skip to main |
skip to sidebar
Matamshi ya Rasmussen juu ya kuondoka mapema vikosi vya NATO Afghanistan
Kuongezeka mashambulizi dhidi ya vikosi vya NATO nchini Afghanistan
kulikopelekea kuuawa askari wengi wa jumuiya hiyo kumesababisha baadhi
ya nchi zenye askari wake nchini humo zitake kuharakishwa kuondoka
vikosi hivyo nchini Afghanistan kabla ya muda uliopangwa. Takwa hili
limezidi kutolewa katika miezi ya hivi karibuni baada ya kushika kasi
wimbi la mashambulio yanayofanywa na maafisa wa jeshi na polisi wa
Afghanistan dhidi ya askari wa kigeni suala lililopelekea makumi ya
askari hao kuuawa. Mashambulizi hayo ambayo yamepewa jina la
‘mashambulio ya ndani’ hadi sasa yamepelekea askari 52 wa NATO
kuangamizwa. Kuhusiana na suala hilo Anders Fogh Rasmussen Katibu Mkuu
wa Shirika la Kijeshi la Magharibi NATO sambamba na kukiri mashambulio
hayo pamoja na kudhoofika morali wa askari wa jumuiya hiyo ameelezea
uwezekano wa kuondoka mapema askari wa kigeni nchini Afghanistan.
Rasmussen amesema, askari wa nchi za Magharibi wanaweza kuondoka
Afghanistan mapema na kabla ya muda uliopangwa, kwani mashambulizi ya
wanajeshi wa Kiafghani ambayo amesema yanahesabiwa kuwa stratejia mpya
ya Taliban yamefanikiwa kudhoofisha morali wa askari wa kigeni. Pia
katika kujibu suala la mashinikizo yanayotolewa ya kutaka kuondoka
haraka vikosi vya jumuiya hiyo Afghanistan Katibu Mkuu wa NATO amesema,
suala hilo linajadiliwa na kufuatiliwa na kwamba katika miezi mitatu
ijayo uamuzi utachukuliwa. Aidha ameongeza kwamba, kuanzia sasa hadi
mwaka 2014 majukumu na kuwepo askari wa NATO nchini Afghanistan
kutategemea hali ya usalama wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, iwapo hali
hiyo haitaimarika, suala hilo litapelekea kuharakishwa kuondoka vikosi
hivyo nchini humo. Katibu Mkuu wa NATO vilevile ameshiria kuuawa askari
zaidi ya 50 wa NATO mwaka huu katika mashambulizi yaliyofanywa na vikosi
vya Kiafghani dhidi ya askari wa kigeni na kusema, suala hilo
limeuwekea doa uhusiano kati ya vikosi vya NATO na askari polisi na
jeshi la Afghanistan kwani mashambulizi hayo yameondoa kabisa uamunifu
kati ya pande mbili.
Marekani na washirika wake wametambua kwamba kuendelea kuwepo kijeshi
vikosi vyao nchini Afghanistan hakuna faida nyingine kwao zaidi ya
kuzidi kushambuliwa na kuuawa raia wa nchi hizo. Wakati huo huo kupungua
bajeti ya askari wa Marekani walioko Afghanistan kumesababisha wapanga
mipango wa Pentagon walazimike kupunguza operesheni za kijeshi za nchi
hiyo hadi kufikia mwaka 2013. Taarifa zinaeleza kuwa, bajeti iliyotengwa
na Marekani mwaka huu wa 2012 kwa ajili ya vita nchini Afghanistan ni
karibu dola bilioni 118 lakini mwaka ujao wa 2013 bajeti hiyo itapungua
na kufikia dola bilioni 89. Kwa mujibu wa mkakati mpya wa Marekani
uliotangazwa mwaka jana na Rais Barack Obama wa nchi hiyo, Washington
imesema kwamba inakusudia kuondoa polepole askari wake nchini
Afghanistan na kuwaachia askari wa Kiafghani jukumu la kulinda usalama
wa nchi hiyo. Lakini pamoja na mipango hiyo ya kubadilisha mikakati
yake, inaonekana kuwa Marekani ina lengo la kuendelea kubakia nchini
Afghanistan kwa sura nyingine kwa mujibu wa makubaliano ya kistratejia
ya kiusalama ya nchi mbili hizo
No comments:
Post a Comment