Tanzania ni muungano wa nchi mbili huru, yaani Tanganyika na Zanzibar. Nchi hizi kila moja ina Serikali yake na uongozi wake. Bila shaka uchumi wa nchi unategemea sana rasilimali zake zikiwemo watu, Utawala bora, na maliasili zilizomo.
Tanzania, ni moja kati ya nchi zenye utajiri mkubwa hapa barani Afrika kwa kuwa na rasilimali kadhaa ambazo hata nchi za wenzetu zilioendelea hazina neema hizo. Cha kusikitisha kabisa juu ya nchi yetu hii ni kuona kila uchao hali ya uchumi inazidi kudorora huku rasilimali zetu lukuki zikifaidisha mataifa mengine makubwa na madogo.
Mfano mzuri umewahi kutolewa na watafiti kadhaa na moja kati ya utafiti ninaoukumbuka zaidi ni ule uliowasilishwa katika chuo kimoja jijini London mwishoni mwa mwaka jana 2011, usemao ‘ Rasilimali za Tanzania, kwa faida ya nani?’. Utafiti huu kama kuna mtu alieuona au kuusikiliza siku ambayo uliwasilishwa basi angeona jinsi gani Serikali zetu zinavyochangia kwa kiasi kikubwa kuiuza na kuibananga nchi yetu bila huruma wala kimeme.
Utafiti huo unabainsiha wazi kuwa rasilimali kama vile mazao ya mbuga zetu za wanyama, migodi, fukwe na ardhi zetu zinamilikiwa na wageni huku nchi yetu ikipata asilimia ndogo sana ya mgao au mapato yatokanayo na rasilimali hizo. Kibaya zaidi utabaini kuwa hata hicho kipato kidogo huwa ni mgao wa wakubwa wenyewe na kwa hivyo hauwanufaishi wananchi kamwe.
Utafiti unaendelea kuivua nguo Tanzania kwa kuweka bayana kuwa baadhi ya viongozi wakuu wa nchi wakiwemo watendaji wakuu wa Serikali ndio hasa wamiliki wa rasilimali hizo za wanachi kwa maslahi yao binafsi. Rejea migodi ya meremeta, Kiwira, kashfa za Richomond na nyenginezo kwa bara. Na pia rejea habari za kuuzwa kwa jengo la nyaraka mambo msiige, Jumba la yatima forodhani, Kuuzwa kwa MV. Mapinduzi, kukodishwa kwa kisiwa kimoja huko Unguja kwa miaka 100, wizi wa Ardhi Pemba, na hoteli kubwa ilioko Wesha huko Chake Pemba, kwa uchache wa mifano hio.
Haya yote yanaeleweka lakini kinachoshangaza zaidi kwa sasa ni kuwepo kwa meli zipatazo tisa za uvuvi za kigeni, huko nje ya Ras Kiuyu, mkoa wa Kaskazini Pemba, ambazo zimekuwa zikijishuhulisha na uvuvi bila kibali na ruhusa yaSerikali zetu mbili. Meli hizi zimekuwa zikivua hapo kwa takribani miaka mwili sasa na hakuna chombo chochote cha ulinzi wala usalama kilichojali kufuatailia uharamaia huu.
Meli hizo kubwa za kigeni zenye zana nzito husogea karibu wakati wa usiku na kuvua na baada ya mapambazuko ya giza la usiku, meli hizo hujiingiza mikondoni (deep seas) kwa kujificha. Kuna wanachi kadhaa ambao ni wavuvi wamethibitisha kuwepo kwa tukio hili na pia tukio hili limeshawahi kuripotiwa kwa Serikali husika na pia kwa vyombo vya habari bila mafanikio yoyote.
Bwana Hamad Ramadhani, mkazi wa Tumbe, ambae ni mvuvi wa siku nyingi wa Jarife, amemuambia mwandishi wa habari hizi kuwa zipo meli zipatazo tisa nje kidogo tu ya Ras Kiuyu ambazo kwa muda mrefu sasa zimekuwa zikivua na bila shaka ni isivyo halalali.
Bwana Ramadhan pia aliongezea kwa kusema kuwa ‘Tumeshawahi kumuita Waziri wa Uvuvi (Bila shaka Hamad Massoud wakati huo) na kumueleza kadhia zinazotukumba sisi wavuvi hapa zikiwemo kero mbali mbali zinazotukabili. Kwanza tulimuomba waziri atusaidie pale ambapo mitego yetu huharibiwa na Chongowe. Na pia tulimwambia kuwa kuna meli kubwa za uvuvi ambazo huvuwa kiasi kikubwa cha samaki na kuifanya bahari yetu kukosa samaki kwa wavuvi wenye zana ndogo ndogo za uvuvi’.
Hata hivyo pamoja na Waziri huyo husika kupewa habari nyeti kama hizo hadi sasa hakuna kilichofanyika na bado suali la kuwepo wavuvi hao wa kigeni wenye zana nzito za uvuvi linaendelea kuwepo huku Serikali zetu mbili zikifumbia macho upotevu huu wa mali za Taifa bila kujali hasara tunayopata kama taifa kwa kupoteza rasilimali hizi.
No comments:
Post a Comment