Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Saturday, October 27, 2012

DR SHEIN, ENZI ZA WIZARA NDOGO YA KISONGE ZIMEKWISHA, CHONDE CHONDE!



Dr Shein
Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi, Dr Ali Moh’d Shein
Maskani za CCM zinafahamika na kila mwenye kufuatilia siasa za Zanzibar. Ni genge la watu ambao wengi wao hawakupata bahati ya kwenda skuli ambao walikusanywa na utawala wa Dr. Salmin Amour na kujengewa majengo kwa ajili ya kupotezea muda na kushiriki shughuli za siasa za chama hicho. Maskani kuu ni ile inayoitwa KISONGE iliyop
o katika eneo la Michenzani round about. Fikra za kimaskani zote na malengo yake ni sawa na maskani hii kaka ya KISONGE. Lengo ilikuwa ni kuwatumia wanamaskani kama hazina ya kuzalishia nguvu kazi inayohitajika katika hujuma mbali mbali zinazokilenga chama cha CUF, wafuasi wa CUF, wazanzibari wanaoipenda nchi yao, viongozi wa CUF na wazanzibari wenye asili ya Pemba. Genge hilo lilipewa maarifa, ujuzi, mbinu na uwezo wa kutosha ili kutekeleza kwa ufanisi hujuma dhidi ya walengwa. Kwanza kabisa
walikusanywa vyema na kufundishwa hadithi za uongo na propaganda za chuki zilizotungwa na akina Mrina, Mattoke na Maliamkono kwamba waarabu, wazanzibari wenye ngozi nyeupe na wapemba si wazanzibari halisi bali ni wageni waishio kwa ihsani hapa Zanzibar. Elimu hiyo iliyokuwa ikisimamiwa na viongozi wakubwa wa serikali kwa wakati huo akina Mapuri iliwafundisha wanakisonge maarifa kwamba wenyeji halisi wa Zanzibar ni wale wazanzibari wenye ngozi nyeusi na wenye asili ya kibantu (kibara). Ni vyema hapa tuekane sawa kwanza kwamba kutokana na sababu za kihistoria za kiuchumi (si za kisiasa) za enzi hizo sura ya mjengeko wa kiasili na kikabila watu katika jamii za visiwa viwili vya Unguja na Pemba ilitofautiana sana. Kisiwa cha Pemba kilichokuwa zaidi ni kwa ajili ya kilimo cha karafuu ni mjengeko wa jamii yake ulikuwa washirazi (watu wenye asili ya Iran) na waarabu wanafanya asilimia kubwa ukilinganisha na wabantu (wenye asili ya bara) wachache. Kisiwa cha Unguja ambacho kilikuwa zaidi ni cha kibiashara na maofisi ya seikali na makao makuu ya utawala kinaonyesha kuwa na mjengeko wa idadi kubwa ya washirazi na wabantu ikifuatiwa na waarabu na wachache kutoka asili nyenginezo.
Mjengeko huu ulitumiwa vibaya na wakoloni wa kiingereza katika siasa za miaka ya 1960 ya kupigania uhuru kuwagawa wazanzibari wa Unguja na Pemba katika siasa zinazopingana kikabila. Wingi wa watu wenye asili ya kibantu Unguja uliwafanya wanasiasa na watawala wa Zanzibar wa baada ya mapinduzi kuihesabu Unguja kuwa ndio Afika ya kweli na iliyonasibika na mapinduzi ya 1964. Kinyume chake, Pemba kwa kuwa na watu wachache wenye asili ya kibantu ikazingatiwa kuwa mapinduzi ya 1964 hayakuwa yao. Wakati ukweli ni kwamba wazanzibari katika siasa za miaka ya 1960 waligawanyika kwa misingi ya makabila yao na sio kisiwa gani anaishi. Afroshirazi ilikuwepo Pemba na Unguja kama ilivyokuwa kwa ZNP na ZPPP.
Kilichofanywa na kina, Mrina, Mttoke, Maliamkona na Mapuri ni kuwapa wanakisonge picha ya uongo ya Pemba kutokunasibika na ASP na Mapinduzi badala yake kuinasibisha na ZNP (HIZBU) na ZPPP na hivyo kuwajenga wanakisonge waone Pemba na wapemba ni maadui wa Unguja na serikali ya mapinduzi inayotawala hivi sasa. Hata hivyo historia ya ASP na mizizi yake inaonekana kutokukubaliana na uongo huo wa akina Mapuri kwani Pemba ina mchango mkubwa katika uanzishwaji wa ASP pamoja uendelezaji wa chama hicho. Pemba ndio iliyokuwa ngome kuu ya ushirazi. Jumuiya ya washirazi (Shirazi Association) ambayo ni mmoja ya wazazi wa ASP haikuwepo hapo kabla. Kuzuka kwa Jumuiya ya washirazi ni pale washirazi wa Pemba walipokwenda kwa wakoloni kudai uwakilishi wao baada ya kuona Jumuiya ya waafrika (African Association) ilikuwa ikiwawakilisha waafrika wenye asili ya kibantu peke yao. Kama ishavyoelezwa pia hapo kabla kuwa waafrika kutoka bara walikuwa wamejikita zaidi katika kisiwa cha Unguja kuliko Pemba na washirazi walionekana walijikita zaidi Pemba kuliko Unguja, hivyo Jumuiya ya waafrika kuonekana kutokuwa na nguvu za kuwawakilisha washirazi ambao ndio wengi katika kisiwa cha Pemba.
Hivyo washirazi walianza kujikusanya na kuunda jumuiya yao iliyojulikana Jumuiya ya Washirazi, au Shirazi Association. Jumuiya hii ilianzishwa mnamo mwaka 1940 na washirazi huko Pemba. Muasisi wa Jumuiya hii alikuwa Bwana Ali Sharif wa Pandani. Wakati akitoa hoja ya kuanzisha jumuiya hii, Bwana Ali Sharif alimuandikia barua mkuu wa wilaya wa serikali ya kikoloni huko Pemba kwamba kati ya wenyeji 73,000 wa Pemba asilimia kubwa yao walikuwa washirazi. Hivyo basi alifafanua kwamba jumuiya yao ina malengo ya kujaribu kupata uwakilishi wa kitaifa kwa kuwa jumuiya ya waafrika inayotetea maslahi ya watu wenye asili ya kibantu ilikuwa haiwawakilishi watu wa Pemba kwa kuwa watu wa asili hiyo walikuwa wachache huko Pemba .
Jumuiya ya washirazi iliundwa huko Unguja katika mwaka wa 1941 mwaka mmoja baada ya kwisha kuundwa huko Pemba. Sheikh Thabit Kombo muanzilishi wa jumuiya hiyo huko Unguja alimuandikia katibu wa jumuiya ya washirazi Pemba kujiunga na jumuiya yao. Barua hii mpaka leo ipo pale nyaraka za Taifa Kilimani. Maombi hayo yaliambatanishwa na orodha ya wanachama 54 wakiongozwa na Sheikh Ameir Tajo. Hapo baadae baada ya siasa kuanza viongozi wa African Association na Shirazi Association kwa upande wa Unguja walikubaliana na viongozi wa Shirazi Association wa Pemba kuunda chama cha ASP. Hivyo basi akina Sheikh Ali Sharif (mwasisi wa Shirazi associataion) na Sheikh Moh’d Shamte (mwenyekiti wa Shirazi associataion) ndio watu muhimu waliokikaribisha chama cha ASP Pemba na kuitafutia uungwaji mkono. Kwa kiasi kikubwa kutokana na jitihada za watu hao chama cha ASP kilijipatia umaarufu na uungwaji mkono na umma wa wapemba. Haikuwa rahisi kwa Africa association kufanya siasa bila ya kuugana na Shirazi association kwani kwa Zanzibar nzima wazanzibari wenye asili kutoka bara walikuwa 19%, waarabu 17% na washirazi 53%.
Takwimu za uchanguzi mwisho wa mwaka 1963 kabla ya mapinduzi zinaonyesha kuwa ASP ilishinda kwa 44.39 (wakati hivi sasa CCM inapata ushindi wa chini ya asilimia 10) huko Pemba wakati ZNP/ZPPP ilishinda kwa 45.79 huko Unguja. Hii inadhihirisha kuwa ushindi wa ASP ulisababishwa na mjengeko wa makabila katika visiwa viwili hivi na sio upemba na uunguja. Mwarabu, mshirazi, mbantu wote walikuwa na misimamo yao ya kisiasa isiyobadilika bila ya kujali walikuwa Unguja au Pemba.
Uunguja na upemba uliletwa na watawala baada ya kukidharau kisiwa cha Pemba na kukiweka nyuma kimaendeleo kwa miaka mingi tokea mapinduzi ya 1964. Ndio maana ASP ilishinda kwa 44.39 katika mwaka 1963 lakini CCM ilishinda kwa 10% katika uchaguzi wa 2010 kwa sababu wapemba wote waliuchukia utawala bila ya kujali ubantu, uarabu au ushirazi walionao. Hata mzalia cha kibantu kindakindaki ambae anatokana na mizizi ya kiafroshirazi huko Pemba hutamkuta akiunga mkono CCM kwa kuwa nae pia amedharauliwa bila kujali ubantu wake. Baada kupindishwa kwa ukweli huo na kufundishwa hadithi za uongo wanakisonge walijazwa chuki dhidi ya wapemba na wazanzibari wenye asili zisizokuwa za kibantu.
Mabango maalum ya KISONGE yakatengezwa ambayo kazi yake ni kuwatukana wafuasi wa CUF, viongozi wao na watu wenye asili ya kisiwa cha Pemba. Ujumbe wa kila aina wa kuwambia watu hao si wazawa, ni vijukuu vya sultani, ni watoto wa wakoloni, ni mahizbu n.k ulikuwa ukichapishwa katika mabango hayo huku vitendo hivyo vikisherehekewa na SMZ/CCM.
Maskani ya kisonge na nyenginezo ndizo zilikuwa ndio hazina ya kuchagua watu kwa ajili ya askari polisi, jeshi na vikosi vya SMZ. Ajira nyingi za kiaskari zilitolewa kwa wanamaskani ili kuhakikisha nidhamu ya utiifu kwa dola/CCM na chuki dhidi ya wapinzani wa serikali na wapemba inajengewa misingi imara ndani ya idara hiyo. Hapa ndipo askari polisi na askari wa vikosi vyote vya SMZ walipopata nidhamu yao walionayo sasa ya kufanya majukumu yao ya kiaskari kwa kuongozwa na misingi ya chuki na uonevu. Askari polisi au askari wa kikosi anaona fakhari kumshambulia raia bila ya kosa na hata kumuua akigundua tu ndie yule aliyefunzwa kuwa ni adui yake. Askari hawa ndio hao hao tulionao leo eti wanatulinda. Walidhibitiwa kidogo na nguvu ya maridhiano lakini sasa kwa kasi kubwa wanarejea katika misingi yao ya awali baada ya Dr Shein kuanza kuupoteza muelekeo na misingi ya maridhiano hayo.
Maskani ya KISONGE ndio ilikuwa hazina ya kuwaajiri maharamia wajulikanao kama MAJANJAWIRI. Majanjawiri si askari rasmi. Hii ni hatua ya awali kabla hawajawa askari kamili anaevaa sare na kukabidhiwa silaha. Manjawiri wao hutumika kuwavamia watu, kuwapiga kwa na kuwaua kwa kutumia marungu na mapanga ili ionekane sio chombo cha dola kilichotumika kufanya hujuma hizo. Majanjawri wakifanya maonevu zaidi kuliko askari polisi kwani hata askari polisi na askari vikosi baadhi ya wakati huvua sare na kubeba silaha zao na kujiunga na vikosi vya majanjawiri, kushambulia na kuua watu. Hii ndio KISONGE na kazi yake katika siasa na utawala wa Zanzibar ilivyokua. Katika enzi hizo hazina kubwa ya serikali ilitumika kugharamia shughuli za uharamia za watu hawa kwa kulipwa pesa nyingi, vyakula na starehe kadhaa wa kadhaa. Wakati huo huo maeneo mbali mbali yakinyimwa mgao wa huduma za maendeleo kwa fedha nyingi kupotelea katika uharamia huu.
KISONGE ndio hazina ya wapiga kura mamluki. Kura kumi kumi hugaiwa KISONGE siku za chaguzi zinapofika. Mbinu na mafunzo ya kuvuruga uchaguzi kwa kujiandikisha mara nyingi na kupiga kura nyingi hutolewa hapo. Hapa huambiwa kuwa kura zenu kumi kumi zinakwenda kuzuia usultani usirejee Zanzibar na waarabu (wapemba) wasichukue serikali watakuja kuwafagilisha tena waafrika kwa kutumia maziwa yao. Huambiwa kura zenu kumi kumi zitazuia waarabu wasichukue dola wakaja wakawalipizia kisasi kwa kuwachinja na kuwatia katika matanuri ya mbata kama walivyowafanya wao babu zenu huko nyuma.
Alichokifanya Amani Karume na Maalim Seif Novemba 9, 2009 kupitia Maridhiano na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ni pamoja na kulidhibiti kundi la wahafidhina lenye fikra potofu, mafunzo ya kishenzi na misingi miovu ya KISONGE. Azma kubwa ya hili ni kuwafanya wazanzibari waongozwe na uzanzibari wao katika kuishi kwa amani na utulivu katika nchi yao na kuyatafuta maslahi yao. Kuondoka kwa utawala wa Karume imechukuliwa na wahafidhina kua ni sawa na kuirejesha Zanzibar katika mikono yao na mtandao wao ndani ya sura mpya kabisa ya kuwateka nyara washirika wa Maridhiano hayo na serikali ya umoja huo wa kitaifa.
