TAMKO LA PAMOJA LA KONGAMANO LA KITAIFA LA KUZUNGUMZIA NAFASI YA ZANZIBAR KATIKA MJADALA WA KATIBA MPYA, UKUMBI WA SALAMA, HOTELI YA BWAWANI, TAREHE 06 OKTOBA, 2012
Sisi washiriki wa Kongamano la Kitaifa la Wazanzibari tuliloliitisha kuzungumzia Nafasi ya Zanzibar katika Mjadala wa Katiba Mpya leo hii Jumamosi, tarehe 06 Oktoba, 2012 katika Ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar tunatambua kwamba fursa iliyopo mbele yetu katika Mjadala huu wa Kitaifa ni fursa adhimu ambayo inapaswa kukumbatiwa na kila Mzanzibari Mzalendo katika kuamua Mustakbali wa Zanzibar na watu wake.
Katika kuikumbatia fursa hii, tunatambua, kuheshimu na kuthamini hatua
iliyofikiwa ambapo Wazanzibari kutoka makundi na taasisi tofauti
wameungana na kuja pamoja katika kusimamia na kuendesha harakati zenye
lengo la kuirejesha Zanzibar yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa
itakayofuatiwa na mashirikiano ya Muungano wa Mkataba kati yake na
Tanganyika.
Hata hivyo, tunaelewa pia kuwa zimekuwepo jitihada za makusudi za
kujaribu kuuvunja umoja huu wa Wazanzibari kwa kutumia hoja dhaifu zenye
lengo la kutuondoa katika mstari ili kuzima vuguvugu la Wazanzibari.
Hatua ya leo ya kuwa na wasemaji na washiriki kutoka makundi na taasisi
tofauti ni kudhihirisha kwamba njama za kutugawa tutazishinda kwa njia
za amani na za kidemokrasia.
Kutokana na hali hiyo, ndiyo leo hii tumeamua sisi Wazanzibari tunaotoka
makundi na taasisi tofauti lakini tunaounganishwa na UZANZIBARi na
imani yetu kwamba wakati umefika wa ZANZIBAR kurejesha mamlaka kamili
kitaifa na kimataifa, kutoa tamko LIFUATALO.
KWAMBA umoja wetu ndiyo nguvu yetu na ngao yetu, hivyo tumeamua
kuunganisha nguvu zetu katika kusimamia madai halali ya Wazanzibari na
kwamba tunakataa njama zote za kutaka kutugawa ili kuendeleza mipango ya
wasioitakia mema Zanzibar ya kutaka kuendelea kuidhibiti.
KWAMBA tutaendeleza harakati hizi za Wazanzibari kwa njia za amani na za kidemokrasia.
KWAMBA hatutositisha harakati zetu za amani na kidemokrasia hadi lengo la ZANZIBAR yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa litimie, na kwamba juhudi zozote za kutaka kubadilisha matakwa ya Wazanzibari kwa kuwakisia na kuwakadiria cha kuwapa hazitokubalika. Tunachokisimamia ni HAKI yetu na si OMBI au fadhila kutoka kwa yoyote.
KWAMBA tuna imani na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa
Umoja wa Kitaifa chini ya Raisi Muheshimiwa Dk. Ali Mohammed Shein na
pia tunaimani na viongozi wetu. Na tunaamini Serikali yetu na viongozi
wetu hao ni wazalendo wa Zanzibar na kwamba ridhaa yao imetoka kwa
wananchi wa Zanzibar. Hivyo basi, tunaamini na kuwategemea kuwa kama
wanavyoendelea kutuahidi watasimamia na kutetea matakwa na maamuzi ya
Wazanzibari walio wengi.
KWAMBA tunatoa wito kwa Jumuiya ya kimataifa kufuatilia kwa kina
mchakato wa katiba mpya na kufuatilia matakwa ya Wazanzibari wanayoyatoa
katika mijadala mbali mbali inayoendelea. Tunaitegemea jumuiya ya
kimataifa hatimae iunge mkono matakwa ya Wazanzibari yanayotolewa kwa
njia ya amani na kidemokrasia.
KWAMBA Zanzibar tunayotaka kuiona ni Zanzibar itakayojengwa chini ya misingi YA UHURU, USAWA, DEMOKRASIA, UVUMILIVU, HAKI ZA BINAADAMU, AMANI NA UJIRANI MWEMA, NA YENYE MAISHA YA NEEMA KWA WATU WAKE WOTE.
ZANZIBAR KWANZA
Limetolewa leo
Tarehe 06 oktoba 2012
ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment