SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuliendeleza na
kulifanya eneo la Michenzani kuwa kituo kikuu cha biashara ikiwa ni
pamoja na kujenga mnara wa kumbukumbu ya miaka 50 ya Mpinduzi ya
Zanzibar.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk. Khalid Salum Mohammed, alisema hayo jana wakati akiwasilisha muongozo mbele ya wahariri na waandishi wa habari katika hoteli ya Ocean View mjini Zanzibar.
Alisema Michenzani itachukua nafasi ya biashara badala ya kituo kikuu kilichokuwa Darajani kuhamishwa kwa kuepusha msongamano wa magari na watu.
Dk. Khalid alisema kivutio kikubwa kitakachokuwepo katika maeneo hayo ni kujengwa kwa mnara utakaokuwa na urefu wa mita 30 utakaogharimu sh bilioni 1.5.
Ujenzi wa mnara huo ulioanza kujengwa unatarajia kukamilika baada ya miezi miwili ambapo gharama za ujenzi zitagharamiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF).
Mnara huo utatoa fursa ya kiuchumi pamoja na ajira kwa vijana kwa kuwepo migahawa na maduka pamoja na vivutio vingine vya utalii ikiwemo sehemu ya mapumziko ya bustani.
Mkurugenzi wa mipango miji, Ramadhani Bakari, alisema azma ya serikali ya kuboresha eneo hilo ni hatua mpya ya kuonyesha mawazo ya mabadiliko ya mji wa Zanzibar, ili kuendeleza azma ya Rais wa kwanza, marehemu mzee Abeid Amani Karume.
Alibainisha kuwa azma ya serikali kupitia mipango miji ni kufanya mji wa Michenzani kuwa mji bora kwa kisiwa cha Unguja na vile vile kufanya mji wa Chake Chake kuwa ni mji bora kwa Pemba.
No comments:
Post a Comment