Tayari wamejaribu kumchimba Dr Ali Moh’d Shein aiwachie kamba ya maridhiano ambayo Amani Karume na Maalim Seif waliishika na baadae kumkabidhi Dr Shein aienzi. Amekuwa kwa muda mrefu akishawishiwa kuwateka nyara viongozi wa CUF serikalini na kuwawacha kama wageni waalikwa wa GNU. Lengo ni kuwa viongozi hao wa CUF serikali wabakie hawana sauti yoyote yenye nguvu, si kimaamuzi wala kiushauri. Kundi lililoasisi maridhiano ikiwemo kamati ya watu sita (six comandos) tayari limeshatangaza wazi msimamo wake wa kutaka mabadiliko ya muungano kutoka mfumo na muundo kandamizi uliopo sasa wa serikali 2 kwenda katika muungano wa MKATABA. Katika waasisi wa maridhiano na serikali ya umoja wa kitaifa, ambae hajaweka hadharani msimamo wake huo ni Muadham Amani Karume peke yake.
Baada ya hilo kufanyika kundi la kisonge limejaribu kumteka Dr Shein na kumfanya aamini kuwa wana CCM hawana haki ya kuweka msimamo wa mabadiliko ya mfumo na muundo wa muungano kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sera ya chama chao. Akina Mhe Mansoor na Mzee Moyo ambao ni machampioni wa maridhiano ndani ya CCM wanaendelea kutishwa kwa kauli kali kali, kutukanwa, kufanyiwa vitendo vya kuwakatisha tamaa, na kudharauliwa kutokana na misimamo yao ya kudai mabadiliko ya mfumo wa muungano. Lengo ni kuwatisha na kuwafanya waamini kwamba fikra, misingi, ushawishi na nguvu za KISONGE zimerejea katika safu yake ya awali na zimeshika hatamu upya. Wanavyoamini wahafidhina akina Mhe Mansoor na wenzao watamini kwamba misingi, fikra na nguvu za maridhianao na serikali ya umoja wa kitaifa iliyotandikwa na Amani Karue na Maali Seif bila shaka ishapigwa teke na wao watakuwa woga wa kusimamia misimamo yao ya mabadiliko.
Vitimbi kadhaa wa kadhaa vinavyoendelea dhidi ya harakati zote zinazodai mabadiliko, CUF, UAMSHO, kamati ya maridhiano, akina Mansoor, Mzee Moyo, Amani Karume nk ni suala moja tu, yaani ni vita dhidi ya umoja ambao wazanzibari wanaringia hivi sasa. Hivyo vyote ni visu vinabadilishwa hiki na kile kuhakikisha kuwa kamba hii ya umoja iliyowaweka pamoja na kuwapa sauti moja wazanzibari bila kujali vyama vyao, asili zao, rangi zao wala historia za babu na bibi zao inakatwa ili wasambaratike wasifikie lengo tulilolikusudia na badala yake nguvu ya KISONGE ichukue nafasi yake. Amani Karume aliyapuuza mengi ya Dodoma na maagenti wao waliopo Zanzibar ndio umoja wa wazanzibari ukapatikana na serikali ya umoja wa kitaifa ukaundwa. Aliamua kubakia zaidi kwao Zanzibar kuliko Dodoma. Aliamua kubaki na uzanzibari zaidi kuliko chama chake. Aliangalia maslahi ya Zanzibar na wazanzibari zaidi kuliko maslahi binafsi. Alimpigia debe Dr Shein ili awe rais na amrithishe kiti cha serikali ya umoja wa kitaifa kwa misingi hiyo hiyo ya kuangalia zaidi uzanzibari kuliko Dodoma kwenye chama chao.
Kitu cha kusikitisha sana ni kuona Dr Shein amekubali pole pole kutolewa katika mstari wa uzanzibari na kusogezwa zaidi Dodoma ambako wahafidhina ndiko wanakokuangalia zaidi, ndiko wanakokutegemea na ndiko kuliko na ushawishi na nguvu zao zote. Anajaribu kupokea kila analoambiwa na wahafidhina na kila hila ya kuwaondoa wazanzibari katika agenda yao bila ya kufikiria kwa kina athari yake kwa kuogopa eti wahafidhina ndio waliomueka madarakani. Anajaribu tena kubariki vitendo vya chaguzi za KISONGE, za upigaji kura wa kimamluki, enzi za anjaribu kuunga mkono tena vita ya kuzuia mabadiliko ambayo wazanzibari wanayadai, anajaribu kubariki tena uundwaji wa vikundi vya uharamia na kufanywa vitendo vya uharamia na kuwasingizia wanaharakati wanaodai mabadiliko. Yale yale yaliofanywa Shengejuu Pemba enzi za KISONGE eti wanakijiji waliwavamia askari watatu na kuwapora silaha. Matokeo yake ni kijiji kuvamiwa baada ya kuzuliwa uongo huo, wanakijiji kuteswa, mali kuibwa, wanawake kubakwa na wanaume kukimbilia msituni kwa miezi kadhaa wakiziwacha familia zao na njaa.
