Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Thursday, October 25, 2012

Wiki ya kujibari na taghuti nchini Bahrain

Wiki ya kujibari na taghuti nchini Bahrain
Wananchi wanamapinduzi wa Bahrain wamesema, sambamba na kuonyesha mshikamano wao na wananchi wenzao waliowekewa mzingiro katika mji wa al Akar wanaitangaza wiki hii kuwa ni wiki ya “Kujibari na Taghuti”. Muungano wa Vijana wa Februari 14 umeeleza kwamba katika kuendeleza harakati ya malalamiko ya wananchi wanaitangaza wiki hii kuwa ni wiki ya “Kujibari na Taghuti”. Harakati hiyo imewataka wananchi wote wa Bahrain kutumia suhula zote za kisheria ili kuuondoa mzingiro
katika mji wa al Akar.
Tangu siku ya Alkhamisi iliyopita mji wa al Akar umewekewa mzingiro na vikosi vya usalama vya utawala wa Aal Khalifa. Imeelezwa kwamba vikosi hivyo vimesambazwa hadi kwenye mapaa ya nyumba za mji huo ili kudhibiti nyendo na harakati yoyote ile ya watu. Duru za habari zinaeleza kuwa hali ya kibinadamu ni mbaya katika mji wa al Akar, kwani hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kuingia au kutoka katika mji huo. Ripoti zinaeleza kwamba kitoto kimoja kichanga kimekufa shahidi baada ya askari usalama kumzuia mama yake asiende hospitalini kumnyonyesha mwanawe huyo. Katika tukio jengine mama mmoja mjamzito ambaye alikuwa anahitaji kufayiwa upasuaji naye pia amekufa shahidi baada ya vikosi vya usalama vya utawala wa Aal Khalifa kumzuia asipelekwe hospitalini. Vikosi hivyo vya usalama vinazuia hata madaktari kuingia mjini al Akar.
 Inavyoonekana, utawala wa ukoo wa Aal Khalifa unawaadhibu kwa halaiki wakaazi wa mji wa al Akar. Kupigwa, kutusiwa, kudhalilishwa na kuwekwa kizuizini wakaazi hao wakiwemo wanawake, wanaume na hata vijana wadogo ndio matokeo ya mzingiro unaoendelea kwa muda wa wiki moja sasa dhidi ya mji wa al Akar. Kutokana na hali mbaya na ya kusikitisha inayoendeelea kushuhudiwa katika mji huo, Qasim al Hashimi, mkuu wa ujumbe wa wananchi wa Bahrain uliotumwa kwa jumuiya za kimataifa ametaka Waziri wa Mambo ya Ndani Rashid Abdullah Aal Khalifa apandishwe kizimbani kwa makosa ya kuuwekea mzingiro mji wa al Akar na kupigwa, kutusiwa na kudhalilishwa wakaazi wa mji huo. Amesema, waziri huyo ametumia kisingizio cha mkasa wenye utata wa kuuliwa askari polisi mmoja ili kulipa kisasi cha kuuliwa askari huyo kwa wananchi wa Bahrain wa mji wa al Akar. Al Hashemi amesisitiza kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Jinai inapaswa kumtia nguvuni Rashid Abdullah Aal Khalifa kwa kutenda jinai dhidi ya binadamu. Wakati huohuo mtandao wa habari wa al Wifaq umeripoti kuwa wawakilishi wa makundi na jumuiya mbalimbali za Bahrain hivi karibuni wamemkabidhi barua mwakilsihi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo wakimtaka Katibu Mkuu wa umoja huo Ban Ki-moon atoe uamuzi wa haraka ili kukomesha mzingiro wa kidhalimu na kionevu uliowekewa mji wa al Akar. Na hii ni katika hali ambayo katika kipindi cha siku chache zilizopita wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Bahrain wameelekea mjini al Akar kwa lengo la kuwafikishia misaada wenzao walioko kwenye mzingiro, hata hivyo walikabiliwa na mashambulio ya vikosi vya usalama. Watu kadhaa wamejeruhiwa na wengine wengi kutiwa nguvuni na kupelekwa kwenye korokoro za utawala wa Aal Khalifa katika mapigano kati ya vikosi vya usalama na wananchi madhulumu wa Bahrain. Matukio yote haya yanajiri katika hali ambayo jumuiya za kutetea haki za binadamu duniani zimenyamaza kimya na kufumbia macho ukiukaji wa waziwazi wa haki za binadamu unaofanywa nchini Bahrain, suala ambalo linadhihirisha sura halisi ya jumuiya za kimataifa na ushawishi wa madola ya Magharibi katika maamuzi yanayochukuliwa na jumuiya hizo…/  

No comments:

Post a Comment