VIGOGO watano wa Uamsho wanashikiliwa na
polisi na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo huku Jumuiya hiyo
ikitoa waraka wa kuwataka Waislamu wadumishe amani.
Viongozi hao wako mikononi mwa polisi
tangu juzi wakihojiwa mambo kadhaa likiwemo la kutoweka mmoja wao, Farid
Had Ahmed ambaye ilidaiwa kuwa alikamatwa na polisi kwa siku nne.
Mbali na Farid vigogo wengine wa uamsho
ambao wanahojiwa na polisi ni Amiri wa Uamsho, Sheikh Mselem Ali Mselem,
Naibu wake, Azzan Khalid Hamdan, Mussa Juma na Hassan Bakar.
Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa
Ali Mussa alisema jana kwamba wanawahoji msheikh hao na watawafikisha
mahakamani leo iwapo wataona kuna mashitaka ya kujibu.
Katika hatua nyingine, Uamsho imetoa
waraka kwenye misikiti ya Zanzibar wakiwataka Waislamu wawe watulivu na
kuhudhuria kwa wingi mahakamani leo wakiwa na vitambulisho vya
Mzanzibari Mkaazi.
Waraka huo uliosambazwa unasema hivi:
“Kama hali ilivyo na mnavyosikia mnaombwa muwe watulivu na mufanye subra
na leo (jana) hapo Msikiti wa Mbuyuni hapatakuwa na muhadhara si
Adhuhuri wala Alasiri. Mnachoombwa na viongozi wenu muwe wavumilivu na
watulivu hadi kesho (leo) mufike mahakamani bila ya fujo na muchukue
kopi za vitabulisho vyenu vya Mzanzibari.
“Jingine ni kuwa msikae vikundi na
mkawapa askari sababu, tunasisitiza amani na utulivu na Waislamu ni
wenye kutii amri za viongozi wao. Tunasisitiza amani na utulivu pia
subra na dua kwa wingi . Ukipata taarifa hii mjulishe na mwenzio toa
kopi na uwape wengine. Wabillah taufq.”
Waraka huo ambao ulikuwa unasambazwa katika misikiti jana haukutiwa saini na mtu yeyote wala haukutaja umetolewa na nani.
Wakili wa Uamsho, Salim Tawfik alisema
jana kuwa wateja wake watafikishwa mahakamani leo lakini akalaumu kwamba
Polisi wamewahoji bila ya yeye kuwepo.
“Mimi nilikwenda polisi nikakuta Mselem
anahojiwa nikataka kuingia wakanizuia, wakasema wataniita lakini
hawakufanya hivyo,” alidai wakili huyo.
Hali ya Zanzibar imetulia lakini ulinzi
wa polisi na askari wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
wameimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ya mji huu wakiwa
wanazunguka na silaha mikononi.
Kwa siku tatu mji wa Zanzibar ulikumbwa
na ghasia kubwa kwa askari kupambana na wananchi ambao walikuwa
wakiamdamana wakitaka Sheikh Farid aachiwe.
No comments:
Post a Comment