Dr Shein anasema kuwa muda wote huo alikua anastahamili tu ila sasa ustahmilivu wake na umefika mweisho. Hii ni kweli kwani mahafidhina kila walipoona wimbi la kudai Zanzibar linakuwa kali humlilia Dr Shein na kumuuliza unafanya nini? Mbona hivi lakini? Mwanzoni aliiogopa serikali ya umoja wa kitaifa na kuheshimu sauti za wanaodai mabadiliko. Baada ya kupoteza muelekeo Dr Shein amehamia KISONGE kwa kutii na kubariki ushauri wa kuvuruga uchaguzi wa Bububu na kuleta tena katika enzi ya maridhiano chaguzi za KISONGE. Amehamia KISONGE na kuamua kutokuheshimu demokrasia na uhuru wa kutoa maoni na kubariki ushauri na uwamuzi wa KISONGE wa kukuwashambulia wafuasi wa UAMSHO na viongozi wao eti kwa kosa la kuweka bayana uovu wa muungano na kuwashawishi watu kuukataa.
Amehamia KISONGE kwa kubariki bila ya hata kukemea matusi dhidi ya Amani Karume, dhidi ya Maalim Seif, dhidi ya Mzee Moyo na dhidi ya wana CUF na wapemba yanayochapishwa wazi wazi katika vipeperushi, maskani za KISONGE na magazeti ya wahafidhina wenye fikra kama za KISONGE. Amehamia KISONGE na kuamua kumfuta uwaziri Mhe. Manssor kwa kosa la kudai muungano wa MKATABA kinyume na fikra ya KISONGE. Amehamia kisonge baada ya kukubali madai ya uongo ya jeshi la Polisi eti kiongozi wa UAMSHO hakutekwa bali alijiteka na hivyo kuamua kuwatia korokoroni viongozi hao wa kidini walioamua kuunga mkono jitihada na harakati za kudai Zanzibar yenye mamlaka kamili.
Tunamwambia na kumtahadharisha Dr Shein, anakurupushwa na kukubali kukurupuka. Sisi wadau wa maridhiano na umoja wa kitaifa tunaoyaheshimu kwa moyo wetu na kuyalinda hayo kwa zetu zote tunataka Dr Shein afahamu sisi ndio tunaostahmilia vitimbi vya KISONGE ndani ya srikali ya umoja wa kitaifa anavyovibariki yeye. Sisi ustahmilivu wetu bado haujafikia kikomo lakini hauko mbali sana. Dr Shein hana budi afahamu kwamba yupo katika serikali mpya inayofuata katiba mpya na misingi mipya ambayo imeasisiwa na watu wawili, Amani Karume na Maalim Seif chini ya timu ya watu sita. Hatukubali hata siku moja kuona Dr Shein unajaribu kupiga teke misingi ya maridhiano na unarudisha misingi ya KISONGE tuliyoikataa. Hivi unadhani askari wako wenye nidhamu ya KISONGE na wale wa kitanganyika watakutosha kukulinda wakati wazanzibari tutakapoamua sote kukabiliana na wewe na utawala wako?
Tunakwambia Dr Shein achilia mbali kuyakumbatia maradhi ya KISONGE. Tumeugua maradhi hayo miaka mingi na mwisho tuliyapatia dawa. Baada ya kuyapa dawa maradhi hayo wazanzibari tumefahamu tutakacho. Si urais wala uwaziri wa SMZ bali ni nchi yetu yenye mamlaka kamili. Wazanibari tumeapa hatuondoki katika kstari huo. Tumeridhia kuwa rais wetu tukiamini utalinda matashi yetu na kuyasimamia kidemikrasia. Si vinginevyo. Tunakutahadharisha sisi haturudi nyuma wala hatutetereki tunazidi kushikamana sote tunaohitaji mabadiliko kuelekea mamlaka kamili ya nchi yetu. Wimbi letu ni kubwa sana, wewe na KISONGE hamna uwezo wa kulishinda. Tafakari kabla ya hayajakukuta ya Mubarrak wa Misri mwaka 2014.

No comments:

Post a Comment