wa udugu uliopo kati ya watu wa Oman na Zanzibar
ambao umepelekea waoman wengi kujitokeza kushiriki kwenye kongamano
hilo.
Alifahamisha kwamba ipo ishara ya kuendelea kwa ziara za mara kwa mara kati ya watu wa pande hizo mbili.
Kongamano
hilo la siku tatu linalofanyika katika Hoteli ya Kimataifa ya La Gemma
Della East Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja na kushirikisha Mataifa
yapatayo 17 lina lengo la kuitangaza Zanzibar katika Nyanja za utafiti
na Taaluma Kimataifa.
Hilo
ni kongamano la Pili la Kimataifa la Ustarabu wa Kiislamu kufanyika
likitanguliuwa na lile la mwaka 2012 lililofanyika Nchini Uganda na
kutolewa uamuzi wa kongomano linalofuata kufanyika hapa Zanzibar
kutokana na Historia yake iliyopo sambamba na uhusiano wa karibu
iliyonayo na Mataifa ya Kiarabu.
No comments:
Post a Comment