Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Friday, November 1, 2013

Tanzania yajiondoa vikao vya mawaziri wa EAC


Tanzania yajiondoa vikao vya mawaziri wa EACTanzania imewazuia mawaziri wake wawili kushiriki vikao viwili vya mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa madai kwamba imekuwa ikitengwa na baadhi ya nchi washirika wa jumuiya hiyo.
Kwa mujibu wa mwandishi wa Radio Tehran mjini Dar-es-Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Bernard Membe amezuiwa kwenda Kenya kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje unaoendela nchini humo huku Naibu Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki akizuiwa na serikali asihudhurie mkutano utakaoanza Alkhamisi Oktoba 31 nchini Burundi.
Waziri wa Afrika Mashariki Samuel Sitta ameliambia Bunge kwamba baadhi ya nchi zinaonekana kuwa na shirikisho lao la Afrika Mashariki hivyo hakuna sababu ya mawaziri wake kuhudhuria vikao hivyo kwa sasa.
Waziri Sitta ametoa ufafanuzi huo Jumatano hii bungeni kufuatia mkutano uliofanyika hivi karibuni nchini Rwanda na kuwashirikisha marais wa Kenya, Uganda, Rwanda na Sudan ya Kusini.
Wabunge wa Tanzania walipomtaka Waziri Sitta aseme kwa nini Tanzania isijitoe katika jumuiya hiyo amewataka wawe na subira kwa muda wa wiki mbili wakati wanasubiri majibu ya msingi kutoka kwa sekretarieti ya jumuiya hiyo.
Jumuiya ya Afrika Mashariki inapita katika kipindi kigumu kutokana na kile kinachoonekana ni baadhi ya nchi wanachama kuitenga Tanzania katika baadhi ya mambo. Suala hilo limepelekea baadhi ya  wananchi na wanasiasa Tanzania kutaka nchi yao ijiondoe katika jumuiya hiyo.

No comments:

Post a Comment