Kiongozi wa Walio Wengi katika Bunge la Kenya Aden Duale
Nchini Kenya Muungano wa Jubilee umesema mkakati wake wa kuiondoa
nchi hiyo katika mkataba wa Roma uliounda Mahakama ya Kimataifa ya
Jinai (ICC) ni jambo ambalo litaiwezesha nchi hiyo kushughulikia
migogoro yake pasina uingiliaji wa kigeni.Kiongozi wa Walio Wengi katika Bunge la Kenya Aden Duale amesema muungano wa Jubilee unaamini kuwa ICC si mahakama huru na ya kujitegemea kama ilivyokuwa na hivyo kuna haja ya hatua za dharura kuchukuliwa kuiondoa Kenya katika mkataba ulioanzisha mahakama hiyo. Duale amesema asilimia 80 ya watu wote duniani si wanachama wa mahakama hiyo. Ametoa mfano na kusema nchi kama vile India, China na Marekani si wanachama wa ICC. Mbunge huyo mwandamizi wa Kenya amesema ICC inaweza kutumiwa vibaya na haina uwezo wa kutoa maamuzi huru.
Muungano wa Jubilee ambao una wajumbe wengi katika Bunge la Taifa na Baraza la Senate umesema utaongoza mjadala wa Alkhamisi wa kutaka Kenya ijiondoe ICC. Mswada huo umewasilishwa bungeni kabla ya kuanza kesi ya jinai dhidi ya binadamu inayomkabili Rais Uhuru Kenyatta itakayoanza mwezi Novemba na ile ya Naibu wake, William Ruto inayotarajiwa kuanza mwezi huu wa Septemba.
No comments:
Post a Comment