Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Sunday, October 14, 2012

Katiba mpya, yatingisha Muungano Zanzibar


Tume ya Jaji Warioba yatika Katika Baraza la Wawakilisji Z’bar leo kukusanya maoni.
Wakati mjadala wa Katiba mpya ukiwa umewagawa viongozi wa dini, siasa na serikali, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, (BLW) leo watakutana na Tume ya mabadiliko ya Katiba kutoa maoni yao.
Akizungumza na Wajumbe wa Baraza hilo jana Naibu Spika, Ali Abdalla Ali, alisema kwamba wajumbe na viongozi watapata fursa ya kutoa maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Tanzania juu ya mambo mbali mbali ikiwemo mfumo wa muungano wenyewe.


“Napenda kuwataarifu wajumbe kuwa siku ya Jumapili Tume ya mabadiliko ya Katiba itakuja kusikiliza maoni ya wajumbe kuhusu mabadiliko ya Katiba ya muungano,”alisema Naibu Spika muda mfupi kabla ua kuahirisha Baraza hilo.
Alisema mkutano wa kukusanya maoni utaanza kufanyika majira ya saa 3:00 asubuhi na kuwataka wajumbe kufika kwa muda muafaka.
Alisema Baraza la Wawakilishi linaangalia uwezekano wa mjadala huo kuonyeshwa moja kwa moja na vyombo vya habari kwa manufaa ya wananchi wake.
Hata hivyo kazi ya kukusanya maoni katiba mpya inafanyika wakati viongozi wa serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar (SUK), wakiwa wamegawanyika kuhusu mfumo unaofaa wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Wakati Makamu wa kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad akitetea mfumo wa Muungano wa mkataba, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi na waasisi wa Mapinduzi na Muungano wameuponda mfumo huo na kutetea muundo wa Muungano wa serikali mbili nchini.
Balozi Seif alisema muongozo wa CCM umeweka wazi umuhimu wa kuwa na mfumo wa muungano wa serikali mbili kwa sababu umefanikiwa kudumisha amani na Umoja wa kitaifa kwa wananchi wa Tanzania tangu kuasisiwa Muungano huo mwaka 1964.
Mwaasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Hamid Ameir, alisema wanaotetea mfumo wa muungano wa Mkataba wana ajenda ya siri ya kutaka kuzorotesha muungano na hatimaye kufikia malengo ya kuvunja muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Upande wake Maalim Seif, amekuwa akipigia chapuo mfumo wa muungano wa mkataba wa serikali tatu ambao amesema utasadia Zanzibar kuwa na mamlaka yake kamili katika muungano wa Tanzania.
Maalim Seif Sharif Hamad, aliwaambia wananchi katika mkutano wake wa hadhara kisiwani Pemba mwishoni mwa wiki kuwa Zanzibar imefika wakati kuwa na mamlaka kamili na Tanganyika yenye mamlaka kamili na baadaye nchi mbili ziwe na muungano wa mkataba.
Akishangiliwa na wafuasi wake, Maalim Seif alisema chini ya mfumo muungano wa mkataba Zanzibar iwe na waziri wake mambo ya nje, benki kuu, mahakama ya rufaa, jeshi la polisi, na kiti chake Umoja wa Mataifa, (UN).
Hata hivyo, wananchi katika kisiwa cha Unguja na Pemba wanaendelea kutoa maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba huku suala la mfumo wa serikali mbili likionekana kuchukuwa nafasi kubwa katika mjadala huo.

No comments:

Post a Comment