Kiongozi
wa Jumuiya ya UAMSHO Sheikh Farid Hadi Ahmed kushoto akiwa na wenzake
sita walioletwa Mahakama kuu Zanzibar Vuga wakiwa hawana ndevu na
kufunguliwa mashtaka manne mapya mahakamani hapo yakiwemo kuharibu mali
za watu zenye thamani ya Shl.Milioni 50 na kufanya vurugu za makusudi
zakuhatarisha amani katika nchi
Baadhi ya Askari wa kutuliza fujo wakiwa Mahakama kuu Zanzibar Vuga kwa lengo la kutuliza amani Mahakamani hapo
Baadhi
ya Viongozi wa Jumuiya ya UAMSHO wakiwa wanatoka katika Mahakama Kuu ya
Zanzibar Vuga baada ya kufunguliwa mashtaka manne mapya..
Mawakili
wa Viongozi wa Jumuiya ya UAMSHO Abdallah Juma kushoto na Salim Tawfik
wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu kujitoa kwao siku ya leo
katika kesi hiyo kutokana na usmbufu wanaofanyiwa wateja wao wa
kuhawangaishwa na kukosa kupelekwa Mahakama ya Kwerekwe kwa muda
muafa.Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar
VIONGOZI
wakuu wa jumuia ya uamsho na mihadhara ya kiislamu Zanzíbar (JUMIKI),
wamenyimwa dhamana katika mashtaka mapya waliyosomewa leo katika
mahakama ya mkoa Vuga mjini Zanzíbar.
Hayo
yamefahamika mbele ya mrajis wa mahakama kuu Zanzíbar George Joseph
Kazi, wakati viongozi hao wakiwa na wafuasi wao watano walipofikishwa
mahakamani hapo kwa ajili ya kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Washtakiwa
hao walifikishwa mbele ya mrajis wa mahakama kwa ajili ya kusomewa
mashtaka mapya yaliyowasilishwa na mkurugenzi wa mashtaka Zanzíbar (DPP)
yanayohusiana na matukio mbalimbali ya uharibifu wa mali, uchochezi,
kumficha Sheikh Farid pamoja na la kumtukana Kamishna wa Polisi wa
Zanzíbar.
Katika mashtaka hayo ambayo waliyakana, upande wa mashtaka ulipinga ombi la washtakiwa hao kupatiwa dhamana.
Mbali
na Farid Hadi Ahmed, washtakiwa wengine ni Mselem Ali Mselem, Mussa
Juma Issa, Azan Khalid Hamdan, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali
Suleiman, Hassan Bakari Suleiman na Ghalib Ahmada Omar.
Wote
hao wameshtakiwa kwa makosa ya uvunjaji wa amani, ushawishi wa
kuchochea na kurubuni watu, kula njama pamoja na shitaka la kufanya
kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani lililokuwa likimkabili Azan
Khalid Hamdan pekee.
Washtakiwa
hao waliomba mahakama hiyo, iwapatie dhamana kwa madai kuwa ni haki yao
ya kimsingi kwa mujibu wa sheria na katiba kwani mashtaka
yanayowakabili si miongoni mwa makosa yasiyokuwa na dhamana.
Wakipinga
ombi hilo, jopo la wanasheria wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka wakiongozwa na Raya Issa Mselem, waliiomba mahakama hiyo
isiwapatie dhamana.
Akiwasilisha
hati ya pingamizi hiyo iliyosainiwa na DPP Ibrahim Mzee Ibrahim, kwa
mujibu wa kifungu cha 19 (1) (2) cha sheria za usalama wa taifa sura ya
47, sheria ya mwaka 2002, Raya alifahamisha kuwa, kwa mujibu wa uwezo
aliopewa DPP chini ya kifungu hicho anawafungia dhamana washtakiwa hao.
Alisema
kuwa, sheria hiyo imempa uwezo DPP kumfungia dhamana mshtakiwa yeyote
ikiwa ataona ipo haja hiyo kwa maslahi ya umma.
Akitoa
uamuzi wake baada ya kusikiliza hoja za pande Mbili hizo, mrajis George
Joseph Kazi, alisema kuwa, amelazimika kuwanyima dhamana washtakiwa hao
kutokana na hati iliyowaslishwa na DPP chini ya kifungu cha 19 (1) na
(2) cha sheria za usalama wa taifa sura ya 47 ya mwaka 2002.
Katika
hatua nyengine, mawakili wawili wa washtakiwa hao, Abadalla Juma na
Salum Taufik, walifika katika mahakama hiyo lakini baada ya wateja wao
kushindwa kuwasilishwa kwa wakati hadi saa tano za asubuhi, mawakili hao
walitangaza kujitoa katika kesi hiyo.
Walidai
hatua yao hiyo imetokana na kutokuwepo mashirikiano kati ya pande mbili
hizo, hali inayoonesha kuwepo njama za makusudi zinazofanywa dhidi ya
wateja wao.
Kesi hiyo imeakhirishwa hadi tarehe 7 Novemba mwaka huu.
NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment